The Chant of Savant

Friday 27 May 2011

Serikali ya CCM imechanganyikiwa

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama si kuishiwa basi imechanganyikiwa, imeishiwa hata uhalali wa kutawala kutokana na matendo yake.

Kashfa zote kubwa za wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma zinaihusu na haijitetei zaidi ya kukiachia chama tawala CCM kufanya usanii ambao nao haufui dafu.

Hebu tujikumbushe kashfa kama EPA, Richmond, uchakachuaji na wizi wa kura, matumizi mabaya ya fedha za umma yanayofichuliwa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uwekezaji wa kijambazi na hovyo na baya zaidi ya yote, mauaji ya watu wasio na hatia.

Hivi karibuni watu wapatao sita waliuawa na polisi wilayani Tarime mkoani Mara. Na hii si mara ya kwanza kwa wananchi wa Mara kuuawa wakipigania haki zao zilizobinafsishwa kwa wawekezaji ambao kimsingi si wawekezaji kitu, bali wachukuaji waliokula njama pamoja na serikali kulihujumu taifa.

Badala ya serikali kutoa utetezi wake hata kuomba msamaha, ilidandia upinzani kudai kuna mbunge alikuwa nyuma ya kadhia ya Tarime.

Rejea tuhuma za kizushi za Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Hamis Kagasheki, akidai kuwa wahanga walikuwa wahalifu na aliyewatuma ni mbunge wa chama fulani.

Hivi watu wasio na uwezo hata wa kutumia busara wanafikiaje kwenye ngazi kubwa kama hizi bila kuwa na namna? Au ni yale ya kuwa mkwe wa rais wa zamani? Kama kuna mbunge wa upinzani nyuma ya kadhia hii, basi huyu ndiye anawafaa wananchi. Maana anaongea lugha wanayoelewa.

Na si kama hawa wabunge wa CCM ambao wako tayari kuuza watu wao kulipa fadhila ya kuwezeshwa kuwa wabunge kupitia uchakachuaji.

Kama huyu mbunge alichofanya ni kuvunja sheria, kwanini asichukuliwe hatua? Maana kwa anayejua siasa na sera za visasi za CCM, kama madai ya Kagasheki yasingekuwa uzushi, huyu mbunge wake angekuwa katika hali mbaya.

Kagasheki anangoja nini? Au ni yale kuwa watawala wetu hawana roho zenye kuwasuta na wako tayari hata kujiuza na kuuza watu wao ili wabakie madarakani? Hakika hii ni changamoto kwa Kikwete na serikali yake yote.

Je, Watanzania wataendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu mlevi kujifunzia kunyoa hadi lini? Waguswe wapi au wauawe wangapi ndipo mikoa yote kwa umoja wao iamke na kuipiga teke serikali hii habithi?

Kuonyesha kuwa serikali imechanganyikiwa, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alikaririwa akitoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu.

Huyu ni bosi wa Kagasheki na kinachoendelea hapa ni serikali moja kupingana.

Huyu anasema ni wahalifu. Mwenzie tena bosi wake anatoa mkono wa rambi rambi! Je, huku si kuchanganyikiwa kwa serikali na kupingana kunakoiondolea uhalali wa kutawala?

Hili lingetokea kwenye nchi zenye viongozi wenye akili na si watawala wa wasanii, serikali yote ingetimuliwa bila mjadala.

Kituko kingine, eti polisi waliotuhumiwa kuua ndio wanatumwa kuiwakilisha serikali na kushauri wahanga wazikwe. Tangu lini polisi wakawa wawakilishi wa serikali wakati wanapaswa kutokuwa na upande?

Polisi wa Tanzania licha ya kuwa vinara wa ufisadi, kusaidiana na majambazi, wanasifika kwa kuua wananchi. Ni juzi juzi waliua kule Arusha, Shinyanga, Mbeya na sasa Mara. Halafu hawa hawa wanajiletaleta kwa kutumia kodi za wahanga hao hao kujifanya waelekezi wa nini kifanyike.

Huyu Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja na wenzake wanapaswa kujiuzulu badala ya kujifanya washitaki, waendesha mashitaka na mahakimu.

Hata Waziri Kagasheki aliyekaririwa akisema wahanga walikuwa wahalifu anapaswa kuachia ngazi bila kujali ni mkwe au mtoto wa nani.

Je, haya ndiyo matokeo ya chama kuiweka serikali mfukoni huku kikitumia taasisi za umma kama polisi kufanya kazi zake chafu?

Polisi wetu siku hizi wamegeuka walinzi wa migodi ya wawekezaji huku sisi tukikabwa na vibaka waliowatengeneza kila uchao!

Je, Watanzania kwa sasa ni salama? Je, waende kwa nani zaidi ya kujipigania wenyewe? Je, polisi wa namna hii wanapaswa kulipwa kodi zetu kila mwisho wa mwezi? Kwa kazi na sifa gani?

Ajabu, wakati watu wanaonewa kutokana na sera chafu na chovu za serikali ya Rais Jakaya Kikwete, yeye alipata mshipa wa kwenda Namibia kutanua!

Nasema kutanua kutokana na kulinganisha umuhimu wa alichokwenda kufanya na uhai wa binadamu.

Isitoshe, nasema alikwenda kutanua kutokana na kuficha majina ya watu alioandamana nao, tabia ambayo imeanza kuota mizizi.

Je, kwanini anaficha ujumbe wake kama hakuna watu wenye kutia shaka? Je, huyu kweli anawajali Watanzania?

Kuna haja ya kuendelea kuipa serikali ya Kikwete ushauri wa bure kutokana na umahiri wake wa kuvurunda badala ya kulikwamua taifa.

Wakati kadhia ya Tarime ikiendelea, Shirika la Habari la Uingereza (BBC) liliripoti kuwa Tanzania imeuza ardhi kwa kampuni la Kihindi kufanya shughuli za kilimo.

Najua serikali itakanusha kwa kusema imewakodisha ardhi kwa miaka 99 sawa na inavyowafanyia Watanzania. Kwa wageni huku ni kuuza.

Kabla ya kashfa hii hata kutolewa maelezo, ilifumka kashfa nyingine ya utoroshwaji wa nyara zetu kwenda Uarabuni.

Ajabu wanaofanya hivi ni Wakenya na Wapakstani wakishirikiana na Watanzania. Baada ya habari hii kutoka serikali imefanya nini? Kimya kama kawa!

Serikali yetu inajulikana kwa ubingwa wake wa kunyamaza ili mambo yajifie. Je, Watanzania wataendelea kuuawa, kuuziwa mali zao na nchi yao hadi lini? Kwanini wenzetu wa Kenya na Uganda wanahamanika kulinda masilahi yao huku sisi tukijifanya kila mtu alimhusu na kuishia kulalamika? Je, Watanzania wataendelea na serikali yenye tabia sawa na kuku alaye mayai yake hadi lini?

Tumalizie kwa kuuhimiza upinzani kushikia bango jinai hizi. Kadhalika tunawapa changamoto Watanzania kuachana na ukondoo unaowafanya wageuke wahanga wa kila jinai inayotendwa na kundi dogo la wahalifu wenye madaraka.

Haya ndiyo matokeo ya serikali zitokanazo na ufisadi. Ziko tayari kufanya lolote inayoamriwa na mabwana zake, yaani mafisadi na wawekezaji walioiwezesha kuwa madarakani.

Kwanini watu hata kama ni wachache wasiwe na uchungu wa nchi yao na watu wake? Anayetaka kujua ni kwanini Watanzania hawapaswi kuogopa kundi dogo la wahalifu, ajiulize serikali anayodhani ni yake wakati si yake imefanya nini kujibu tuhuma za wizi wa pesa za umma, kuanzia uliotajwa hadi ule wa rada na ndege mkangafu ya rais?

Ajiulize majibu na utekelezaji au tuseme urejeshaji wa nyumba za umma zilizoporwa na genge hili la wezi umefikia wapi?

Ajiulize zaidi kwanini deni la taifa linaumuka kila siku huku hali ya maisha ya Watanzania ikizidi kuwa mbaya? Jibu la yote ni moja, serikali fisadi na isiyo na visheni wala ajenda ya kulikwamua taifa bali kuliibia kila uchao.

Serikali hii inaingia kwenye vitabu vya historia kama taasisi iliyoiuza Tanzania.

Hakika CCM imechanganyikiwa kiasi cha kutoa matamshi na misimamo inayokinzana na yenye kuiacha uchi. Damu ya Watanzania wa Tarime haipaswi kupotea.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 25, 2011.

No comments: