How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday 16 March 2013

Tusiligeuze taifa kaburi la waandishi



Taifa letu, kwa sasa, ni maarufu dunia kutokana na tabia mbaya. Hakuna ubishi kuwa kwa sasa Tanzania inasomeka sana kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kutokana na uchafu wake. Hivi karibuni kulikuwa na umaarufu wenye harufu mbaya utokanao na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Baada ya kadhia ya mauaji ya kishenzi, kinyama na kishirikiana na watu wenye ulemavu wa ngozi yanayofanywa na watu wenye imani chafu na tamaa utajiri, wanaofuatia ni waandishi wa habari.
Mwaka jana mwandishi Daudi Mwangosi alipigwa risasi na kuuawa na polisi jambo ambalo lilifanya taifa letu kujulikana kwa tabia hii chafu kwenye vyombo vya kimataifa vya habari na vya kutetea haki za binadamu.
Hata kabla ya vumbi kutua, mwandishi mwingine wa habari Shaban Matutu wa Tanzania Daima alipigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake. Hadi sasa haijulikani wahusika ambao wanafahamika walichukuliwa hatua gani.
Hivi karibuni mwandishi mwanadamizi Absalom Kibanda, mhariri mtendaji wa New Habari (2006) alitekwa akiwa anashuka nyumbani kwake. Kibanda alipigwa sana, kung’olewa meno na kucha kiasi cha kukimbizwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu.
Kwa wanofatilia matukio haya kwa undani, watakubaliana nasi kuwa kinachojibainisha ni dalili za mfumo fisadi na wa kimafia unaoanza kujengeka nchini. Si uvumi, waandishi wa habari wanalengwa na makundi ya watu hata taasisi yanayowaona kama tishio la maslahi yao ya kijinai. Waandishi mahiri wanaofichua uchafu unaotendwa na wakubwa wamekuwa wakaitishiwa maisha na hata kuumizwa na hakuna kinachofanyika. Je namna hii tunalipeleka taifa wapi kama si kuligeuza kaburi la waandishi wa habari? Je nchi na serikali vinaweza kuwapo na kuendesha shughuli zake bila waandishi wa habari?
Nchi zilizoendelea zinajua umuhimu wa waandishi wa habari. Ndiyo maana tasnia ya habari huitwa fourth estate yaani mhimili wa nne wa dola baada ya Utawala, Bunge na Mahakama. Inashangaza kuona watumishi wa mihimili mingine wakilindwa na kuheshimiwa huku waandishi wa habari wakiendelea kuishi kwa wasi wasi. Inasikitisha kuona hata mamlaka zinazojigamba kuwapo kwa ajili yakulinda raia na mali zake hazichukui hatua.
Umefika wakati wa waandishi wa habari kuanza kumsaka mbaya wao na kumfichua bila woga wala ajizi. Inasikitisha kuona waandishi wa habari wakitolewa kafara na manyang’au wanaolihujumu na kuliibia taifa kwa kutumia madaraka waliyopewa na umma.
Ifikie mahali waandish tukatae udhalili na utumwa huu. Japo wanandishi wa habari nchini hawezi kuwa kitu kimoja kutokana na kuzuka aina fulani la waandishi nyemelezi ambao hutumiwa kama nepi na wakubwa kuficha uchafu wao, waandishi makini na safi tushikamane tupamane na mfumo huu zandiki. Tusiendelee kugeuzwa mabunga kwa kuhadaiwa na tume za uongo na ukweli zinazoundwa pale wenzetu wanapouawa au kuumizwa kama iliyotokea kwa Kibanda. Pia tusiridhike na salamu na pole za wakubwa yanapotupata. Salamu si muhimu kama kutafuta suluhu na kujenga mazingira ya uwajibikaji haki na usawa.
Tunafahamu fika kuwa adui mkubwa wa waandishi wa habari ni waandishi wa habari wanaotumia matumbo yao kufikiri badala ya vichwa. Ni waandishi waliojigeuza nepi za wakubwa ambao wako tayari kuficha na kufumbia macho uoza ilmradi wanakatiwa kitu kidogo au kupewa vyeo vya uongo na ukweli kwa wale wanaotumikia taasisi au watu wachafu. Je waandishi wote wa habari tutajiruhusu kusaliti taaluma na maadili yake ili kupewa makombo na kuyafakamia kama wafanyavyo waandishi nyemelezi au makanjanja?
Umefika wakati wa waandishi wa kweli kusimama kidete na kuibana serikali ili ituhakikishie usalama na kufanya kazi bila vitisho wala bughudha sawa na wanajamii wengine.
Ninapoandika makala hii nafahamu waandishi wa habari tena nguli wanaoishi kwa shinikizo na hofu baada ya kupokea vitisho toka kwa mafisadi wanaowaona kama tishio la shughuli zao haramu za kulihujumu na kulizamisha taifa.
Nimewahi kupokea malalamiko toka kwa waandishi Ansbert Ngurumo, Mbaraka Islam, George Maziku na Evarist Chahali ambao wamekuwa wakipokea vitisho na wakati mwingine kuvipuuzia. Kwa lililomfika Kibanda, nawashauri waandishi ambao wamekuwa wakitishiwa maisha wachukue hatua hata kama itabidi kuondoka Tanzania kwa wale walioko huko. Maana inavyoonekana, serikali na taasisi zake hawako tayari kuwahakikishia usalama.
Ingawa magenge yanayoendesha hujuma dhidi ya waandishi yanaweza kushinda kwa kipindi fulani, hayatashinda milele. Je wataua wangapi? Nadhani dawa si kuua waandishi bali kuacha kutenda jinai dhidi ya taifa. Waandishi wengi hasa niliowataja hapo juu wanachukiwa si kwa sababu ya kumuonea wala kumhujumu mtu. Wanachukiwa, ima kwa kukataa kuwekwa mifukoni mwa mafisadi, au kuandika vitu vinavyowaudhi watawala na mafisadi. Tanzania ni nchi yetu kwa sawa. Ni mali yetu sote kuanzia rais hadi msukuma mkokoteni. Hivyo, hakuna mtu mwenye mamlaka wala haki kumtoa roho mwenzie kwa kulinda uchafu wake. Kwangu mimi kinachoendelea ni kichocheo cha kuwa mkali zaidi bila kujali matokeo. Kinachonisaidia tofauti na wengine ni kwamba niko mbali na makundi haya ya kiharamia.
Kwa wale walioko ndani ya nchi, hakikisheni mnapiga kelele na kusikika ingawa kuna gharama ya kufanya hivyo. Tanzania imefanikiwa kuwa na genge la wahalifu lisiloguswa na vyombo vya habari kwa sababu ya kutokuwa na Gutter Press. Magazeti haya fichi husaidia kufichua kashfa zenye kuwa tishio kwa waandishi wa habari kwa vile hayataji majina ya waandishi wala hayana ofisi maalumu na anayeyamilki huwa hajulikani. Kwa waliosoma chuo kikuu cha Dar es salaam watanakumbuka Punch. Mr Punch alikuwa anaogopewa na kila fisadi chuoni kwa kujua kuwa atamfichua na kutoa uoza wake bila ya mtoa taarifa kujulikana. Wenzetu Kenya wanayo Gutter Press ambayo hufichua maovu mengi ambayo magazeti ya kawaida huogopa kuandika kwa sababu za kisheria na kiusalama. Hufikia mahali vyombo vya habari vikapata fununu hata stori kama hizo na kuzirusha kwa Gutter Press ambayo huuzwa kwa bei nafuu kwenye vituo vya mabasi hata baa bila kubughudhiwa. Serikali zinazowajibika na kuchukia uoza huacha Gutter Presses zifanye kazi bila kuziingilia. Sasa ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na nyenzo hii ili kuendeleza mapambano dhidi ya ufisadi.
Chonde chonde, tusiigeuze Tanzania kaburi la waandishi wa habari. Hawa ni wajumbe tu wasiopaswa kutishwa kudhiriwa wala kuuawa. Wao ni sauti ya wasio na sauti na sauti ya umma isiyopaswa kuchukiwa wala kunyamazishwa.
Chanzo: Dira Machi, 2013.

No comments: