The Chant of Savant

Saturday 2 March 2013

Kufeli Bongo: Suluhu somesha nje au…

Juzi nilicheka hadi nikapaliwa na ulabu. Kama sio kuwahishiwa maji, huenda ningelazwa.
Kwa vile si mtu wa kuibiwa mchana, sikwenda hospitali kuishia kulipa ‘fweza’ za kumuona daktari ambaye angeniandikia dawa na kuniagiza nikanunue kwenye ‘famasi’ yake.
Wajua nini? Hakuna kitu kilichonivunja mbavu kama majibu ya baadhi ya watahiniwa wa form fail.
Nasikia badala ya watahiniwa kujibu maswali ya mtihani, waliamua kuonyesha vimbwanga vyao hasa chuki kwa waheshimiwa na usongo wao katika mapenzi. 

Japo wengi waliona hili kama jambo la ajabu, walishindwa kuelewa kuwa haya yote yanasababishwa na kaya yetu kuwa ya siasa na mapenzi.
Ukisikiliza miziki inayochezwa kwenye radio zinazoendeshwa na watangazaji mabambataa, utagundua kuwa hupenda kucheza nyimbo za mapenzi tena X ndicho chanzo.
Sasa mnategemea nini? Sababu nyingine ni ile hali ya `wadanganyika’ kuabudia `ustaa uchwara’ na usanii.
Baada ya mkulu `kuwashobokea mastaa’ hasa alipokwenda kumzika mwenzao mmoja, kila kitu kilibadilika, wasijue jamaa alikuwa akikwepa joto la migomo. Hayo tuyaache.
Kimsingi, mambo yasiporekebishwa hasa kumtimua kazi waziri mhusika aitwaye Doc Thanks Kawambwa, mambo yatazidi kuharibika.
Natabiri kuwa kwenye majibu ya mwaka ujao, watahiniwa wanaweza kuonyesha hata video za ngono kama majibu.
Wakati vitegemezi vyenu vinavyosoma `uswekeni’ vinaotea bongofleva na mapenzi, vigegemezi vyetu vinavyosoma ‘majuu’ vinaota kurithi ukubwa wetu.
Usishangae ya Ndalichako kusema eti vitegemezi vya wachovu viliandika mistari ya love.
Kitegemezi changu kilichosoma huko kwa Mama kiliandika kwenye mtihani, once I am done hither, I become a ruler like my dad and mam. Waulize akina Jan Makamba au Hossein Mwinyi watakwambia.
Watoto wa wakubwa hawali ‘bwimbwi’ wala kuiba kuku, bali ‘midola’.
Ila wachovu wakitaka watoto wao wawe wanasiasa, hawana haja ya kuwapeleka nje hata Uganda au Kenya.
Hebu, mfano, angalia hiki kitegemezi kilivyowashukia jamaa wa ‘mjengoni’.
“Unakuta mwanafunzi anaeleza anavyolishangaa Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge, wamekaa kama wapo kijiweni…”
“Wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za wananchi waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda Kombe la Kagame inapokelewa bungeni…”
“Bunge limekuwa kama kijiwe, bungeni siyo ukumbi wa starehe, kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika ofisi zao au viwanjani.”
Je, unaweza kusema kuwa hicho ‘kitoto’ hakina elimu? Sema, hakina cheti ila kina elimu kuliko waheshimiwa.
Hiki kitegemezi ‘noma’ kweli kweli. Kumbe kinajua kuwa sheria mbovu wanazopitisha wahishimiwa ‘mjengoni’ ndizo chanzo cha maangamizi yake! Good kid, good job!
Japo wengi wasiojua falsafa ya elimu watawalaumu vitegemezi vyao kwa kuandika vitu vya ajabu.
Mlitaka waandike nini iwapo kila uchao mnawahubiria maloveydovey? Nadhani vitegemezi vyenu vimeonyesha umahili wa kusoma magazeti ya uchafu na kuangalia luninga kwa sana. 
Mnapopanda ngono na ufisadi mnategemea mvune elimu? Mnapopanda ‘mitusi’ tena ‘mjengoni’ mnategemea nini?
Waulize akina Jobless Nduguy. Aliposema kuwa mwenzake kazoea kuchamba sana au Nahoda aliyemwambia mwenzake kuwa hatumii akili, ana tofauti gani na yule aliyesema kuwa waheshimiwa wanatumia masaburi kufikiri badala ya vichwa?
Nadhani wakati muafaka umetimu kuwashauri waheshimiwa wakae ‘mjengoni’ na kutunga sheria itayolazimisha kila mzazi kupeleka kitegemezi chake kusoma nje.
Kama wakubwa wanatibiwa India, kwa nini vitegemezi vitibiwe ujinga wao nje? Mie napendekeza vipelekwe Syria ili vijifunze kupambana na kukomboa kaya yao.
Vingine vipelekwe Afghanistan ili vijifunze jinsi ya kupambana na ugaidi wa kidini kama ule uliotokea Zenj ambapo kasisi mmoja alinyotolewa roho.
Watahini wanalalamika kuwa wamepewa majibu ya urongo. Hivi walitegemea nini kama waheshimiwa wanapewa majibu ya uongo na mawaziri na hakuna kinachofanyika?
Walitegemea nini iwapo ujambazi unaoitwa twisheni umehalalishwa? Hivi mlitegemea waogope kutoa majibu ya uongo kwa vile wanaogopa kufeli?
Siku hizi hakuna anayeogopa kufeli. Unafeli darasani na kwenda mtaani na kununua cheti na shahada na kuendelea kupeta. Anayedhani namdanganya akawaulize wale mawaziri waliotuhumiwa kughushi shahada.
Si wanaendelea kupeta na kupetuka tena kwa pesa ya mlipa kodi kapuku. Sasa Mungu awape nini zaidi ya ulaji huu wa ‘dezo’ na laini?
Ukifeli darasani huna haja ya kuhofu. Kama hutaki kununua shahada basi unaanzisha mradi wako wa kuuza bwimbwi kama si kuimba mistari na kuukata.
Ukiona haya huyapendi, unaanzisha kampuni ya kushindanisha ma-miss vichochoroni na kupata ‘mshiko.’
Juzi mlevi mwenzangu alituacha hoi. Alisema mwanae alilalamikia maswali ya mitihani.
Alisema kuwa mwanae alipoulizwa swali la: Define the law of floatation alijibu simpo kuwa you sniff cocaine and start floating.
Hii maana yake ni kwamba tubadili mitaala. Badala ya kuwauliza vitu kama Newton’s laws of motion waulize Adam’s and Eve’s secrets and the fruit they ate.
Tupige marufuku ma-novels kama Things Fall Apart, The River Between, No longer at ease na mengineyo ili yasiwaumize vichwa watoto wetu.
Tufundishe elimu yetu kwa Kiswahili kwa sababu soon kitakuwa lugha ya dunia. Mambo sonic subsonic and supersonic tuwaachie wenyewe tuwe watazamaji au vipi?
Badala ya kuwasumbua na kukariri `matabu’ kama history of the time- Stephen Hawking waulize maswali toka kwenye magazeti ya udaku muone watakavyotoka na flying colours kama siyo cum laude.
Ningekuwa mwalimu ningeuliza maswali kama: What do people do in short-time guest houses? What are the effects of barning marijuana and the effects of legalizing impunity?
Mlevi mwingine alituacha hoi aliposema kitegemezi chake kilipoulizwa kuelezea maana ya siasa kilijibu kuwa:
Siasa ni mfumo wa uongo na usanii unaomwezesha mtu kuukata haraka na kuitwa mheshimiwa hata kama anayofanya hayastahili heshima.
Nasikia eti mwenzie alipotakiwa afafanue maana ya uhuru, alisema eti uhuru ni hali ya kila mtu kufanya ufisadi na usanii atakavyo bila kuvunja sheria.
Tumalizie kwa kuwapongeza vitegemezi vyetu kwa kutufungua macho. Ingawa wengi wanavilaani, kimsingi majibu yake yanatoa jibu la tatizo kuwa tusomeshe watoto nje au tubadili mitaala.
Badala ya kuwekeza sana kwenye grossaries, short-time guest houses na siasa za kibabaishaji, tuwekeze katika elimu. Simpo. Anyways, napita tu.

Chanzo: Nipashe Jumamosi Machi 2, 2013.

No comments: