The Chant of Savant

Monday 29 April 2013

Makinda: Nakuzimikia (You're my heroine)









Mpendwa Anna,
Kwanza, nisamehe. Sitakuita Anne kama unavyopenda kuitwa. Tunaokujua twajua wewe ni Anna na si Anne. Enzi za Mchonga na zile za alikwina uliitwa Anna. Anne inasound kisomi kuliko Anna. Umenikumbusha Musa Nnauye aliyejipachika Moses. Tuyaache.
Pili, nikufamishe.  Huwa nazimia vitu vyako hasa kuburuza--- sorry--- kuongoza Mjengo. Napenda unavyokomesha wapingaji. Wewe ni shujaa kwenye chama chako. Hawajui wewe ni kada nambari wani wa nambari wani? Walidhani utaruhusu wavuruge ulaji wenu? Imekula kwao!
 Nakupongeza, naibu wako Jobless Nduguy na fyatu Pita Sheukamba aka mzee wa f*ck you. Wamesahau Job alisema: Waishiwa wanakula bwimbwi? Je Pita alitoka kupata bwimbwiz au hajui maana ya fwaki you?  Tungejuaje anajua kimombo tena cha mitusi? Kazi kwa waliofanya makosa kumchagua wasijue anawakilisha tumbo na bangi zake? Siku hizi mitusi na sanaa ni sera ati. Ukisikia mheshimiwa kuishiwa na kuwa muishiwa ndiyo huku.
Naandika kukushukuru.  Staili yako ya kuwakomesha wapingaji imenisaidia kuwakomesha walevi kijiweni. Kama si kuiga mfano wako waingereza wauitao bulldozing or maumauing, ningeshapigwa chini zamani. Believe me. Ubabe wako uliniokoa na kusaidia kuendelea na ulaji wangu Kijiweni aka Mjengoni.  Hakuna kitu kinanikera kama wapingaji kujidanganya kuwa wana haki ya kufaidi demokrasia wasijue yenu ni domoghasia yenye wenyewe ambao ni nambari wani.
Acha nikupe ushauri wa chee. Akiamka mpingaji kutoa hoja hata kama ina mashiko bamiza. Akiinuka mwenzenu, hata kama anatoa pumba na kutukana fwaki you, minya aendelee kuwapa vipande vyao. Hawajui ulisimikwa hapo baada ya mzee Sam Sixx kukaanga chata pale aliposababisha kutoswa kwa Eddie Ewassa na baadaye mawaziri wengine?
Juzi nilisikia wapingaji wakilalamika kuwa unawaburuza na kupendelea chama chko. Noma ni nini? Hakuna kitu kiliniudhi nusu nijinyotoe roho kama wapingaji eti kutaka kuja na hoja ya kukuwajibisha wewe na Jobless ambaye wanamtuhumu kuongea bila kufikiri. Hii ilinitokea Mjengoni kwangu hivi karibuni. Si walevi walitaka kuni-impeach wakidai ninaiba pesa yao na kuwaburuza! Kama kawa, nilitumia mbinu yako ya kuwatoa nje ya Mjengo na kupeta kama ulivyowafanyia akina Tundul Issu.
Kwa vile mimi ni mpenzi na shabiki wako, kijiweni kwetu wananiita Makinda na majina mengi mengine ya hovyo. Hakuna waliponikera kama kusema eti mzee Sam Sixx kweli alikuwa kiongozi wa kupigiwa mfano tofauti na wewe na mimi wanaotuona kama kanyabwoya na mawakala wa mafisadi.
Baada ya walevi kuzidiwa kete si waliamua kufuatilia mambo yangu ya ndani kama vile ndoa na nyumba zangu ndogo! Walipojua sijaoa walikuja na mambo ya kijinga kutaka mkuu wa Mjengo wetu lazima awe ameoa au kuolewa! Pia wapo waliosema eti mkuu wa Mjengo lazima awe amesomea sheria na awe msomi kweli tofauti na wewe wanayesema eti una elimu ya kuungaunga. Kwa vile mimi ni msomi mwenye shahada magunia, waliamua kukutumia kujiridhisha. Baada ya kuona wamezidi niliwapa live na kuwaambia: You can go to hell kama Joni Malisela alivyowapa akina Agwe zama zile. Hata hivyo, wana bahati. Angekuwa fyatu Pita Sheukamba angewaambia fwaki you all.
Una habari? Yeyote aliyefanyiwa nchezo huo hudhani wote wanafanyiwa hivyo! Kuna mlevi alituacha hoi alipouliza, “Huyu anayewowa na kufwaki watu anapata wapi jeuri? ashukuru. Zingekuwa enzi za Mchonga anayewambia wenzie fagi you angefwagiwa yeye ajikute hana kazi.” Alisema atakwenda Mwisho wa Reli kuwatafsiria mitusi waliokuchagua fyatu Pita ili wasimchague tena kuwaangusha watu wastaarabu kama wao. Yupo aliyesema kuwa Pita alitukana wana kaya wote, wewe hata mkuu maana Mjengo ni sehemu takatifu.
Walevi ni viumbe wa ajabu! Kweli walevi ni walevi katika kila kitu! Hawakosi la kusema utadhani wanasiasa! Si juzi walisema eti huna lako.  Eti kila ufanyalo sharti uwe remote controlled na mafisadi waliokusimika kulinda uoza wao! Laillah illallah! Niliposikia matusi haya nilirusha ngumi na kuwajeruhi kadhaa ndipo waliamua kutoka unyoya na kikao kwisha bila maridhiano. Sikuona haja ya kuendelea kuwatoa nje wakati wenzao wakibakia na kuendeleza libeneke ya kutuacha uchi.
Hata hivyo, kabla ya ngumi kufumka niliwapa laivu wanaokuchukia kuwa mwenye wivu ajinyonge.  Kama ulisimikwa na mafisadi kwanini nao inawauma nini?
Kuhusu la elimu niliwapa wazi kuwa kwenye kaya yetu elimu nzuri au uzoefu kwa wanaojuana chini ya dhana ya kulindana na kulipana fadhili, elimu na uzoefu si muhimu. Kama mawaziri walighushi wazi na wanaendelea kutesa kwanini nawe usitese, kupeta na kupetuka? Hata hivyo, nashauri. Badala ya kuendelea kusumbuliwa na madai kuwa hukubukua ningeshauri uongee na chuo kimoja feki ndani au hata ng’ambo wakuzawadie PhD kama yule rais wa Unyasani alivyofanyiwa hivi karibuni akafikia hata kutumia pesa ya walevi kubadili picha zake ili ziwe na neno Dk.
Isitoshe, hautakuwa peke yako. Huoni akina Dk Emmy Nchimvi na Dororas Kamala ambao walizoea kuitwa madaktari wakati walikuwa kanjanja hadi juzi niliposikia kuwa wamehitimu shahada za udaktari? Hata hivyo, nina wasi wasi kama wamehitimu zaidi ya kuhitimishwa. Kama walishindwa mwanzo kutambua umuhimu wa kubukua hadi wakaghushi kwanini wasiendeleze libeneke yao hasa ikizingatiwa kuwa hata mkuu anakubaliana na jinai yao?
Nilipowabana walevi watoe ushahidi kama ambavyo huwa unawafanyia wapingaji mjengoni, walisema kuwa zilipotolewa shutuma kuwa ulikuwa umeandaliwa na kusimikwa na mafisadi hukupinga wala huwa hutaki kujadili suala hili. Niliwauliza: So what? You can go to hell. Hata hivyo, hawa jamaa ni wapumbavu wa kutupa. Walitaka ujibu shutuma ili ziibuke nyingine nyingi ambazo hazijulikani siyo? By the way, ule mjengo wako wa Sinza Uzuri umeishakamilika? Naomba unialike kwenye ufunguzi wake. Vipi ile barabara ya Mto wa Ng’ombe uliyokuwa umefunga ushaifungua?
Sista Anna,
Acha nimalizie kwa kukupongeza kwa kulinda amani ya kaya yetu kwa kuwakomesha wapingaji. Napendekeza waishiwa wa chama chako wawe wanaingia Mjengoni na kamusi za mitusi ili kuwakomesha wapingaji. Pia Pita Sheukamba achaguliwe mwenyekiti wa kamati ya mitusi akisaidiwa na Mwehuhuyu Michembe kuwakomesha wanaosumbua ulaji wenu.
Nisalimie Pita, Job na Lameck Michembe. Wambie nazimia vitu vyao pia.
“Blessed be.”
Chanzo: Nipashe Jumamosi Aprili 27, 2013.

No comments: