The Chant of Savant

Wednesday 22 December 2010

Madaraka hulevya kuliko hata ulabu

MWENZENU nimerudi wiki jana kutoka Ivory Coast au Cote d' Ivoire kwa wale wanaojua Kifaransa yaani nchi ya wale jamaa waliofungwa na vijana wetu juzi juzi tu na kuleta ujiko kwa wasioustahili yaani wanasiasia.

Wanasiasa walidandia ujiko huu wakati wao ndiyo kikwazo kwa ufisadi ujinga na usanii wao! Hayo tuyaache.

Nilikaribishwa kule kwenda kujaribu kusuluhisha mgogoro wa uchakachuaji ambao umeanza kuwa tatizo sugu na kansa ya kisiasa barani humu. Niliitwa kutokana na kaya yetu kuwa na uzoefu au tuseme ukondoo.

Maana kwetu tulipochakachuliwa, kwanza hatukuwa na marais wawili kama kule wala wachovu hawakuingia mitaani kama Cote d' Ivoire. Walevi huwa hawana taimu na mambo kama hayo bali kuuchapa ulevi. Pili tuliyamaliza kivyetu vyetu kiasi cha wenzetu kutamani nao wajue sayansi hii wasijue ni balaa na kiama cha jamii!

Pia nilialikwa kule kutokana na kaya yetu kuwa karimu kiasi cha kuwa inawazawadia hata matapeli njuluku kama ilivyotokea kwa Dowanis. Waivorien walisema wakimaliza aibu yao watakuja kuwekeza huku ili nao wachume na kufaidi pepo hii ya mabwege.

Leo sitaongelea sana mambo ya Ivory Coast kwa sana kutokana na kutimuliwa na waivorien baada ya kuwambia kuwa natokea Bongolala na siyo Bongo kama walivyodhania.

Walinipa laivu kuwa hawataki mtu wa kwenda kuwafundisha ukondoo na ubongolala ili hapa baadaye wachezewe kama tunavyochezewa na gendaeka wachache waliojipenyeza kwenye maulaji yetu. Walisema wazi kuwa hawakuhitaji mtu wa kuwakeketa kiakili wala kuwaingilia na kuharibu!

Sababu ya pili ni kugundulika kwa njama zangu za kutaka kumtetea Laurent Gbagbo kutokana nami kujua nisipomtetea wakati nilichakachukua ukuu wa kijiwe ingekuwa unafiki. Hivyo, jamaa walinistukia wakanizomea na kuniita Gbagbo wa Kijiweni huku Gbagbo akiitwa Jackalent Kikwegbo sorry. Naomba nisitaje jina jingine walilompa huyu mchakachuaji marhuni.

Ila walimpa sifa ya usanii mfu na nyemelezi vitokanavyo na ufisi na mawazo mgando.

Niliondoka pale Felix Houphet Boigny International Airport kwa aibu kabla ya jamaa yangu mmoja kunikaribisha kupitia kwake na kushuhudia maajabu karibu na yale yanayoanza kujipenyeza kwenye kaya yetu.

Kutoka huko nilipata mwaliko kwenda kumfunda jamaa mmoja mpenda madaraka aitwaye
Dk. Dk. Prof, Alhaj, Mtakatifu, Mtukufu, mhe. Mpendwa mnyenyekewa Mlambwa miguu. Kanali na makorokoro mengi, Yahya Jemus Jukung Jammeh. Jamaa pamoja na kujipachika vyeo na heshima zote hizo ni kihiyo kama jamaa yangu.

Nilitua Yundum Airport salama salimini na kuelekea kula mahanjumati na jamaa yangu huyu ambaye wengi humuona kama kihiyo tapeli na mchakachuzi wa aina yake. Nionye. Hii yandum haitokani na ndumu ya vichaa wangu wanayovuta ili waweze kuhimili mateso ya walaji wa Dowanis.

Huyu jamaa wengi humuona kama juha aliyekaa madarakani kitambo na asifanyiwe kweli.

Huyu jamaa ana nafuu kiasi fulani ikilinganishwa na ukihiyo wake. Siyo kama yule mwingine ambaye leo nitamhifadhi. Tena ni juzi tu tapeli mmoja aliyeshindwa maisha ughaibuni alimtungia kitabu cha kumsifu Jammeh wangu. Huu ndiyo huwa nauita usomi nepi mwenzenu.

Huku ndiyo kujikomba mithili ya changudoa au dungaembe. Huku mwenzenu niliona maajabu ya maajabu!

Jamaa kwa kupenda shahada za dezo na vyuo vya huko vilivyokuwa hovyo, kila chuo kinajikomba kiasi cha wasomi wake nao kugeuka vyangu wa kimaadili tena bila aibu ili kupata madili toka kwa bwana mkubwa mpenda makubwa.

Kila anapokatisha anapewa shahada. Kwangu hivi si vyuo bali vyoo vikuu vya maarifa.

Hata hivyo, sikushangaa sana baada ya shahada kugeuka upuuzi kiasi cha wapuuzi na matapeli kuzighushi na kuzitumia kiasi cha kushindwa kutofautisha kati ya wasomi na waganga wa kienyeji wapendao kujiita maprofesa wakati ukweli ni maprosoo watupu.

Jamaa anapenda dezo kama kapushimo la choo! Hebu katupe chochote uone. Angalau hata kapu na shimo la choo hutosheka, maana lau hujaa. Yeye hatosheki! Ni laana na ufisi kiasi gani?

Ila pamoja na tamaa za shahada na ujiko, rafiki yangu si kiruka njia wa kudandia kila tetea apitaye mbele yake kama jamaa yangu. Ana wake zake wawili, wote waarabu na vitoto vyao viwili.

Hana watoto wa kuokota au kubwagiwa mlangoni au wasiojulikana waliletwa lini. Ukimuuliza swali kuhusu familia yake hasiti wala kuona aibu anakupa jibu linaloingia akilini.

Vitoto vyake bado ni vichanga. Havina sifa ya ulevi wala kupenda kudandia madaraka yake navyo vionekane virais vidogo kama wengine. Kwa hili nimemsifu jamaa huyu pamoja na mapungufu yake.

Kitu kingine nilichogundua kuhusiana na jamaa huyu ni kupenda sifa. Kila tapeli humpa tuzo naye hukenua wakati anatumiwa. Si unajua tena NGO zilivyogeuka miradi ya wake wa vigogo. Lol! Ngoja niishie hapa bi mkubwa wangu asijeinyaka akanipa adhabu ya kudeki na kuosha vitoto.

Turejee kwa matapeli wanaozuga na tuzo uchwara. Anyways, wanatumiana. Si unajua matapeli walivyokuwa na urafiki na usuhuba wa mashaka? Usishangae kesho baada ya jamaa fulani kuondokewa na maulaji hata shoga yake Kagoda bin Dowan akampiga teke na kudandia mwingine atakayemweka mkononi. Kwani matapeli hawa wanaaminika?

Baada ya kuona jamaa anapenda tuzo, nimepanga, siku nikipata kurudi kule nimpelekee tuzo za uzembe, matumizi mabovu, ukabila, uchakachuaji, uzururaji, usanii, ufisadi, usiri, visasi na mengineyo.

Madaraka ya jamaa yangu yamempofusha na kumlewesha kiasi cha kutumiwa na kila tapeli na msaka, ngawira, cheo hata ujiko.

Si wasomi, hasa wale nepi na kanyaboya, wala majuha na matepeli wa kawaida. Wote wamemgeuza mradi wa mafisi na majuha na asikengeuke!

Wa kumtunuku shahada za uongo na ukweli, wanamtunuku na wa kumtungia vitabu na kuimba sifa za uongo wanafanya hivyo kwa namna yake na wakati wake na hastuki japo umma wamcheka kwa ulimbukeni na mapenzi ya dezo.

Jamaa hastuki bado! Amegeuka kokoro au tuseme kichwa cha mwendawazimu mchana kweupe! Ama kweli wahenga walinena. Madaraka hulevya kuliko hata ulabu hasa yaangukiapo mikononi mwa juha na limbukeni mufilisi!

Duh! Kumbe leo ni siku ya mgao (mdowan). Acha niwahi kununua mafuta pale nayo sijui kama hayajachakachuliwa kama sisi!
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 22, 2010.

No comments: