Mpendwa Anna,
Kwanza,
nisamehe. Sitakuita Anne kama unavyopenda kuitwa. Tunaokujua twajua wewe ni Anna
na si Anne. Enzi za Mchonga na zile za alikwina uliitwa Anna. Anne inasound
kisomi kuliko Anna. Umenikumbusha Musa Nnauye aliyejipachika Moses.
Tuyaache.
Pili,
nikufamishe. Huwa nazimia vitu vyako hasa kuburuza--- sorry---
kuongoza Mjengo. Napenda unavyokomesha wapingaji. Wewe ni shujaa kwenye chama
chako. Hawajui wewe ni kada nambari wani wa nambari wani? Walidhani utaruhusu
wavuruge ulaji wenu? Imekula kwao!
Nakupongeza,
naibu wako Jobless Nduguy na fyatu Pita Sheukamba aka mzee wa f*ck you.
Wamesahau Job alisema: Waishiwa wanakula bwimbwi? Je Pita alitoka kupata
bwimbwiz au hajui maana ya fwaki you? Tungejuaje anajua kimombo
tena cha mitusi? Kazi kwa waliofanya makosa kumchagua wasijue anawakilisha tumbo
na bangi zake? Siku hizi mitusi na sanaa ni sera ati. Ukisikia mheshimiwa
kuishiwa na kuwa muishiwa ndiyo huku.
Naandika
kukushukuru. Staili yako ya kuwakomesha wapingaji imenisaidia
kuwakomesha walevi kijiweni. Kama si kuiga mfano wako waingereza wauitao
bulldozing or maumauing, ningeshapigwa chini zamani. Believe me. Ubabe wako
uliniokoa na kusaidia kuendelea na ulaji wangu Kijiweni aka Mjengoni.
Hakuna kitu kinanikera kama wapingaji kujidanganya kuwa wana haki ya
kufaidi demokrasia wasijue yenu ni domoghasia yenye wenyewe ambao ni nambari
wani.
Acha nikupe
ushauri wa chee. Akiamka mpingaji kutoa hoja hata kama ina mashiko bamiza.
Akiinuka mwenzenu, hata kama anatoa pumba na kutukana fwaki you, minya aendelee
kuwapa vipande vyao. Hawajui ulisimikwa hapo baada ya mzee Sam Sixx kukaanga
chata pale aliposababisha kutoswa kwa Eddie Ewassa na baadaye mawaziri
wengine?
Juzi nilisikia
wapingaji wakilalamika kuwa unawaburuza na kupendelea chama chko. Noma ni nini?
Hakuna kitu kiliniudhi nusu nijinyotoe roho kama wapingaji eti kutaka kuja na
hoja ya kukuwajibisha wewe na Jobless ambaye wanamtuhumu kuongea bila kufikiri.
Hii ilinitokea Mjengoni kwangu hivi karibuni. Si walevi walitaka kuni-impeach
wakidai ninaiba pesa yao na kuwaburuza! Kama kawa, nilitumia mbinu yako ya
kuwatoa nje ya Mjengo na kupeta kama ulivyowafanyia akina Tundul Issu.
Kwa vile mimi
ni mpenzi na shabiki wako, kijiweni kwetu wananiita Makinda na majina mengi
mengine ya hovyo. Hakuna waliponikera kama kusema eti mzee Sam Sixx kweli
alikuwa kiongozi wa kupigiwa mfano tofauti na wewe na mimi wanaotuona kama
kanyabwoya na mawakala wa mafisadi.
Baada ya walevi
kuzidiwa kete si waliamua kufuatilia mambo yangu ya ndani kama vile ndoa na
nyumba zangu ndogo! Walipojua sijaoa walikuja na mambo ya kijinga kutaka mkuu wa
Mjengo wetu lazima awe ameoa au kuolewa! Pia wapo waliosema eti mkuu wa Mjengo
lazima awe amesomea sheria na awe msomi kweli tofauti na wewe wanayesema eti una
elimu ya kuungaunga. Kwa vile mimi ni msomi mwenye shahada magunia, waliamua
kukutumia kujiridhisha. Baada ya kuona wamezidi niliwapa live na kuwaambia: You
can go to hell kama Joni Malisela alivyowapa akina Agwe zama zile. Hata hivyo,
wana bahati. Angekuwa fyatu Pita Sheukamba angewaambia fwaki you all.
Una habari?
Yeyote aliyefanyiwa nchezo huo hudhani wote wanafanyiwa hivyo! Kuna mlevi
alituacha hoi alipouliza, “Huyu anayewowa na kufwaki watu anapata wapi jeuri?
ashukuru. Zingekuwa enzi za Mchonga anayewambia wenzie fagi you angefwagiwa yeye
ajikute hana kazi.” Alisema atakwenda Mwisho wa Reli kuwatafsiria mitusi
waliokuchagua fyatu Pita ili wasimchague tena kuwaangusha watu wastaarabu kama
wao. Yupo aliyesema kuwa Pita alitukana wana kaya wote, wewe hata mkuu maana
Mjengo ni sehemu takatifu.
Walevi ni
viumbe wa ajabu! Kweli walevi ni walevi katika kila kitu! Hawakosi la kusema
utadhani wanasiasa! Si juzi walisema eti huna lako. Eti kila
ufanyalo sharti uwe remote controlled na mafisadi waliokusimika kulinda uoza
wao! Laillah illallah! Niliposikia matusi haya nilirusha ngumi na kuwajeruhi
kadhaa ndipo waliamua kutoka unyoya na kikao kwisha bila maridhiano. Sikuona
haja ya kuendelea kuwatoa nje wakati wenzao wakibakia na kuendeleza libeneke ya
kutuacha uchi.
Hata hivyo,
kabla ya ngumi kufumka niliwapa laivu wanaokuchukia kuwa mwenye wivu ajinyonge.
Kama ulisimikwa na mafisadi kwanini nao inawauma nini?
Kuhusu la elimu
niliwapa wazi kuwa kwenye kaya yetu elimu nzuri au uzoefu kwa wanaojuana chini
ya dhana ya kulindana na kulipana fadhili, elimu na uzoefu si muhimu. Kama
mawaziri walighushi wazi na wanaendelea kutesa kwanini nawe usitese, kupeta na
kupetuka? Hata hivyo, nashauri. Badala ya kuendelea kusumbuliwa na madai kuwa
hukubukua ningeshauri uongee na chuo kimoja feki ndani au hata ng’ambo
wakuzawadie PhD kama yule rais wa Unyasani alivyofanyiwa hivi karibuni akafikia
hata kutumia pesa ya walevi kubadili picha zake ili ziwe na neno Dk.
Isitoshe,
hautakuwa peke yako. Huoni akina Dk Emmy Nchimvi na Dororas Kamala ambao
walizoea kuitwa madaktari wakati walikuwa kanjanja hadi juzi niliposikia kuwa
wamehitimu shahada za udaktari? Hata hivyo, nina wasi wasi kama wamehitimu zaidi
ya kuhitimishwa. Kama walishindwa mwanzo kutambua umuhimu wa kubukua hadi
wakaghushi kwanini wasiendeleze libeneke yao hasa ikizingatiwa kuwa hata mkuu
anakubaliana na jinai yao?
Nilipowabana
walevi watoe ushahidi kama ambavyo huwa unawafanyia wapingaji mjengoni, walisema
kuwa zilipotolewa shutuma kuwa ulikuwa umeandaliwa na kusimikwa na mafisadi
hukupinga wala huwa hutaki kujadili suala hili. Niliwauliza: So what? You can go
to hell. Hata hivyo, hawa jamaa ni wapumbavu wa kutupa. Walitaka ujibu shutuma
ili ziibuke nyingine nyingi ambazo hazijulikani siyo? By the way, ule mjengo
wako wa Sinza Uzuri umeishakamilika? Naomba unialike kwenye ufunguzi wake. Vipi
ile barabara ya Mto wa Ng’ombe uliyokuwa umefunga ushaifungua?
Sista
Anna,
Acha nimalizie
kwa kukupongeza kwa kulinda amani ya kaya yetu kwa kuwakomesha wapingaji.
Napendekeza waishiwa wa chama chako wawe wanaingia Mjengoni na kamusi za mitusi
ili kuwakomesha wapingaji. Pia Pita Sheukamba achaguliwe mwenyekiti wa kamati ya
mitusi akisaidiwa na Mwehuhuyu Michembe kuwakomesha wanaosumbua ulaji
wenu.
Nisalimie Pita,
Job na Lameck Michembe. Wambie nazimia vitu vyao pia.
“Blessed
be.”
Chanzo: Nipashe Jumamosi Aprili 27, 2013.