The Chant of Savant

Thursday 23 July 2015

UKAWA hawana sababu kumuogopa Magufuli

Image result for photos of magufuli and ukawaImage result for photos of magufuli and ukawa
       Hakuna ubishi kuwa mgombea mteule wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli ana ushawishi mkubwa nchini. Hata hivyo, hii si sababu ya wapinzani chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kumgwaya.
Baada ya kuteuliwa Magufuli, wengi walisikika wakisema sasa kiatu kimepata mvaaji. Ni kweli, lakini hata UKAWA wanao wavaaji wa kiatu sawa na Magufuli. Katika kuthibitisha hilo Dk Makaidi ambaye pia ni Mwenyekiti wa NLD kinachounda UKAWA alikaririwa akisema, “Hatustushwi na (Dk John) Magufuli kwa lolote na mashambulizi yetu yatakuwa makubwa. Lengo letu la kuiondoa CCM madarakani liko palepale.” Maneno ya Makaidi yana ukweli. Wale wanaodhani wapinzani wanamgwaya Magufuli wanataka apitishwe bila kushiriki uchaguzi?
Nadhani Makaidi ana sababu nzuri tu za kusema hawatishwi na Maguguli. Anasema, “Ajenda na hoja tulizonazo ndizo zitakazotubeba mbele ya wananchi… tutawapelekea ili waamue wakiwa na taarifa sahihi. Kama ni kutowajibika au ufisadi ndani ya CCM, suala hilo linaanzia ngazi ya juu mpaka kwa mwanachama wa kawaida.” UKAWA bado wana imani kuwa wananchi watawaelewa hasa pale watakapowakumbusha utendaji mbovu wa CCM.
Pia ni vizuri tukaamini kuwa kwenye siasa lolote linaweza kutokea. Nani aliamini kuwa rais Uhuru Kenyatta wa Kenya angemshinda waziri mkuu wa zamani Laila Odinga ambaye hata rais wa zamani Mwai Kibaki alimgwaya kama umeme? Japo siasa za Tanzania na za Kenya ni tofauti, bado ni mapema kwa yeyote kusema atashinda. Hatujui wananchi hasa wapiga kura wanafikiri nini na wataamua vipi. Hivyo, ushauri wa maana hapa ni kwa wagombea wote kutobweteka na umaarufu walio nao bali kwenda kwa wananchi na kueleza sera zao ili wapate nafasi nzuri ya kuamua.
Japo Magufuli anajulikana kwa utendaji wake, vile vile chama chake kinajulikana kwa utendaji mbovu. Hii dichotomy, au ndiyo siyo ni vizuri ikazingatiwa katika kuelekea uchaguzi ujao. Sidhani kama wananchi ambao bado hawana barabara maji wala umeme wana wanachoona ni bora kwa Magufuli. Sidhani kama wananchi ambao ardhi yao imetwaliwa ima na wawekezaji au viongozi wa CCM wanacho cha mno wanachokiona CCM. Sidhani wajawazito wanaotimliwa na manesi kiasi cha kuzalia vyooni wanacho cha mno katika CCM.
Kimsingi, hali ya CCM bado ni ngumu sema unafuu ilio nao ni kuwa na mgombea ambaye hana tuhuma za ufisadi ua uzembe. Kwa umaarufu, uchapakazi na uzalendo alio nao Magufuli anaweza kushinda.  Lakini CCM itegemee kuwa na hali ngumu kwenye ubunge. Maana wabunge wengi wanaomaliza muda walichakachua kiasi cha wengine kuchukiwa vibaya sana kwenye majimbo yao. Sijui wabunge kama hawa watarudi. Sidhani –kwenye uchaguzi ujao –kama wananchi wataruhusu uchakachuaji kama ule tulioushuhudia mwaka 2010. Nadhani wananchi sasa wamechoka na wako tayari kusimamia haki zao kuliko wakati wowote katika historia ya taifa letu. Hivyo, CCM wanapaswa kulizingatia hili huku na wapinzani wakizidi kuhanikiza kufichua maovu ya CCM kama taasisi badala ya kuhangaika na mtu mmoja.
Nadhani Makaidi anaposema tutabebwa na hoja anatoa onyo kwa CCM kuwa wasibwete na Magufuli. Wanajua fika kuwa mtu hawezi kuzidi chama. Wana mifano hai ya watu waliongia wakiitwa Mr Clean wakaondoka wanaitwa Mr Dirt.
Kitu kingine wanachopaswa kuzingatia wananchi si ukubwa jina la mtu wala umaarufu wake bali sera anazokwenda nazo kwao na utekelezaji wake.
CCM pamoja na Magufuli wanapaswa kujifunza toka kwenye mchakato wao ulioisha na kumuibua Magufuli. Nani alijua kuwa Magufuli angewapiku vigogo waliokuwa wanajiamini kuwa ndiyo watakao kuwa wao kwenye kupeperusha bendera ya CCM? Nani alitarajia vigogo kama Edward Lowassa, Bernard Membe na Mark Mwandosya kuangukia pua na kushindwa na rookie kama Magufuli? Huo ndiyo uchaguzi. Si vyema kuwasemea wapiga kura au kujaribu kutabiri watafanya nini. Kinachopaswa kufanya kwa pande zote ni kuheshimu kanuni na kupeleka sera kwa wanachi huku wale walioko madarakani wakitakiwa kutoa maelezo yanayoingia kichwani pale walipoboronga.
Kama watanzania watajifunza tokana na makosa yao, tunaweza hata kutegemea maajabu. Jakaya Kikwete aliingia na sifa nyingi za kweli na za uongo. Je anaondoka na hizo sifa tena? Unategemea nini kama wapinzani watatumia udhaifu wa Kikwete wakiupambanisha na ahadi na sifa alizoingia nazo kumbomoa Magufuli? Kwangu mimi ngoma hii bado ni mbichi na lolote linaweza kutokea kufikia Oktoba.
Mfano mzuri ni ile hali ya Magufuli kuanza kuona hatari inayokabili chama chake hasa kuhusiana na ufisadi. Ameanza kuto ahadi za kutomugopa yeyote wala kumuonea. Je hii inatosha? Atakapokwenda kwa wananchi watamuuliza nini atakachofanya kuhusiana na mazimwi kama EPA, Richmond na Escrow. Majibu atakayotoa na usayansi wake vinaweza kuwa vigezo amuzi kuliko mtaji alio nao wa kuwa mchapakazi bora na kusifika kusimamia ujenzi wa barabara. Je hizo barabara zinakidhi viwango au kulingana na kiasi cha fedha kilichotumika kuzijenga? Maswali mbona yapo mengi kuanzia ya barabara hadi nyumba za umma zilizouzwa chini ya usimamizi wake.
Tumalizie kwa kuzishauri pande zote kujikita kwenye masuala badala ya personalities.
Chanzo: Dira Julai 23, 2015.

1 comment:

Anonymous said...

Ana nini Magufuli
Tumeona mafunguo na yote yalipita
Wote wale wake CCM kifo cha Mende