How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday, 18 February 2008

Bunge lisiwe kapu la makapi

KWANZA simpongezi Rais kwa kulazimika kuvunja na kuunda upya Baraza la Mawaziri ambalo kimsingi si jipya bali lenye viraka.Kama amekwenda dukani kununua nguo, akaja na hii yenye viraka kama majinzi ya watoto wa kihuni wa sasa, nitampongeza kwa lipi?Nilipongeze Bunge, waandishi wa habari na wananchi na kusihi tuendelee kumbana hadi kieleweke.

Nitampongezaje wakati kuna sura kuukuu, tena zenye kulalamikiwa, kama Andrew Chenge, Juma Kapuya na Peter Msola?Chenge analalamikiwa kuizamisha nchi kwenye ubinafsishaji mchafu alipokuwa mwanasheria mkuu wa serikali inayosifika kwa uchafu.Kapuya analalamikiwa kwa matumizi mabaya ya ndege za jeshi na kuwa na biashara ya mgodi huko Arusha, huku Msola akilalamikiwa kwa ufisadi uliofanyika chini yake alipokuwa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), ukiacha kuvurunda kwenye elimu ya juu, hasa mikopo kwa ajili ya elimu ya juu.

Kitu cha msingi alichofanya Rais, nacho kwa kuchelewa ni kupunguza ukubwa wa baraza kutoka 61 na kufikia 47. Hapa tukubaliane, Rais kwa kuendekeza kuwa na mawaziri wengi wasio na kazi wala tija, alilihujumu taifa kwa kuwagharamia maisha yao ghali ilhali hali ya uchumi wetu inazidi kuwa mbaya. Inashangaza uzalendo hasi kama huu kuwa nao kiongozi wa nchi!

Kwa hiyo, tuseme kabisa Baraza la Mawaziri linaloitwa jipya halina jipya kama ilivyo serikali mpya ya awamu ya nne. Litakuwaje na jipya iwapo linapatikana kwa kusukumana na kuumbuana huku likijaa makapi ya utawala uliopita?

Kuna taasisi nyingine inayopaswa kuangaliwa tena kwa jicho kali. Hakuna kitu kinanisikitisha kusikia bunge letu likiitwa tukufu, ingawa kipindi hiki limetutoa kimasomaso liliposimama kidete na kumwajibisha Waziri Mkuu na baadhi ya mawaziri kutokana na ufisadi.

Nasema hivi kutokana na wale waliotimuliwa kwenye uwaziri kubakia ni wabunge. Je, Bunge si taasisi ya umma kama ilivyo 'cabinet'?Inawezekanaje mtu akutwe na hatia kiasi cha kutimuliwa uwaziri ambao ni dili kuliko ubunge, ingawa ubunge ndiyo mtaji, lakini bado abakishwe bungeni?Tunamhukumu kwa lipi na kumvumilia kwa lipi? Ufisadi ni ufisadi na mtu anapotokwa na udhu hana nusu ya usafi wala nusu ya uchafu. Hana udhu. Ni mchafu, hafai kuswali msikitini.

Hivyo basi, kwanza tuseme wazi, watuhumiwa waliolazimika kuwajibika wabanwe zaidi waachie na ubunge. Maana kwa uovu wao, wakiendelea kuwamo bungeni, wata 'influence' kufanyika kwa madudu waliyokwisha kufanya.Wana marafiki na ushawishi mbali na kuwa na kisasi kwa waliowafikisha hapo. Kama mlivyomsikia kwenye hotuba ya kulazimika kujiuzulu, Waziri Mkuu, Edward Lowassa bado anaamini ameonewa na angetaka nasi tuamini hivyo.

Hapa ndipo msisitizo uwekwe; kwa mfano, wanangoja nini wabunge waliotuhumiwa kughushi vyeti, kutoa rushwa na wengine wenye makovu?Watolewe. Hili ni bunge la wananchi, siyo lao. Na kama bunge linaitwa tukufu, basi liwe na sura na sifa ya utukufu, siyo maneno tu.

Na kwa nini wabunge waliovuruga wasukumizwe kwenye majimbo yao wakavuruge zaidi? Hawana udhu hawa. Hawafai kabisa.

Ubunge ni utumishi wa umma. Na Bunge ni taasisi ya umma yenye dhima kubwa ya kutunga sheria na kuidhibiti serikali. Hivyo watolewe na humo bungeni. Nasisitiza.

Kitu kingine muhimu ni kuzingatia kuwa Rais anatawala kwa ridhaa ya umma. Kwa mfano kung’ang’ania kwake baraza kubwa la mawaziri ambalo lilikuwa ni mzigo wa taifa ni kukiuka utumishi wa umma. Ni ufalme usio rasmi; lazima nao ukomeshwe mara moja.

Hapa ndipo umuhimu wa wananchi kuwa wakali unapojitokeza. Kwa mfano, Tanzania inahitaji katiba mpya. Serikali inasema hapana! Je, katiba safi ni ile iliyoridhiwa na umma au serikali?Serikali ipo kwa ajili ya umma. Lakini umma haupo kwa ajili ya serikali. Hivyo basi, katika kupambana na ufisadi, tupambane na ufisadi wa kukatalia kuandikwa katiba upya.

Tukirejea kwa watuhumiwa ambao wengine wamerejeshwa kwenye ‘cabinet’ na Rais kwa sababu azijuazo binafsi, kuna haja ya wadau kushinikiza waondolewe. Tusiwaogope hata kidogo. Kama kigogo kama Lowassa kimefyekwa, hawa ni nani na wana nini? Na isitoshe nchi ni ya wananchi siyo ya rais peke yake.

Kwa nini Rais amekuwa bingwa wa kurudia makosa? Nakumbuka alionywa kuhusu kuteua marafiki, hata kabla hajaunda serikali yake. Lakini kwa kiburi aliwajaza wale wale tena waliokuwa wameishachosha kuanzia utawala wa Mkapa.

Hivi Kikwete, kwa mfano, huwa hasikii watu wasivyotaka hata kusikia jina kama Chenge likitajwa hata kwenye ukuu wa wilaya? Kama hasikii, hivi vyombo vyote vya usalama vya kazi gani? Je, kwa nini Rais anakuwa mbabe na mwenye kibri kiasi hiki?Niliwahi kuandika makala moja mwaka jana juu ya sura inavyoweza kuficha kilichopo nyuma yake, nilimnukuu mwandishi Philip Zambardo kwenye kitabu chake cha 'Effects of Lucifer - Understanding How Good People Turn Evil' (Hardcover), akisema uzuri wa sura unaweza kuficha ukatili hata ubaya wa roho.

Je, sura za baadhi ya watawala wetu ni kichaka cha ujeuri, kiburi hata ukatili? Mbona anatufanyia ukatili kuwarejesha watu ambao licha ya kuwa watuhumiwa wa ufisadi, tuliishawachoka?

Hivi Rais hajui watanzania wamechoka na makapi? Akitaka kujua watanzania ni watu wa namna gani, ajikumbushe jinsi walivyomchukia Lowassa lakini wakawa wanajifanya kumheshimu hata kumpenda wakati si hivyo.Je, Rais anadhani kamchezo kalikotembea ambako imebidi mtu mmoja afe ili wengi wanusurike kanaonekana kukubalika hivyo rais anadhani ataendelea kunusurika hata kwa vitu vilivyo wazi?Huwa siachi kunukuu maneno haya ya Kiingereza: 'Show me your friends I’ll tell you who you are - au nionyeshe rafiki zako nitakwambia wewe ni nani. Au ni yale ya kujuana kwa vilemba kwa Waarabu wa Pemba? Tuhitimishe kutaka taasisi zetu zisiwe vichaka vya waovu, hata kama wanajuana na wakubwa.

Tusisitize. Kurejea kwenye baraza la mawaziri kwa watu kama Chenge licha ya kuwa aibu kwa taifa, ni fumbo ambalo anayeweza kulifumbua ama ni rais au watanzania kuamua kushupaa na kupinga jinai hii ya ubabe na kujuana.



Source:Tanzania Daima Februari 17, 2008.

No comments: