Tarehe 18 Agosti, rais Jakaya Kikwete alipokea ‘ripoti’ ya tume ya kuchunguza kashfa ya wizi wa dola 133,000,000 uliofanyika katika benki kuu ya Tanzania (BOT).
Taarifa ya Ikulu kuhusu makabidhiano hayo ya kimya kimya inaeleza kuwa Kikwete alikabidhiwa ripoti hiyo na mwenyekiti wa timu iliyokuwa inafanya uchunguzi huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.Mbali ya Mwanyika, wajumbe wengine wa kamati hiyo waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea.
Ukimuondoa Mwema, wajumbe waliobaki wanaguswa na tuhuma nyingi tu. Mwanyika anatuhumiwa kutoa ushauri mbaya kwa serikali kwenye zoezi zima la ubinafsishaji sawa na mtangulizi wake Andrew Chenge maarufu kama bilionea wa vijisenti jambo linalochukuliwa kama ni ufisadi.Hosea anatuhumiwa; kwanza, kuiendesha TAKUKURU kwa maslahi yake binafsi ukiachia mbali kuwahi kutumiwa na waliokuwa wakubwa serikalini kuwasafisha wakati kashfa ya Richmond iliyomsomba waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ilipokuwa ikifumka.
Je kupokea taarifa kimya kimya bila vyombo vya habari ni dalili za nini? Je tutakachoambulia ni tofauti na tulichotegemea? Kuna nini nyuma ya pazia? Kwanini rais anaanza kufanya mambo kisirisiri ukiachia mbali kupuuzia miito mingi ya kumtaka apambane na ufisadi? Je hii haiwezi kutafsiriwa kuwa naye ni sehemu ya ufisadi? Maswali ni mengi tu kuliko majibu.
Hebu angalia tungo hii. "Msione ma-gentle men wanapita mitaani wamefunga tai, tayari wengine tumewafilisi, tayari magari, hati za kusafiria na hata nyumba zao zimekamatwa, matajiri wa EPA wana hali mbaya kweli". Huu ni uongo na usanii. Wataje tuwajue na wapelekwe gerezani siyo kuendelea kutanua mitaani.Mbona hii inakinzana na misingi yote ya utawala bora? Kwanini rais ‘anajipiga mtama’? Maana katika maagizo yake ya awali, aliagiza timu hiyo iwe inatoa taarifa kwa umma mara kwa mara juu ya uchunguzi wake baada ya kuiteua na kuitangaza kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Luhanjo, Januri 9, siku tatu baada ya Rais kukabidhiwa ripoti ya awali ya uchunguzi uliofanywa na Ernst & Young. Rais alikabidhiwa na CAG Januari 7.
Ni kitu gani kimemfanya rais kuunyima umma taarifa hii muhimu kabla ‘hajaishughulikia’ ajuavvyo? Kunani hapa? Taarifa kutoka ikulu, ilipobanwa, ielezee ni kwanini rais ameibinafsisha ripoti ya tume zilisema: ‘‘Baada ya (rais) kuwa ameisoma na kuitafakari ripoti hiyo, ataitolea maamuzi katika siku chache zijazo na taarifa rasmi ya maamuzi hayo ya rais itatolewa kwa wananchi."Tulidhani rais aliunda tume ili kutoa fursa kwa wananchi:Kwanza kujua ukweli ni upi baada ya kusumbuliwa na uvumi na utata mwingi juu ya kulindana na kupotosha mambo.
Je hofu ya umma hatimaye imedhihirika?Pili, kutoa mapendekezo yao kwa vile pesa iliyoibiwa ni yao. Rejea maneno ya rais ya kwenye hotuba yake mbele ya bunge. "Kumekuwa na maneno ya hapa na pale, hizi fedha ni za nani, za serikali au si za serikali, hizi ni fedha za watu, hata timu iliponikabidhi ripoti nikauliza, mmepata kiasi gani wakaniambia Sh53 bilioni, nikawauliza mnazo, wakasema ndiyo," alisema na kuongeza:"Niuliza mbona hamjaziwea katika Mfuko Mkuu, wakasema si za serikali, zitakuwa za serikali labda ikizichukua, hadi sasa zipo katika akaunti maalumu hazina".
Ingawa rais amejiridhisha kwa maneno matamu na mengi kuwa amegusa mzizi wa EPA, ukweli ni kwamba bado ni ngonjera, mizengwe, kuhadaana na kulindana kama kawa. Hapa ndipo watanzania wanapaswa kutia akilini kuwa wana kila sababu ya kufikiria kulitaka bunge lim-impeach rais kama mambo yataendelea hovyo kama yalivyo sasa.Sasa nani amempa rais mamlaka ya kuunda tume hapo hapo akawa ni mwenye kusoma mapendekezo yake peke yake kwanaza ili hatimaye kutoa ‘jibu’? Swali kuu linalojitokeza mara kwa mara ni je rais anaogopa au kutaka kuficha nini na kwanini?
Kwa vile bunge letu limeishaunda tume kushughulikia ufisadi na kutenda haki, ingawa siyo muarobaini, basi kuondoa utata na kutoaminiana huku, Bunge liunde tume huru lichunguze kashfa ya EPA upya na kutoa ripoti kwa wananchi ili wajue ukweli ambao wamekuwa wakiungojea kwa muda mrefu.Rais kisheria yuko kusimamia serikali. Haiingii akilini serikali ile ile inayotuhumiwa kushiriki ufisadi ijiundie tume na kujipa ripoti na hatimaye kutoa jibu. Likitoka jibu litakuwa si jibu bali jipu tu lisilotumbuliwa.
Kuna utata mwingine. Waliounda tume ni wateuliwa wa rais. Hivyo, wanafanya kazi kwa niaba ya serikali yake na hata kwa shinikizo na maelekezo ya rais mwenyewe. Wakikuta serikali imekosea hawana ubavu wa kusema hivyo. Rejea tume ya jaji Walioba juu ya rushwa iliyouawa na utawala kidhabu wa Mkapa. Je tutashuhudia mauaji ya tume nyingine karibuni? Kwanini kupoteza pesa na muda wa umma kwenye vitu vya kisanii?Bunge ni taasisi ya wananchi na wabunge wanawakilisha wananchi moja kwa moja bungeni ili kuichungua na kuishauri serikali. Huu ndiyo mgawanyo wa madaraka na utawala bora. Hivyo, kwanza tukubaliane. Kwa kumwamini rais na kumpa madaraka ya kujichunguza tulifanya kosa ambalo rais anazidi kulitumia kutuhujumu kwa mara nyingine. Anayetilia hili shaka arejee rais kushindwa kuwawajibisha watuhumiwa wa ufisadi ambao miongoni mwao ni wajumbe wa tume tuliowataja hapo juu. Hii ni sawa na kumwamini nyani achunguze kesi ya ngedere wakati wote ni wezi wa mahindi.
Akitangaza kuanzishwa kwa uchunguzi huo, Januari 19, 2008, Luhanjo, alisema:"Baada ya (Rais) kuipitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na ya mkaguzi wa nje, yaani, Kampuni ya Ernst and Young, rais amesikitishwa na kukasirishwa na taarifa ya kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti kama vile Benki Kuu.Mbona naye rais anavunja sheria kwa kuwa hakimu, mwendesha mashitaka, mtuhumiwa na wakili wa utetezi? Kinafichwa nini hapa? Je watanzania watafanya uzembe waamini atakachokuja nacho rais? Kilichomsikitisha na kumchukiza ni nini kama anatenda kile kile hata zaidi?
Kwanini tusijifunze kutoka Kenya? Waziri wa fedha, Amos Kimunya, alipotuhumiwa kuiuza hoteli ya kifahari ya Grand Regency na gavana wa banki kuu ya Dr. Joseph Mullei ilipobainika kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika tenda na ajira, waliwasilisha barua ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi na haki itendeke? Tujikumbushe EPA ilipofumka. Rais hakuwataka Gavana wa benki kuu, marehemu Daudi Ballali, waziri wa fedha Zakhia Meghji wala katibu wa wizara mwenye kutuhumiwa moja kwa moja Gray Mgonja wapishe wengine ili uchunguzi ufanyike kwa haki. Na isitoshe, tume ya EPA itamkamata nani iwapo mtuhumiwa mkuu na mwasisi na mtekelezaji wa kadhia hii aliishauawa?
Rais ameshindwa tuseme amekataa kuunda hata tume ya kuchunguza kifo tata cha Ballali!Kwa mujibu wa hotuba ya rais kwa bunge ya tarehe 21 Agosti hii, mafisadi wa EPA wameshinda na serikali imedhihirisha kuwa nao ubia. Rais amepata wapi mamlaka ya kutoa rikizo na upenyo wa 'kuweka mambo sawa' kama yeye siyo mmoja wao?Mwisho, hotuba ya rais aliyoitoa bungeni ilikuwa tupu na aibu tupu. Kwani haijaangalia matatizo ya msingi na kutoa majibu sahihi zaidi ya kuzunguka zunguka kwa maneno ya kuokoteza. Ila wakati umebadilika na watanzania wanapaswa kubadilika kwa spidi ya roketi kama watataka kupata maisha bora kwa kila mtanzania.
Chanzo: Dira ya Tanzania Agosti 26, 2008.
No comments:
Post a Comment