BAADA ya kukabidhiwa ripoti ya WEPA (Wasamehe Epuka Aibu) na wajumbe niliowateua toka kwenye kijiwe chetu wakiongozwa na Mbwa Mwitu, niliona ni vema kuhutubia wanakijiwe wote ili wajue mipango yangu katika kuokoa uchumi wao.
Wajumbe wa kamati ni Jonisoni Mwananyika, Saidia Wema, Dk. Eddie Washea n.k. Ni wanachama watiifu wa chama changu ingawa nyadhifa zao zinawakataza kisheria.
Nilianza.
Ndugu wana kijiwe watukufu, kwanza sitaongelea suala la Muungano na Kijiwe kile cha Makunazini. Nauacha ujifie wenyewe ili tuone. Kama wana kijiwe hamuupendi basi uache ujifie. Kama wakitaka na waende.
Kwanza wana nini iwapo wamekuwa wakinywa kahawa yetu bure ilhali hawana hata mbuni mmoja? Ila wajue nasema. Huko hakutakakalina na namuonea huruma ndugu yangu Karumekenge hamuwezi Madevu. Nawaonyeni sana kwa hili.
Haya mawazo ya kiuhaini ya akina Shehe Muhuna hatawasaidia. Watadhni wanatunyoa sisi leo nao kesho watanyolewa hata kukatwa mashingo. Mazibu yakizibuka sisi hatutakuwapo wala kutoa msaada. Hatutakubali hata wakimbizi watokanao na choko choko na fyoko zao. We waache tu.
Ndugu wana kijiwe, nani ana muda wa kupoteza kwenye mambo ya hovyo kama haya badala ya kuchangamkia ulaji na ziara za nje? Zinalipa. Hamuoni mie na bi mkubwa tulivyochana kinomi nomi?
Najua watu wengi wenu mnangojea kwa hamu nini ntasema kuhusiana na ripoti ya kashfa ya WEPA. Sitaiepa kama EPA.
Kuna watu wasiojua vijiwe vya kisasa vinavyoendeshwa. Wanaohoji kwanini nimepokea ripoti hii kimya kimya na kuamua kuibinafsisha.
Kwanza niwajibu. Mimi ni rais wa kijiwe na mlinichagua wenyewe mkijua nitakuwa na madaraka makubwa karibu na Mungu. Je, ni vibaya kutumia mwanya huu kufanya vitu?
Mgosi Machungi alitikisa kichwa na kupayuka. “Wewe ni msanii husemi ukwei”.
Nasikia sana kejeli zenu. Wapo wanaosema mimi ni msanii. Naungana nao mia kwa mia. Utawala ni usanii. Ni sawa na abracadabra. Unadhani ni mchezo wa kuwaweka watu sawa ukiwaaminisha mambo ni shwari wakati ni tete.
Lazima uwe msanii kweli kweli kufanikisha hili. Wakilala njaa unasema wanashiba. Na bila ya usanii utapata wapi moyo wa kuwasamehe mafisi wanaowahujumu watu? Huu ndiyo utawala.
Nilikoha kidogo na kuendelea. Wapo wanaosema wajumbe wa kamati yangu licha ya kuwa waajiri na wateuliwa wangu, baadhi yao ni watuhumiwa na marafiki zangu. Sasa mlitaka niwateua maadui zangu wanikaange kwa kitu kilicho wazi? Lazima uteue watuhumiwa wanaojua kila kitu ili watakapoondoka wakiri na kusema kila kitu kama ilivyo hapa.
Niaminini haki itatendeka hata kama ni kwa wachache. Haki ni haki bwana na kufa kufaana na isitoshe bila kujuana mambo hayaendi.
Wengine wanasema nimekuwa hakimu, mwendesha mashitaka, wakili wa utetezi, mzee wa baraza na askari wa mahakama. Kwa zengwe kama hili ungekuwa wewe ungefanyaje? Ni nani huyu ajivuaye nguo hadharani tena mbele ya maadui zake? Hekima husema, umdhaniaye ndiye siye na aliyesimama achunge asianguke.
Wataalamu wangu wa masuala ya fedha wakiongozwa na Mstaafu Mkullu waliniambia hii pesa siyo ya serikali.
Ni ya watu. Hata hawa marafiki zangu mnaowaita mafisadi ni watu. Na serikali huundwa na watu. Na serikali yangu ni ya watu na watu wenyewe ni wao. Mimi ni kipenzi cha watu. Hivyo na chaguo la Mungu.
Kwa kuzingatia hili kwa makini sana, natoa msamaha usio rasmi kwa mafisadi hawa. Wasipolipa pesa hii kufikia Desemba 31 2015 watajua mimi ni nani.
Mungu anasema tupigwapo shavu la kulia tugeuze na la kushoto. Pia anasema umpende adui yako yaliyobaki muachie Mungu.
Nimefanya hivi kwa kuzingatia utulivu, mshikamano na amani ya kijiwe. Siwezi kuruhusu jambo dogo kama WEPA kutugawa. Hii amani mnayolingia itapotea na mtanilaumu mimi.
Kabla ya kumaliza mara mzee Ndevu alipayuka. "Amani haipo na kama amani ni nyinyi kutuibia jua mmechelewa tutachenjiana siku si nyingi.”
Sikumjali ingawa ni vidonge tosha.
Niliendelea kupeta.
Wapo wanaoshinikiza niwataje mafisadi. Hata kama sitawataja, ukweli ni kwamba msiwaone waungwana wakijinata na kutanua mitaani, tumeishachukua mali, pasi, hata wake zao.
Mara Makengeza anahanikiza. "Wataje unaficha wa nini kama wewe siyo mwenzao na mmoja wao? Mbona wewe na mkeo ni mafisadi waliokubuhu?" Nyuki mwingine. Sikujibu. Nilijifanya sijaipata hiyo.
Sikumjibu. Kama kawaida yangu nilijifanya kutosikia na kuendelea na hotuba yangu.
Ndugu wana kijiwe. Wapo watu wamekuwa wakinishinikiza nitaje mali zangu na mke wangu. Huu ni utovu wa nidhamu. Hawajui kuwa mali zangu na mke wangu na marafiki zangu ni sehemu ya siri za usalama wa Kijiwe hata taifa?
Nani awezaye kujipaka petroli halafu apite katikati ya moto? Mie si juha kama nyinyi mnaoibiwa mchana mkamtafuta mwizi usiku. Nitakilinda kijiwe changu kwa nguvu zangu zote na kupamba na kupambana na WEPA.
Leo nitajibu hoja zote za wakosoaji wasio na akili timamu. Wapo wanaohoji ni kwanini nimeamua kurejesha pesa ya kashfa ya HAPA kwa mlango wa nyuma bila kufikisha watuhumiwa mahakamani.
Kwanza mnawajua watuhumiwa hao ni watu wa namna gani? Mara Kapende alihanikiza. "Ni wewe mkeo na maswahiba zenu."
Kama kawa sikuhangaika na kujibizana na chizi. Niliendelea kughani bila kujali kama wasikilizaji wanaambua kitu au la.
Kwanza lazima nijisifu kama wana kijiwe mmeshindwa kunisifu. Uchumi wa kijiwe unapaa si kawaida. Ni zaidi ya hata dege la rafiki yangu Luwasha aliyewashwa na kijiwe cha Nonihino.
Nitajisifu sana ingawa wengi wananilaumu eti sisikilizi vilio vya wana kijiwe.
Kwani mimi ni daktari? Mimi ni mkuu wa kijiwe siyo kasisi wala daktari. Wanaoona mambo hayaendi si waende kwa vigagula wakatambikie? Ila naonya. Nendeni kwa vigagula wa madhabahuni na mitaani lakini msiue mazeruzeru.
Nikirejea kwenye kashfa ya HAPA, nimeamuru wajumbe wa kamati waunde akaunti ya IBA (Initial Banking and Auditing) ili kuweza kutunza pesa zitokanazo na jamaa zangu mafisadi.
Hii akaunti ya IBA ni kiboko. Ingawa jina lake ni iba isichukuliwe kuwa ni rahisi kuiba kutoka IBA. Naomba niwahakikishieni kuwa hakuna hata senti moja itakayoibiwa hapa IBA.
Kwa mamlaka niliyopewa na katiba ya kijiwe, naomba nitoe changamoto kwa mafisadi.
Rejesheni pesa yetu kabla sijawa. Nimesahau! Hata hivyo niseme nini iwapo kila kitu kipo wazi mbele za hawa wadanganyika wana kijiwe.
Sijui nani aliwaroga kudhani kuwa kurejesha pesa ni mchezo! Nilijisemea kimoyo moyo na kuendelea.
Ndugu zanguni, nawaomba muelewe. Serikali yangu haina mchezo wala simile na mafisi. Nitawafuata hata huko porini walipo. Nitawasaka hata hawa wa mitaani. Hili wanalijua wazi na ndugu wana kijiwe mnalielewa fika.
Sasa nitakuwa mkali kama mbwa wa getini. Sina mchezo na mtu. Iwapo niliridhia kutimuliwa kwa rafiki yangu Luwashwa nitashindwa nini kuwapatiliza hawa mafisi?
Hata wawe marafiki zangu lazima cha moto wakione. Kabla ya kumaliza zilizuka vurugu kiasi cha kuwa patashika nguo kuchanika.
Wanakijiwe waliniandama kwa mateke na magumi hadi nikajikuta kwenye hospitali ya vichaa ya Muhimbini nikiwa nakodolewa na vichaa waninyotoe roho.
Onyo. Nchi ya Tanzia haipo ingawa inaweza kuwapo na kuwa karibu na kila msomaji. Ila ni kwa wenye bongo siyo bongo lala. Ni kwa wakereka siyo waathirika.
Tuonane 2015 nitakapoanza kuwashughulikia wezi wa WEPA na kutimiza ahadi zangu.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 27, 2008.
No comments:
Post a Comment