The Chant of Savant

Wednesday 16 December 2009

Jiungeni na CCM hii tuizike CCM ile

KATIKA kuangalia matatizo ambayo taifa letu limeyapata kutokana na usimamizi na uongozi mbovu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuna haja ya kutafuta jibu mjarabu kuondokana na hili.

Wahenga walisema: “Dawa ya moto ni moto”. Hivyo, Watanzania lazima tuanze kufikiria kubadili Katiba yetu ili kuweza kujikomboa na kulikomboa taifa letu.

Hapa ndipo CCM ya pili yaani “Change the Constitution Movement” inapokuja akilini.

Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 licha ya kuandikwa na kuwa ya chama kimoja, imepitwa na wakati na ni ya hovyo ukiachilia mbali historia yake kuwa ilitokana na ya kikoloni.

Kibaya zaidi, inampa rais madaraka makubwa, kiburi na kishawishi cha kufanya atakavyo kwa maslahi yake na kikundi cha watu wachache waliomzunguka. Ni Katiba inayopofusha na kuua moyo wa uadilifu na uchapakazi.

Hata huu ufisadi sugu unaotusumbua, kwa kiasi kikubwa, umechangiwa na Katiba hii. Fikiria kwa mfano, rais kupewa madaraka makubwa kupita kiasi kufikia kuwa juu ya sheria utadhani ni Mungu. Kwa Katiba ya sasa, rais wetu mungu mtu ni mfalme ambaye hakosei wala kuwa na udhaifu.

Kwa Katiba hii viraka, rais wa Tanzania hana tofauti na mfalme Abdullah wa Saudia ambaye anaweza kuweka pesa ya mapato ya taifa kwenye akaunti yake na kutumia apendavyo.

Ingawa rais wa Tanzania hufanya hivyo kwa njia tofauti, mwisho wa siku, huuibia na kuinyonya nchi. Hebu fikiria wateule wa rais ambao wengi ni washirika, vibaraka na marafiki zake wanakomba pesa kiasi gani kila mwezi toka kwenye kodi yako kwa kutofanya lolote zaidi ya kumtumikia kwa maslahi binafsi na kujikomba?

Si uzushi. Mapato yetu mengi yanaishia kuwalisha watawala na mawakala wao. Ndiyo maana pesa nyingi ya bajeti huishia kwenye shughuli za utawala usioleta maendeleo.

Hebu rejea rais kuunda serikali kubwa bila sababu na kupuuza miito ya kutaka aipunguze.

Juzijuzi baadhi ya mawaziri wa serikali hiyohiyo kubwa isiyo ya lazima waligundulika kughushi vyeti vyao na rais Mfalme-Muungu Mtu hakuwachukulia hatua na hajavunja sheria Kikatiba ingawa wahusika walitenda makosa ya jinai.

Kwa nini ana uchungu nao kuliko umma? Jibu ni rahisi. Wao ni washirika na vibaraka wake ambao uwepo wao serikalini ndiyo usalama wake.

Kwa kuwa na hawa hata asipotimiza wajibu wake nani atamgusa iwapo anao wawezeshaji?

Rejea alivyoambiwa awawajibishe mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, au Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyepita, Johnson Mwanyika, kutokana na kushukiwa nyuma ya ufisadi na asifanye hivyo na hakuna kinachomtokea. Je, huyu hajawa mfalme?

Kwa katiba ya sasa, rais ni kikwazo nambari moja cha maendeleo na ustawi wa jamii. Maana hana tofauti na gavana wa kikoloni aliyesimamia unyonywaji wa nchi ambapo mali na pesa ya kodi zilipelekwa kwao sawa na rais wa sasa anavyowafanyia wawekezaji uchwara waliotamalaki nchini mwetu wanaotorosha utajiri wetu chini ya usimamizi wake na asichukuliwe hatua!

Angalia jinsi Katiba inavyotoa kinga dhidi ya mashtaka kwa marais wezi wastaafu.

Yaani hata baada ya Benjamin Mkapa, mkewe, watoto na washirika zake kuwekeza kwenye mazingira tatanishi kwa kuitumia Katiba, hatujashtuka na kufanya jambo la maana!

Yaani hatujashtuka kutokana na rais wa sasa kuendelea kuwatumia na kuwakumbatia mafisadi kiasi cha kugeuka mtumwa kama alivyowahi kusema kada maarufu wa CCM mzee Joseph Butiku?

Huyu, chini ya Katiba ya sasa, akitaka, anaweza kutumia vibaya madaraka yake kama mtangulizi wake na Katiba itamlinda kama ilivyofanya kwa Mkapa.

Na hapa ndipo kiburi cha mafisadi na Mkapa kilipo. Hapa ndipo upuuzi wa kutaka jopo la majaji lichunguze Richmond upya ili kumnusuru mtu mmoja mshirika na kibaraka wa rais ulipo.

Katiba yetu inampa rais, hata mkewe, kibali cha kufanya na kushiriki uhalifu hasa kulihujumu taifa bila kufikishwa mahakamani. Hapa ndipo siri ya wake za marais kuchangamkia usasi wa ngawira kupitia NGO zao uchwara.

Angalia rais anavyojifanyia atakavyo bila kuweza kuzuiliwa. Rejea kufanya ziara kila uchao ughaibuni akitumia mabilioni ya fedha za walipa kodi huku akikwepa matatizo ya ndani na tusiweze kufanya lolote kisheria.

Kimsingi Katiba ya watawala inayoitwa yetu imetugeuza mateka na watumwa wa rais na watu wake. Katiba ya sasa imeiba na kuuza uhuru na utu wetu.

Tunaweza kujidanganya kuwa sisi ni jamhuri kwa maana ya kuwa huru. Hatuko huru chini ya Katiba hii.

Kwa Katiba ya sasa, kama ilivyotekea hivi karibuni nchini Uganda, rais anaweza kumteua mkewe kuwa balozi, mbunge hata waziri kama Yoweri Museveni alivyomteua mkewe kuwa waziri kwenye serikali yake na Katiba ya Uganda isifanye kitu kwa sababu haikuvunjwa.

Hapa ndipo ilipo siri ya rais kujaza vibaraka wake kwenye nafasi nono. Anajua udhaifu huu wa Katiba na anautumia vilivyo. Na anayebishia hili aangalie mashindano ya vigogo kuwajaza watoto wao kwenye nyadhifa nono kila mahali.

Hii ni nini kama siyo kujenga tabaka tawala litokanalo na watawala wa zamani! Na hii ndiyo siri ya kuanza kuzuka majina ya watoto wa vigogo wa chama kujirudia kwenye safu za juu chamani na serikalini.

Katiba nyingi za nchi za Kiafrika ni za kijambazi ambapo madikteta na wezi huitumia kuwapa ulaji watu wao. Rais wa sasa wa Gabon (Ali Ben Bongo) na Faure Eyadema walikuwa mawaziri kwenye serikali za baba zao kutokana na kuwa na katiba uchwara na dhalimu kama yetu.

Nchini Libya, imla Muamar Gadaffi anamuandaa mwanaye, Saif al Islam, huku nchini Misri Hosni Mubaraka akimuandaa Gamal kuchukua madaraka baada yao huku rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika, akimuandaa mdogo wake, Said Bouteflika, kuchukua nafasi yake.

Kwa kutumia katiba hizi hizi za kihuni nchini Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali anamuandaa mkwewe, Sakhr el-Materi kumrithi. Na kwa Tanzania tunavyokwenda na uroho wa madaraka unavyozidi kuumka, tusipogutuka, kuna siku upuuzi huu utafanyika nchini mwetu tukiangalia. Maana hawa wanaoufanya kwa kiwango hiki walianzia huku tuliko.

Bila kuanzisha vuguvugu la kudai Katiba mpya, tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu huku watawala wetu wakiendelea kutukamata mateka na kutunyonya.

Kwa Katiba ya sasa, watawala wetu ni wakoloni weusi tena walio hatari kuliko weupe ambao kwa kiasi fulani walikuwa na utu na kiwango kidogo cha ufisadi.

Katiba ya sasa inatengeneza ukupe wa kimfumo ambapo umma unanyonywa hadi kwenye mifupa tofauti na ukoloni uliotengeneza ubepari ambapo angalau ng’ombe alinyonywa lakini akapewa majani.

Kupe hana muda wa kutoa chochote kwa ng’ombe. Anaweza kunyonya hata mzoga hata ngozi ilmradi lake liwe. Namna hii hatuwezi kuwa taifa huru hata kidogo.

Hapa ndipo watawala wetu wanaotuaminisha kuwa wanatutakia maendeleo wanapaswa kuelewa kuwa wasiporidhia mabadiliko ya Katiba basi waseme wazi wasivyo na mpango wa kufanya wasemayo majukwaani. Maana kwa Katiba yetu nao si huru.

Na ndiyo maana wanajizungushia walinzi wengi kutokana na kujua wazi umma unavyowachukia na kujua matendo yao machafu hata kama yamehalalishwa na Katiba ya kijambazi.

Tumalize kwa kuwakengeua Watanzania kuwa wakati wa kuanzisha CCM nyingine kuiondoa CCM ya sasa iliyojificha na uovu wake kwenye Katiba ni huu.

Bila vuguvugu hili, kelele zote tutapiga na rais atatupuuza na kuendelea kufanya chochote atakacho.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 16, 2009.

No comments: