Nilisoma habari ya kuchefua na kutisha kuhusiana na vifo vya mazeruzeru nchini mwetu iliyoandikwa na Vicky Ntetema wa BBC ambaye maisha yake yako hatarini na anaishi kwa kujificha kutokana na kuchukiwa kwa kazi yake.
Siyo siri. Kwa sasa Tanzania ina sifa mbaya kuhusiana na haki za binadamu hasa mazeruzeru na vikongwe wanaouawa kutokana na imani za kishirikina.
Kwa mujibu wa Ntetema ni kwamba mazeruzeru takribani 25 wameishauwa hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Kwanza niwapongeze Ntetema na BBC kwa ujasiri na mapenzi yao kwa haki za binadamu. Wao wameanza. Wengine wafuatie kufichua jinai hii dhidi ya ubinadamu.
Kinachonishangaza na kunisikitisha ni kuona rais wetu akilichukulia suala hili kama la kawaida! Sijamsikia akielezea mikakati ya kupambana na uchafu huu. Kama kawaida yake ya kufanya mambo mazito kuwa mepesi na mepesi kuwa mazito, rais ameonekana akifanya ziara mikoani akila na kunywa na kupewa uzee wa kikabila bila kuchukua hatua mujarabu!
Hii ni nini kama siyo kushindwa kuongoza nchi? Bahati mbaya hata vyombo vya habari vimeshabikia habari za kisiasa kiasi cha kuacha kuvalia njuga janga hili la kuuawa watu wasio na hatia. Kifo cha mtu mmoja Chacha Wangwe na habari za EPA vimechukua nafasi kubwa kuliko zile za maisha ya jamii ya watu fulani katika jamii. Sasa iko wapi dhana nzima kuwa vyombo vya habari ni sauti ya wasio na sauti (The voice of voiceless)? Tubadilike.
Yanatangazwa maandamano Zanzibar ya kumlaani waziri mkuu Mizengwe Pinda kwa tamko lake kuwa Zanzibar si nchi.
Nasikia maandamano ya mashehe wakitaka shehe mkuu ajiuzulu. Yanatangazwa maandamano ya kila aina. Lakini ajabu sijasikia maandamano ya kumshinikiza rais awatendee haki mazeruzeru na vikongwe wanaouawa kwa sababu za kishenzi na kishirikina!
Je zaidi ya kulinda uhai wa binadamu likiwa ni jukumu la kwanza na kubwa kuliko yote, kazi ya serikali ni nini?
Ajabu serikali imeweza kukomesha uwindaji haramu wa wanyama wanaotishia kutoweka kama faru na tembo lakini imeshindwa kuwalinda mazeruzeru? Au ni kwa vile wanyama wanaingiza pesa nyingi zitokanazo na utalii tofauti na mazeruzeru na vikongwe?
Nchi inapofikia kushindwa kulinda uhai wa watu wake basi nchi hii imeharibikiwa na inaelekea kubaya. Leo wachawi wanaua mazeruzeru na vikongwe. Kesho watataka watu wafupi au wenye vipara na kadhalika.
Ingawa mimi siyo mshauri wa rais katika lolote, lakini kama raia wa nchi hii namtaka rais aunde mkakati na kuongoza kampeni kupambana na janga hili dhidi ya binadamu.
Je rais hasomi hizi taarifa za kuchefua juu ya uchafu unaofanyika kwenye nchi yake? Kama anasoma na hachukui hatua, kazi yake ni nini na analipwa kwa lipi?
Ajabu utamsikia rais huyo huyo akijigamba kuwa nchi imetulia. Bado ana mawazo yale yale ya kisiwa cha amani kisicho! Alituahidi maisha bora kwa watanzania. Hata mazeruzeru na vikongwe ni watanzania. Wana kila haki ya kuishi bila kubughudhiwa wala uhai wao kutishiwa na mtu au kikundi chochote.
Tanzania inayoweza kushuhudia na kunyamazia mauaji dhidi ya watu wake haina maana na wanaoiongoza hawana maana kabisa. Juzi waliuawa waliodhaniwa kuwa ni majambazi toka nchi ya jirani ya Kenya. Pamoja na kukabiliwa na makosa ya jinai, serikali ya Kenya ilikuja juu kutaka maelezo. Maana hili ni jukumu la serikali yoyote yenye akili na kujua wajibu wake.
Kadhia ya mauaji ya vikongwe na mazeruzeru ahitaji tambo na lugha za kisiasa balia amri toka kwa rais kusimamisha mara moja jinai hii.
Ntetema ameisharahisisha kazi. Ingawa ni kinyume cha maadili kuwataja sources, inapokuja kwenye haki za binadamu hasa uhai wake, sheria inaweza kupindwa akatoa majina ya wale aliowahoji wakakamatwa na kuhojiwa ili kujua ukubwa wa tatizo na jinsi ya kuushughulikia. Maandili yapo kulinda haki za binadamu.
Watuhumiwa na washiriki wakuu wa jinai hii ni waganga wa kienyeji. Wanajulikana. Ajabu wakati zahama hii ikiendelea, kuna vyombo vya habari hasa magazeti na wakati mwingine radio na runinga zinatoa air times kwao kutangaza upuuzi wao na serikali inaangalia tu!
Hali ni mbaya. Imefikia hata mahali wabunge wanafanya vitendo vya kishirikina bungeni halafu serikali inawaficha! Hawa ndiyo wangebanwa kwanza waeleze ukweli ili kunusuru maisha ya watu wasio na hatia.
Bahati nzuri sana, rais mwenyewe aliishaonja joto ya jiwe ya ushirikina pale Mwanza alipovamiwa jukwaani na kuangushwa. Hivyo kama atakuwa makini basi anajua hatari ya janga hili.
Ajiulize. Kama imeweza kutokea kwake pamoja na ulinzi na wapambe wote, hali inakuwaje kwa watu maskini wasio na ulinzi wala sauti? Au wauawe wanasiasa na waandishi wa habari ndipo rais achukue hatua?
Tanzania imgeuka nchi ya hatari kwa mazeruzeru na vikongwe kuishi. Ingawa wote hatutakuwa mazeruzeru, tutazeeka na kuwa vikongwe. Bahati mbaya wakati ule tutakuwa hatuna ubavu wa kusema wala kutenda.
Nchi yetu iko vitani ingawa haijatangaza. Najua rais ni mwanajeshi. Anajua mbinu nyingi za kijeshi. Kwanini asianzishe kampeni ya makusudi nchi nzima ili kuwanusuru mazeruzeru na vikongwe huku akikomesha jinai hii na kulisafisha jina la Tanzania?
Chanzo kikuu cha ushirikina na tamaa ya mali ni ufisadi. Ufisadi wa serikali kutohoji watu wanavyopata utajiri wao vimejenga mazingira mazuri kwa watu wachoyo na makatili kuwaua wenzao eti kufanikisha biashara na mapenzi. Ni biashara na mapenzi gani halali vinaweza kufanikishwa kwa damu na viungo vya mtu?
Nadhani ni Tanzania pekee ambapo mtu anaweza kuamka na kujitangaza mganga au mchungaji na akatibu au kuhubiri miujiza bila kushughulikiwa. Huu nao ni ufisadi wa kimfumo na kiakili. Leo nchi yenye madaktari na matabibu wengi eti inaridhia watenda miujiza na waganga!
Kuna haja ya kuanza kuachana na ukale. Waganga na wachungaji wa kujipachika lazima wasomee. Bila ya hivyo wasiwe na haki ya kuendesha shughuli zao ambazo nyingi ni mama wa jinai hizi za mauaji.
Bila kubadili mfumo wetu wa mapato na umilki mali watu wengi watapoteza maisha. Ajabu pamoja na rais kuandikiwa makala milioni kidogo ataje mali zake ili na waliomzunguka wafanye hivyo, amezidi kupuuzia na kujifanya hasomi! Huu nao ni mlango mkuu wa ufisadi. Rais anaogopa nini kutaja mali zake kama hazina walakini?
Ntetema anasema viungo vya binadamu vinauzwa kwa shilingi 2,000,000! Ni Tanzania pekee ambapo binadamu anaweza kupangiwa bei na wahalifu na serikali ikaangalia tu huku ikiwaaminisha kuwa itawaletea maisha bora.
Nashauri kampeni za kuokoa vikongwe na mazeruzeru zivuke mipaka ya itikadi na imani. Vyama vyote vya siasa na mashirika ya dini yasimame kidete kuhakikisha jinai hii inakomeshwa mara moja. Na hiki kiwe kigezo mojawapo cha ufanisi wa serikali.
Pia rais aangalie suala la ujinga na umaskini kwa watanzanania walio wengi. Apambane na ufisadi unaoleta umaskini na hatimaye ujinga na wendawazimu wa kuwa na imani za kishirikina.
Wakati wa uongozi wa Mwl Julius Nyerere vitu hivi havikuwepo. Ni kwa sababu hakuna aliyeweza kumilki mali bila kutoa maelezo ya alivyoichuma. Hii ilizuia kuzuka kwa tamaa ya kutafuta pesa kwa kila njia-money by all means illegal and legal.
Kuanzia kazi ya Ntetema itambuliwe na serikali na apewe ulinzi ili aendelee na kazi zake. Bila kufanya hivyo mikono ya Kikwete itaendelea kububujika damu ya mazeruzeru na vikongwe.
Busara ya leo ni toka kwa Tolstoy. "Huwa tunaishi kwa ajili yetu pindi tu tuishipo kwa ajili ya wengeni" Basi tuishi kwa ajili ya vikongwe na mazeruzeru.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 10,2008.
No comments:
Post a Comment