How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday 15 February 2013

Tusiruhusu bangi za akina Kashillillah Bungeni

 Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (Picha kwa hisani ya IPPMedia).
Taarifa kuwa katibu wa Bunge Dk Thomas Kashillillah alipendekeza kuwa vikao vya Bunge visitangazwe moja kwa moja ni upuuzi. Kuna haja ya kuwafahamisha akina Kashillillah wote wa wazi na waliojificha kuwa hili Bunge ni la watanzania wala si lao, wabunge wala mama zao. Bunge lipo si kwa utashi wa CCM au Spika, naibu wake wala wabunge bali watanzania. Linaendeshwa kwa pesa ya mlipa kodi na linafanya kazi za wananchi na si vinginevyo.
Kuna haja ya kuwafahamisha akina Kashililah kuwa zama za genge la watu wachache kuuburuza umma zimepita kitambo. Wafahamu kuwa ufisadi wa kiakili na kimfumo utaendelea kutawala huku wajinga wachache wakijihadaa kuwa wataliburuza taifa milele. Wasihadaike na ufisadi wanaofanya bila kuchukuliwa hatua wakadhani kila kitu kitaendelea kuwa kama wanavyotaka. Ni ajabu kwa mtu anayeitwa Daktari sijui wa nini kufikiria acha kutenda vitu kama hivi. Je Kashililah ni kati ya wale madaktari feki wa kughushi waliotamalaki kwenye baraza la mawairi? Inakuwaje udaktari wake hamsaidii kuona jambo jepesi kama hili? Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ambapo madaraka yote ni ya umma na si ya watawala. Hata wakati wa udikteta wa chama kimoja, hakuna aliyefikia kutenda wala kufikiria kufuru kama hii. Hata kama ni ulevi wa madaraka, huu sasa umevuka mipaka na dawa yake ni kwa umma kuhakikisha hizi bangi za akina Kashililah zinakomeshwa mara moja.
Kumekuwa na lawama nyingi kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefanya jambo baya kuweka wazi namba za simu ya spika wa Bunge Anna Makinda. CHADEMA si wendawazimu wala wapumbavu---wanajua wanachofanya na walichofanya ni sahihi na ni kwa ajili ya maslahi ya watanzania.
Ni bahati mbaya kuwa watetezi wa upuuzi huu hawaji na hoja zaidi ya kuokoteza vijisababu uchwara. Mfano, kuna mtu mmoja ameandika kwenye blog kuwa kitendo cha kufichua namba za spika kitamdhalilisha kijinsia. Ebo, mbona alipoteuliwa kugombea uspika kwa sifa moja tu ya ujinsia hakudhalilishwa? Kwani namba za watendaji wa umma zinazojulikana kama vile wakuu wa polisi wa mikoa ambao ni wanawake zinawadhalilisha? Hoja za ujinsia na kudhalilishwa ni chovu na hovyo. Ni hoja zilizojaa 'ukashilila' mtupu.
Kiongozi yoyote kama anafanya kazi kwa misingi ya utawala bora hana haja ya kuficha namba zake za simu. Inakuwaje simu hizi zilipiwe kwa pesa ya umma lakini bado ziendeleee kuwa siri? Wanachoficha ni nini kama wanawajibika?
Nadhani kinachowasumbua wale wote wanaoamini katika kufanya namba za watumishi wa umma kuwa siri ni ukale na mawazo mgando yanayofanya shughuli za umma zionekane kama suala binafsi.
Hizi ndizo naita bangi za akina Kashililah na wote wanaotetea uoza huu ni wavuta bangi hizo.Je watanzania watakubali Bunge lao kutaifishwa na kubinafsishwa kwa wachovu wachache wasiojua hata wanachofanya kwenye nyadhifa zao? Wanataka kugeuza Bunge letu chumba cha mganga wa kienyeji na mchawi ambao kazi zao hufanyika kizani na kwa kificho? This should not happen in Tanzania. Never never never.
Tumalizie kwa kuwaonya wenye mawazo mfu na mgando kama Kashililah kuwa kutangaza vikao vya Bunge siyo suala la hiari wala hisani bali haki ya watanzania. Lazima watanzania wajue na kuona wabunge wao wanafanya nini, na  kwa namna gani Bungeni. Wamewachagua kufanya kazi kwa niaba yao. Sasa kama ni hivyo, hii jeuri na ufidhuli vinatoka wapi kama siyo kutafuta balaa na bangi za mchana? Shame on you Kashililah na wenzako!

No comments: