Baada ya Chama Cha Maulaji (CCM) kupitisha mtu wao wa kugombea urahis, Dk Kanywaji Makufuli, wabongo wamechachawa kiasi cha kuanza kumshabikia na kumuona kama ndiye rahis ajaye wasijue hiyo siyo inshu. Kijiwe pamoja na kumpitisha mzee mwenye Mpayukaji Msemahovyo kugombea urahis, kinawataka wachovu wamchague yeye kwa vile amejipambanua na mafisadi majambazi, wauza mihadarati wazembe na wasanii.
Mgosi Machungi anaoneyesha shaka yake, “Hebu tisaidiane. Juzi tiiona wagombea wa CCM wakitanua kia mahai wakipiga kampeni wakidai wanajitambuisha. Je hayo magari na madege wanayotumia siyo ya umma kwei? Wanatumia njuluku za wachovu kumnadi bwana Kanywaji Makufuli huku mzee akitumia ya kahawa.” Anageuka na kunitazama na kutabasamu.
Mpemba anaamua kula mic, “Yakhe huyo Kanywaji Makufuli ni ni wale wale ati. Kambale wote wana sharubu na huu nchezo wa kutumia raslimali zetu kunadi walaji wao twapaswa kuupinga kwa nguvu zetu zote wallahi.”
Sofia Lion aka Kanungaembe leo anaingia mapema. Anakula mic na kusema, “Hivi mnaodai zinatumika njuluku za umma mna ushahidi gani au ni yale yale ya kumsingizia mheshimiwa Luwasha kuwa ni fisadi msilete ushahidi mlipotakiwa kufanya hivyo?”
Mijjinga anajibu, “Da Sofi una matatizo gani ndugu yangu? Hivi juzi hujasoma gazeti la Mchovu lilioandika jinsi Njaa Kaya alivyomkaanga rafiki yake kwa kusema wazi kuwa utajiri aliotuhumiwa kuwa nao wakati wa mzee mchonga umeongezeka maradufu?”
“Jamani achana na habari za Luwasha. Hizo habari na utetezi muachia Kimdunge Ngumbaru Mwehu anayelipwa kwa kazi hiyo. Tunachoongelea hapa ni matumizi ya raslimali za umma kwenye kampeni za chama fulani. Hivyo, tunachopaswa kudurusu ni hiki si akina Luwasha ambao wamefutwa kwenye ramani ya siasa za wachovu,” anajibu Msomi Mkatatamaa huku akibofya ki-sumsung galaxy 6 chake.
Kanji anaamua naye kula mic mapema, “Hii Kanyaji Kufuli iko very powerful. Kama pinjani pana pata mtu iko na guvu kuba hii Kufuli naweza funga yeye.” Kijiwe hakina mbavu anavyobukanya Kiswahili ambacho anajifanya kutokijua wakati anakifahamu vizuri tu.
“Ni kweli Makufuli ana nguvu usipime ingawa bado wapingaji tunaweza kumuangusha. Nina imani na kidume chetu mzee Mpayukaji Msemahovyo. Hivyo, sina shaka ya ushindi ingawa hili la kutumia njuluku zetu linapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote. Hii ni aina fulani ya uchakachuaji ambapo wagombea wa chama twawala wanaanza kampeni kabla ya wenzao,” analalamika Kapende.
Mipawa anaamua kutia guu, “Mie sioni tishio la Makufuli hasa ikizingatiwa kuwa mtu binafsi hata angekuwa msafi namna gani, anapowakilisha chama kichovu na kichafu anapigwa chini tu. Nadhani tunachopaswa kufanya ni kushinikiza wahusika waache kucheza rafu kwa kuanza kampeni kwa kisingizio cha kujitambulisha kabla ya kipenga kupulizwa.”
Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu, “Japo ni kweli Kanywaji ana nguvu sana kutokana na uchapakazi wake, chama chake kina kashfa lukuki ambazo anapaswa kueleza anavyoweza kujitenga nazo wakati naye alikuwa kwenye lisirikali lile lile. Pia ningependa nimsikie anasema nini kuhusu kashfa kama EPA, Richmonduli na Escrow vinginevyo nakubaliana na Ami wote ni wale wale tu. Kambale ndani ya dimbwi lile lile.”
Mzee Maneno naye anakwanyua mic na kuronga, “Mimi sioni kama tuna haja ya kumgwaya Makufuri. Kama yeye ameweza kuwapiga chini wagombea tishio kama Luwasha, kwanini nasi tusimpige chini pamoja na kutojulikana wala kuwa na makandokando mengi kama haya anayopewa? Nadhani kujulikana kungekuwa dili basi Luwasha angekuwa sasa anachekelea badala ya kuugulia na kulalamika akimtumia babu yake mzee Kimdungu Ngumbaru Mwehu.”
Kapende anakwanyua mic tena, “Pamoja na yote, mimi nina tabu na huyu manzi Suluhisho aliyeteuliwa na Kanywaji. Je mnaweza kutupa CV yake? Maana naye hajulikani hata kidogo. Mie nilidhani Aminia angetesa baada ya kuanguka chali kumbe Kanywaji alikuwa na mtu wake! Kweli CCM chama cha mizengwe!”
Msomi anarejea na kusema, “Huyu manzi asikupe taabu. Una habari kuwa makamu wa rahis hapa kayani huwa si kazi zaidi ya kufungua matamasha na mikutano tu? Kwa ufupi ni kwamba huyu manzi alikuwa waziri kwenye lisirikali la muuganiko na hakujulikana sana. Ila ukimchunguza ni bora kuliko Aminia au Saidia Mkuyati kihiyo aliyepewa uwaziri wa njuluku wakati ni kihiyo kama naibu wake Adam wa Milima ya Kigoma.”
“Msomi unaongelea vihiyo? Hujaona mama Kipaza Sauti Anayecheza Makidamakida alivyoogopa kuchukua fomu kwa vile hana digrii ingawa siku zote hupenda kujionyesha kama msomi wakati ni kihiyo aliyevuruga mjengo wetu kwa kuwakingia kifua mafisadi?”
Mijjinga anarejea tena na kula mic, “Mie nadhani tusihangaike na wagombea wa CCM. Tumpe tafu mgombea wetu mzee Mpayukaji na ikiwezekana kesho aitishe mkutano wa waandishi wa habari na kulaani huu uchafu wa kutumia raslimali za umma kupiga kampeni chini ya kisingizio cha kujitambulisha. Wanajitambulisha kwani wao si wabongo au janja tu ya kucheza rafu?”
Kijiwe kikiwa kinaanza kunoga si ukapita msafara wa Dk Kanywaji akielekea zake Mbagala kwenda kupiga kampeni. Acha tumzomee kwa kuanza kampeni kabla ya wakati wake!
Chanzo: Tanzania Daima Julai 22, 2015.
No comments:
Post a Comment