The Chant of Savant

Thursday 5 May 2011

Wamevuana magamba, sisi nguo

BAADA ya Chama ambacho wabaya wake wamekipa jina la Chama Cha Majoka (CCM) wengine wanakiita cha magamba, kujivua gamba, kijiwe nacho kimekuja na mpya. Kwanza ieleweke. Huu si usanii kama wa CCM bali kutaka kufanya kweli.

Si yametokea mafyatu yanayojifanya yanachukia ufisadi kusema eti tuvuane nguo ili kila mtu abakie alivyozaliwa tumuone! Sikuwa najua kama kahawa inalevya kama maulaji. Baada ya walevi kupwakia kahawa na kashata wacha wachachamae kama siafu!

Ikichukuliwa kuwa ni muda mrefu nimekuwa nikikwepa kuitisha vikao vya kijiwe, walevi walikuwa na usongo sina mfano. Kila mtu alipania kunivaa mwenyekiti ili waje na mkakati wa kuvuana nguo na kunitosa.

Sababu kuu iliyotolewa ni kwamba sisi si majoka wala mijusi bali watu. Hivyo magamba yetu ni nguo tuvaazo. Mijamaa hii mishenzi sina hamu. Moja si lilisema eti majoho, mipete, micheni, misuti na makorokoro yangu ya bei mbaya ndiyo magamba hasa yatokanayo na ufisadi. Mingine ilisema eti NGO ya bi mkubwa ya kashata nayo ni gamba!

Kijiwe kilikaa kikao cha dharura tena bila idhini ya mkiti na kutaka kujadili ufisi na ufisadi. Kwanza walevi wote walipitisha kauli moja kuwa Mgosi Machungi wa Makambale atimuliwe ukatibu mkuu wa kijiwe.

Mzee Maneno ndiye alikuwa wa kwanza kulitibua. Alisema, “Waheshimiwa wajumbe tusipoteze muda. Leo lazima tusafishe kijiwe chetu kwa kuwatimua mafisi wote.”
Inaonekana hii ilikuwa imepangwa. Maana wote waliitikia kwa pamoja isipokuwa washirika wangu waliokuwa wamepigwa na bumbuwazi.

Kuona wanataka kunipindua nikiwepo niliingilia haraka, “Hili ni jambo jema kwa mustakabali wa kijiwe. Natoa baraka zote tuwasulubu mafisi wa kijiwe hiki. Kwanza, watajeni hao mafisi. Mie sitaki unafiki.”

Kabla sijamaliza mzee Maneno alidakia, “Mwenyekiti acha unafiki. Unajifanya hamjijui mko mafisi wangapi? Mbona kwenye kuiba njuluku za kijiwe kupiga kampeni iliyokupa ulaji mlikuwa pete na chanda. Leo unajifanya kuwasahau!”

Kabla ya kumaliza, Msomi alipayuka. “Basi tunawataja. Kwanza mkiti, Mgosi, Ewassa, Roasttamu, Chengee.”

Kabla ya kumaliza Mchunguliaji anakwanyua mic, “Mbona humtaji bi mkubwa wa Mkiti na NGO yake na kitegemezi chake Riziki ambao ni wakwasi wa kutupwa kutokana na kutumia madaraka ya mkiti?”

Makambale alivyo mbishi msambaa huyu si alikataa kufa peke yake. Alisema hawezi kuachia ngazi hadi waganga njaa wenzake wa Kamati kuu ya Kijiwe yaani Kijiwe Central commetee (KCC)nao watimke naye isipokuwa mie mkiti.

Wakati Makambale akipiga mkwara mie nilikuwa nimeishaanza kunonihii kwenye sarawili yangu. Baada ya kujitoa mhanga kufa na wenzake huku akinisaza mimi, nilianza kupumua.

Msomi Mkata Tamaa alikwanyia mic na kutoa wazo la kipumbavu kuwa wa kwanza kuvuliwa nguo na ulaji niwe mimi mwenyekiti. Toba! Nilijisemea moyoni. Mie na kutotahiriwa kwangu si itakuwa shughuli!

Nikiwa natafakari la kusema lau kujiokoa ingawa kiakili sina ujanja wala mshipa, si fyatu wangu Pio Mchekwa akajaribu kuokoa jahazi.

Bila kuomba ruksa Pio alisema kwa kujiamini, “Mkiti ni mtu safi sema anaonekana mchafu kutokana na kushauriwa vibaya na akina Mgosi.”

Kabla ya kuendelea fyatu Andramani Kinamna alikwapua mic na kusema, “Msomi tukubaliane umevuka mipaka. Mkiti ni mtu safi na hata kama ni mchafu inakuwaje atoswe na sisi wenzake bila kutoa wengine sadaka ili apone?”

Kabla ya kuendelea mzee Maneno aling’aka, “We kinamna nyamaza. Uchafu wako wa kutorosha nyara za kijiwe unajulikana. Hivyo funga domo lako hata kama unapewa makombo na mkiti.”

Bila kungoja waende mbali niliingia kati, “Mzee Maneno nakuheshimu sana. Futa kauli yako na uniombe msamaha kabla sijakutoa kafara.”

Mzee Maneno hana subira. Anadandia mic na kusema, “We ni mwizi wa kawaida tu hata kama ni mwenyekiti. Unadhani hatuoni mkeo na vitegemezi vyako wanavyotuibia kashata na kahawa kila siku? Nyamaza mwenyewe kabla sijakuvua nguo kabla hata ya kupitisha azimio la kufanya hivyo.”

Kuepusha shari ilibidi ninywee na kufunika kombe ili mwanaharamu huyu mzee apite nipete.

Kumbe mzee Maneno alikuwa amepania! Pia baadaye niligundua kuwa mpango ulikuwa umesukwa muda mrefu bila sisi kujua. Mzee Maneno alishikilia uzi na kusema lazima tuvuliwe nguo.

Kuona mambo yanazidi kuharibika, nilimtonya kijana wangu Mapepe Ninaye aharibu hewa. Bila kufikiri wala kujivunga ili kunifurahisha akijua nitampa ulaji Mape alinyanyuka na kusema, “Tukubaliane. Hatukuja hapa kupanga jinsi ya kumvua nguo mkiti bali Ewassa, Endelea Chenga na Roast Tamu ambao wanajulikana walivyokwanyua mimali ya kijiwe. Ndiyo siyo?”

Kijiwe wala hakikumsikiliza zaidi ya kuanza kumvua yeye nguo huku akizabwa vibao kama mwizi. Ilisika sauti ikisema, “We Mape ni kinyoka kichanga lazima tukushughulikie ili ufe na joka lenyewe yaani mkiti.”

Bila ajizi kijiwe kilipitisha pendekezo hili na kuamua kutuvua nguo. Tulivuliwa nguo. Tulilambwa vibao kuzomewa na nusu kuchomwa moto kama si busara ya Msomi Mkata Tamaa. Yaani ilikuwa tufe tunajiona!

Wanakamati waliliripuka kwa shangwe kutokana na kujua kuwa nilitaka kuwavua nguo hawa mapacha watatu nisijue ningevuliwa. Hawakungoja niidhoofike kama wengine walivyodhani. Isitoshe, huu ulikuwa kama mtego kwangu kuona nitawanusuru au kuwatosa vipi mabesti zangu. Ilibidi nitumie kanuni ya Yesu ya kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe ingawa haikusaidia.

Sasa Msomi ambaye ndiye mkiti alisema, “Tuweni wakweli. Dawa ya jipu ni kutumbua siyo kuligusagusa. Nashukuru leo mkiti kavuliwa nguo sambamba na watu wake.”
Hii imetutofautisha na wale wasanii wa magamba, wao walivuana magamba. Sisi tumewavua nguo na mmewaona walivyotimka uchi. Hali ilikuwaje, we acha tu sikia hivi hivi.

Kwa sasa niko kijiweni naganga njaa bila joho la uenyekiti. Ushauri wa bure, ukitaka kujivua ufisadi vua nguo badala ya magamba hata kama inauma na kutia fedheha.

Naona wale mafisadi wa magamba wanapita. Acha nikawahi kijiweni tupange jinsi ya kuwavua nguo hasa mkiti wao.

Khalasi kweisine Rais Mtarajali.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 4,2011.

No comments: