Baada ya kung’atuka madarakani na baadaye chamani kwa muanzilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) marehemu Mwl Julius Nyerere kilipata pigo ambalo pengo lake limeshindwa kuzibika. Maana, tangia wakati ule –karibu kila mwaka –CCM imekuwa ikiendelea kuporomoka hadi kuishi kwa matumaini na ubangaizaji utokanao na mchezo wa rafu kama vile kuchakachua uchaguzi na kufadhiliwa na mafisadi.Hivi karibuni mkongwe mwingine –kati ya wachache waliobakia na waliowashinda makuwadi na wasaka urais –mzee Joseph Warioba alikiasa chama chake ingawa sijui kama kitamsikiliza hasa ikizingatiwa uhuni aliokwishafanyiwa na wakubwa wa chama na serikali.
Warioba
alikaririwa akisema, “CCM inakabiliwa na wakati mgumu wa kupitisha jina la
mgombea urais kutokana na waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 38, na
mpaka sasa imekuwa ni vigumu kutabiri atakayepitishwa, jambo ambalo
halikujitokeza wakati wa upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995
na 2005.” Anachobainisha jaji Warioba hapa ni kwamba demokrasia lazima iwe na
mipaka. Wote tunajua kuwa uhuru bila mipaka ni wendawazimu. Kimsingi, sasa
kinachoitwa demokrasia ndani ya chama kisicho na historia ya demokrasia zaidi
ya kuipinga si demokrasia kitu bali wendawazimu na uroho wa madaraka wa kawaida.
Haiwezekani watu wastaarabu wenye kukubaliana na kuelewana wakaruhusu kila
mmoja autake ukuu. Je kama mwili wote ungekuwa sikio kichwa kingekuwa wapi?
Mbona vyama vya upinzani ambavyo viliteseka na kuhakikisha taifa linaingia
kwenye demokrasia ya vyama vingi havina utitiri wa wagombea?
Wahenga
walisema: Sikio la kufa halisikii dawa. Warioba kwa mapenzi na uzalendo wake
vilivyotukuka amejitahidi kuwasaidia wenzake. Je watamsikiliza wakati
walishamdhalilisha hasa baada ya kuwapa ukweli ambao hawakutaka kuusikia? Nani
amsikilize mzee aliyepitwa wakati kama Warioba ambaye badala ya kuchangamkia
madili anahagaishwa na maadili? Warioba ni sawa na mtu aliyeko nyikani. Warioba
amejitahidi kufanya kile ambacho kimewashinda wengi. Amejitofautisha na akina
Kingunge Ngombale Mwiru na Paskari Ndejembi wanaoweza kukodiwa na watia nia
kama bodaboda. Amewashinda akina Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Salmin
Amour na Amani Karume wanaoonyesha kuvizia upepo. Warioba amefanya kile ambacho
waingereza huita to stand up and be
counted au kuwa tayari kufanya maamuzi magumu hata yakimaanisha kulaumiwa.
Hakika wamebakia wachache wa namna hii. Laiti CCM ingewasikiliza.
Warioba
aliongeza, “Waliotangaza
nia wamekuwa wakieleza sera zao na ukiwasikiliza unaona kama walikuwa wagombea
binafsi hivi kwa sababu CCM ina sera, wanayo ilani ambayo ipo tayari na yeyote
atakayepeperusha bendera ya CCM lazima ajikite kwenye ilani ya chama.” Kama
siyo sikio la kufa au tuseme kuchanganyikiwa na kuparaganyikiwa ni nini kwa
chama ambacho kilitumia kila hila kupinga mgombea binafsi kujikuta kikiwa na
wagombea wenye kila sifa za mgombea binafsi? Je ni laana au historia kutaka
kurekebisha mambo? Je CCM watauvuka huu mtihani unaolenga kupima na kuonyesha
unafiki na upogo wao salama bila kuwasikiliza akina Warioba? Je kama hali ni
hii CCM inayokutana hivi karibuni kuteua na kupitisha mgombea wake itampata
wapi wakati waliojitokeza wote hawafai na wala hawana mpango na sera zake?
Laiti akina Abdulramahan Kinana katibu mkuu wa CCM wasingekuwa wamejiingiza kwenye
siasa za usanii walipaswa kuwa na kibarua kigumu cha kuueleza umma mantiki ya
kupambanisha wagombea binafsi kumpata mgombea wa chama.
Je kwa CCM
kutekwa na wagombea binafsi hadi ikawahalalisha kama wagombea wa chama siyo
kuishiwa na kugeuka chama tegemezi ambacho hakina mtaji zaidi ya kutegemea
ubabe wa watia nia? Je CCM hii kipofu itashidwa kumpitisha fisadi kama
alivyowahi kutahadharisha mmojawapo wa wagombea ambaye pia ni mtoto wa wa
mwanzilishi wa CCM, Makongoro Nyerere aliyekaririwa akisema, “Mojawapo ya
matatizo ya chama chetu ambayo ni lazima Rais ajaye apambane nayo ni ukweli
kwamba kuna majimbo ya uchaguzi hapa Tanzania ambayo kama mtu hutoi rushwa
huwezi kupita.” Maneno ya Makongoro ambaye amejizolea umaarufu kwa kusema
ukweli ni ushahidi tosha kuwa bila kuwa fisadi au tajiri CCM hupenyi. Je CCM
itavuka kikwazo hiki wakati imekaa kimya wakati fedha zikimwagwa hata kabla ya
kipenga cha mwisho kupigwa?
Je nini wana
CCM na watanzania wengine wategemee? Jaji Warioba ana jibu, “Hawa ndio
watakwenda kuchuja, sasa hapa itakuwa kazi ngumu na inawezekana kukawa na
mgongano wa maslahi na hilo lisipoangaliwa linaweza kufanya mchujo ukaonekana
kuwa haukuwa wa haki. Jambo hili linatakiwa kuangaliwa na hasa kwa kuwa kuna
makundi.” Kwa lugha rahisi ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa CCM kuanguka
kwenye mtego ikaamua kutokana na msukumo wa mtu na si sera. Hali inazidi kuwa
mbaya hasa ikizingatiwa kuwa CCM ina gonjwa kubwa sana la mitandao ya kimaslahi
ambapo karibu kila kiongozi ana mtandao wake kuanzia watangaza nia hata wale
watakaowachuja.
Tumalize kwa
kusema kuwa CCM sasa ni sikio la kufa ambalo halisikii dawa. Je CCM watamsikiliza
au kumpuuzia mzee Warioba?
Chanzo: Dira Julai 13, 2015.
No comments:
Post a Comment