BAADA ya kuwa nikisikia habari na matukio ya ufisadi kila siku, niligeuka chizi kwa muda na kuanza kuokota makopo huku nikipayuka hovyo hovyo.
Ndivyo alivyoniambia mshirika wangu wa Bedroom Mama Ndiza. Mwanzoni nilidhani alikuwa akinitania.
Bahati nzuri na yake sikufanya kama yule kichaa wa Muhimbili aliyeachiwa na vichaa waliokuwa wakimtibu awaue vichaa wengine sawa na ufisadi unavyowamaliza vichaa wengine wanaochekelea.
Hebu sikiliza stori yangu na yako ya kutisha na kusikitisha.
Mama watoto anasema eti mara aliniona nikiingia ndani. Alinibomu uchache lau watoto weende cho…shindwa na ulegee. Neno gumu japo la kawaida. Silitaji.
Anasema niliingia homu nikipiga miruzi kama kawaida nikijiandaa kumpa nilizokuwa nimetoka nazo kwenye kubangaiza.
He! Akitegemea ningempa lau gwala, mara nikaanza kupayuka. "We mama nawe fisadi kama wale wafanyakazi ambao wamekuwa wakitishia kuandamana ilhali wanamtishia jamaa nyau. Angalia kila wakitishia kufanya kweli, wakubwa zao wanafanya kweli kwa kudakishwa mishiko nao wanawafanyia kweli wafa kwa ngwamba kwa kuwagawanya."
Eti nilitoa mimacho kama yule bingwa wa zamani wa wanaume wenye shepu na sura mbaya. Mwe! Mara eti nikanena. “Wewe mwanamke. Unataka pesa nikaibe wapi iwapo majambazi wameishazikomba kila kona? Nenda MAWA ukachukue kama kweli hii NGO iko kwa ajili yenu na siyo majizi wakubwa.”
Mama Ndiza naye alijibu bila kujua anajibizana na chizi: “He! Mume wangu, yamekuwa hayo tena! Hujui hizo NGOs ni ulaji wa wake waliochagua madume ya mbegu siyo wewe mchovu?"
He! Nasikia nilitaka kumpa displini kwa kunipa ukweli. Mara kwa vile mama amepanda juu kimakwelini alinidhibiti ile mbaya nami nikaamua kubwaga manyanga kama ambavyo jamaa wamebwaga manyanga kwa mafisadi wa EPA.
Anasema niliendelea kupayuka. “Kaya hii ingekuwa na watu siyo vijitu na mbwa mwitu si tungelianzisha mapema kuliko kujigeuza mapanya na fisi hata wadudu tukigugunana sisi kwa sisi. Hivi we mama unajua kuwa Mtibwa K1 na K2, SPM Mgogolo navyo vimeliwa na hawa mafisi wetu wenye nyadhifa zao? Sasa kwa taarifa yao kama wanakaya wameamua kujisaliti kutokana na woga na uchizi wao basi mimi naenda kuongea na mshirika wangu Osama ili tuwatie adabu. Haiwezekani Kaya ikaendelea kunajisiwa na kidume tena Nabii mzima naangalia. Kama wale mbwa tuliodhania simba wameonyesha umbwa wao basi nami nawaonyesha usimba wangu."
Mama Ndiza alidhania utani eti. Mara niliingia ndani na kuchukua mundu na panga tayari nikatokomea mitaani kuelekea kwenye mitaa ya kina Richmond, TICTS, EPA, ANBEN, Tanpower, Fosnik na gendaeka wengine.
Huwezi kuamini. Eti nilipokuwa nikikatisha mitaa ya Kinondoni nikakuta shangingi moja la kigogo mmoja likiwa linangoja taa ziruhusu nikaanza kulipiga mashoka!
Nasikia waathirika walishikwa na kihoro na kuanza kutoka nduki baada ya kuona kichaa nafanya vitu vyangu.
Eti mke wangu aliyekuwa akinifukuza alisikia nikisema. "Kum…. zenu. Kama Cheka Cheka anawachekea basi mimi siwachekei bali mtacheka na mapanga na mashoka.”
Ajabu siku hiyo hata wale mbwa wakali walinigwaya kwa muda wakitafakari jinsi ya kumuokoa kigogo shangingi wa shangingi na shangingi lake.
Nasikia kwa hasira nilipiga mashoka kama saba hivi mlango ukaanguka na kigogo shangingi akatoka nduki. Ole wake ningempata ningetoa somo kwa waliobakia wajue kuwa sasa ukichaa wangu ndiyo dawa ya ufisadi.
Kwanza niwape stori upya. Unajua kama siyo magazeti kuandika kuwa SPM Mgogolo imegawiwa kwa vijisenti vya Kimarekani milioni moja badala ya milioni 26 zilizokubaliwa ingawa Dk. Silaha anasema thamani yake ni milioni 500 mwenzenu yasingenikuta haya ya kuwa kichaa kwenye utu uzima.
Pamoja na uzee na ustaarabu wangu nasikia siku ile nilipata nguvu za ajabu na ithibati sina mfano. Nasikia nilitoa amri mkuu wa Kaya aachie ngazi kabla sijamfuata huko iku… we koma we.
Nasikia hata wale mbwa wa jamaa walinigwaya na kuona mapwenti niliyokuwa nikimwaga. Nasikia nilisema kuwa mimi nimewahi kula na Raila Odinga chakula cha mchana kwenye ile hoteli aliyoikomboa ya Grand Regency. Eti nilisema kuwa tulisoma wote kule Ujerumani ya Mashariki tulipojifunzia uzalendo na uijinia!
Nasikia eti nilisema kuwa wanakaya wetu ni wavivu wa kufikiri hata kuishi kama alivyosema fisi mmoja mkubwa. Niliwazodoa kwa kuwa mafisadi wa kimawazo wakijiruhusu kufisidiwa na kila fisadi hata wasio na mikia kama akina Richmonduli.
Nasikia nilipaka ile mbaya. Hivi unaweza kuamini kuwa nilitishia kumshitaki mkuu wa Kaya Umoja wa Mataifa kwa kushiriki mauaji ya zeruzeru na vikongwe ili wawatoe makafara kufanikisha ufisadi wao?
Eti nilihoji ukibaka wa lisirikali kwa kukubali kuwadanganya wadanganyika kuwa pesa za EPA zinarejeshwa wakati si kweli.
Yaani eti nilitoa data si kawaida. Nasikia nilijfanya mchumi kiasi cha kusema kuwa uchumi wa Kaya ni mfu maana unaibiwa na kubunguliwa na wadudu watu kila uchao.
Turejee kwenye kubomoa shangingi la shangingi. Eti baada ya kuona fisadi amekimbia nami nilitoka mkuku kuelekea mashariki mwa Kinondoni.
Eti nilipofika maeneo ya Oysterbay ndata walinita mikononi wakaanza kunishushia mkong’oto.
Eti nilisikika nikiwaambiwa kuwa wao ni sawa na nepi zitumikazo kuficha uchafu. Eti niliwapa changamoto kuwa waangalie ufisadi wao na vijimishahara masihara yao. Eti niliwatukana kuwa wanapenda dezo kama maiti kwa kung’ang’ania kupanga ngwala ngwala bila kulipa huku majuha wachache wakitanua kwenye mashumbwengu.
Nasikia bosi wao aliyekuwa na kitambi cha rushwa aliwaamrisha waache kupiga kichaa.
Nasikia aliwalaumu kwa umbwa wao. Eti aliwashauri kuanzia siku hiyo wavunje ndoa yao ya kulinda mafisadi wakati nao ni wachovu.
Kilichomkata makali ni maswali yangu kuwa kama SPM Mgogolo ilinunuliwa kwa dola milioni moja hizi milioni 25 alichukua fisadi gani na alizifanyia nini? Eti nilitaka uchaguzi wa mkuu wa Kaya urudiwe na waliotoa takrima wanyongwe!
Nasikia waandishi wa habari walipokuja kuandika maneno ya kichaa mimi walitimuliwa, ingawa wachache waliyasikia kwa mbali wakaamua kuyarusha.
Eti walizuiwa wasiyaandike maana yangewaamsha waathirika na kujua kuwa wanatapeliwa na kila msanii kama ilivyo kwa wafanyakazi wanaotishia kuandamana wasifanye kweli.
Eti hata wale mashehena wanaotaka shehe mkubwa aachie ngazi nao niliwatolea uvivu. Eti nilisema kuwa kibushuti mmojawapo anayewadanganya ni mrundi na fisadi hakuna mfano. Eti nilimtaja kwa jina Khalifisha Khanisi.
Eti nilisikika nimepandisha mwenembago aliyekuwa anataka atulizwe kwa kunywa damu ya mafisadi. Eti jini wangu alitaka damu ya Tunituni na Cheka cheka kabla ya kuletewa nyama ya Richomonduli.
Nasikia nikiwa nimehanikiza kwa kupayuka mgosi Machungi alikuja haraka na kunivisha tunguli iliyofanya nirejee kwenye hali yangu ya kawaida. Baada ya ndata kujua kuwa kumbe nilikuwa nimepandishwa mashetani na mzuka wa kuchukia ufisadi waliamua kuniachia bila kunifungulia kesi.
Maana nasikia ujumbe wangu uliwachoma kiasi cha kugeuka ghafla kuwa wapiganaji kimoyomoyo.
Baada ya kupoma ndipo nikajua siri ya mbweha wajifanyao kondoo kujizungushia walinzi.
Kumbe wanakimbia ufisadi wao! Wanajua siku moja waathirika wanaweza kupata kichaa cha maisha ya kifisadi na kuwatolea uvivu kama nilivyomtolea uvivu shangingi na shangingi lake.
Eti nilisema nikitoka pale nakwenda kwenye mkoa wa Zenj kumshikisha adabu Karumekenge na wale wanaoleta fyoko wakati kile kipande cha nchi ni kipande na siyo nchi.
wooi nahisi mbavu zinauma kutokana na mavune. Acha niende kwa daktari ila nitakuwa makini nisipasuliwe kichwa badala ya mbavu au kuachwa na machizi wakanidedisha.
Kila la heri.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 20, 2008.
No comments:
Post a Comment