The Chant of Savant

Wednesday 25 January 2012

Maskini CUF, fupa la CCM limeisambaratisha!

Kwa mtu anayejua tabia za mbwa, hatapingana nasi kuwa, hata awe mjanja, mwenye nidhamu na mafunzo kiasi gani, mbwa akitupiwa fupa usahau kila kitu. Ukitaka kumuibia mbwa hasa anapokuwa kwenye lindo, njoo na fupa.

Hivyo, ndivyo ilipotokea kwa Chama Cha Wananchi (CUF) mbacho kilichozolea umaarufu mkubwa kwa kuitikisa serikali na nchi kutokana na harakati zake za kudai haki hasa kwa upande wa visiwani. Kwa wanaokumbuka historia ya chama hiki watakubaliana nasi kuwa, licha ya historia yake chafu ya kufukuzana, kilileta changamoto ya kutosha kuanzia miaka ya 1992 ulipoingia mfumo wa vyama vingi nchini.

Ingawa tangu kuanzishwa kwake, CUF ilionyesha wazi kimatendo na kimkakati ilivyokuwa imeegemea upande mmoja, si haba ilileta changamoto kwa nchi nzima. Sasa hii imebakia historia baada ya Katibu wake mkuu Seif Sharriff Hamad kupewa umakamu wa kwanza wa rais. Ingawa wengi wanachukulia mvurugano unaondelea kwenye chama cha CUF kama suala la ndani, ukweli ni kwamba mchawi ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichobuni njia rahisi ya kuepuka madhara makubwa visiwani baada na kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Baada ya CCM kugundua kuwa isingeweza kushinda kihalali na CUF wasingekubali matokeo ya kupikwa, kilikumbuka kitu kimoja-CUF imejengwa kwenye jina la mtu na si sera wala mikakati. Na mtu huy si mwingine bali Seif ambaye kimsingi ndiye CUF na CUF ni yeye. Kwa kujua alivyoachwa nje kwa muda mrefu na kuanza kuishiwa kulhali, CCM walimzuga na kumwingiza kwenye mazungumzo yaliyokuwa yamekwama kwa miaka mingi. Kwa kujua kuwa Seif alikuwa anakabiliwa na shinikizo la wanachama kumuona kama hafanikiwi, hakuwa na jinsi bali kukidakia chambo ili aweze kufaidi lau binafsi hata kama ni kwa kukiua chama.

Baada ya Seif kuingia ubia au tuseme kufunga ndoa ya mkeka na CCM, kuna baadhi ya wana CUF waliona kama wanasalitiwa hata kuuzwa kwa ajili ya maslahi ya mtu mmoja. Huu ni upande mmoja. Upande wa pili ni pale Seif alipokikabidhi chama mikononi mwa mtu mwingine ili aweze kutumikia nafasi yake mpya. Hili lilisababisha kuibuka maswali mengi kuhusu utendaji wa Seif. Seif kuona hivi akaamua kuwa mkali na kumshughulikia yoyote aliyehoji ndoa yake na CCM au kukasimu chama mikononi mwa watu wake wa karibu. Kimsingi hiki ndicho chanzo kizuri cha kuvurugana na kufukuzana kwa CUF ambako bila shaka utakidhoofisha chama.
Kitu kingine kilichomtia motisha Seif kufunga ndoa na CCM ni ile hali ya kudhani kuwa anaweza kujaribu tena akashinda urais wa Zanzibar iwapo rais wa sasa atapendekezwa kugombea kiti cha muungano kama mambo yasiyo ya kikatiba ya zamu za pande za muungano yataruhusiwa badala ya vyama kuteua wagombea wanaofaa.

Kwa mahesabu ya haraka, kama rais wa sasa wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein atasimama kwenye uchaguzi wa muungano CCM haitakuwa na mtu mwenye kuweza kushinda urais wa Zanzibar kama mmojawapo atapitishwa na CCM. Hebu fikiria watu kama Dk Hussein Mwinyi ambaye baba yake alishakuwa rais wa Zanzibar na muungano, nani anaweza kuruhusu utawala wa kurithishana na kufuata majina? Maana ni juzi tu mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar Aman Karume amemaliza kipindi cha miaka kumi. Wengine wanaotajwa na Shamsi Vuai Nahodha ambaye alikuwa waziri kiongozi kwa miaka kumi. Huyu hana ubavu visiwani ingawa aliwahi kushika nafasi ya juu. Mwingine ambaye bila shaka anaweza kuingia kwenye kinyang’anyiro na kutoa upinzani mkubwa wa Seif hata kumshinda ni makamu wa pili wa sasa balozi Idd Seif ambaye chati yake inapanda kwa kasi ya ajabu.

Sababu nyingine iliyosababisha mvurugano ni kuchokwa kwa Seif ambaye amekuwa akigombea miaka mingi bila kufanikiwa ukiachia mbali kuongoza kwa staili moja ya muungu mtu. Zama za chama kumtegemea mtu zimepitwa na wakati.
Kitu kingine ambacho tumeishakiongelea ni ile hali ya CUF kuwa CCM B. Hili limeelezwa wazi wazi na waliofukuzwa na jinsi lilivyowakera. Shoka Khamis ambaye alikuwa Mbunge wa Micheweni, Kaskazini Pemba alikririwa akisema, “Nimejifundisha mengi sana CUF mazuri na mabaya, lakini leo kwa sababu wamenifukuza ngoja niseme mabaya, CUF sisi ni CCM B kama wanavyosema wenzetu. Chama kina sifa mbaya ya kufukuza watu, lakini anayefukuza wenzake, Seif Sharif Hamad yeye anajiona kama mungu hafanyi makosa,”

Sababu ya mwisho ni historia chafu ya kufukuzana au kujenga mazingira ya kuwalazimisha wasiotakiwa kwa kukosoa uongozi wa juu kuhama chama kama ilivyotokea kwa James Mapalala mwanzilishi wa CUF, Maiko Nyaluba, Slivesta Kasulumbai (mbunge), Geoge Shambwe, Shaibu Akwilombwe, Richard Hiza Tambwe,Wilfred Lwakatare, Othman Dunga, Asha Ngende,Khamisi Katuga na Ashura Amazi ambao wallifukuzwa kutoka upande wa bara wakati upande wa visiwani waliotimuliwa au kujiondoa baada ya kuhoji ulaji wa wakubwa au kutofautiana nao kimwazo ni pamoja na Naila Jidawi,Fatuma Magimbi,Juma Othuman, Salumu Msabaha na Hamad Rashid.

Je watafukuzwa au kunyamazishwa wangapi na lini? Hakuna anayeweza kutabiri ingawa hali inaonyesha kuwa ushindi wa Seif ni wa muda. Maana unaweza kuwadanganya watu wote kwa wakati fulani. Pia unaweza kuwadanganya watu fulani kwa wakati wote lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa wakati wote. Kuna haja ya kuwashauri wana-CUF kubadilika na kuanza kupigania maslahi ya chama badala ya kulinda maslahi uchwara ya watu binafsi wanaowatumia kama nyenzo za kushibisha matumbo yao.

Chanzo: Dira Januari 2012.

No comments: