Baada ya kutangaza au kutia nia kwa
wanachama wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wengi tulihoji mantiki ya wageni
nao kutaka urais tena kupitia chama chenye kila aina ya mizengwe. Wageni hawa
katika siasa za ki-CCM si wengine bali jaji mkuu wa zamani Augustine Ramadhan
au mwanadiplomasia ambaye hakuonyesha tangu mwanzo kuwa angejiingiza kwenye
siasa Augustine Mahita ni ushahidi kuwa CCM imechafuka kweli kweli.
Kwa wanaojua
mchezo huu mchafu wa siasa, walihoji zaidi mantika ya wahusika hawa
walioonekana kuwa wanagezi, wasio na mitandao wala uchafu kujiingiza kwenye
tanuri la moto. Wapo walioona kuwa CCM baada ya kufilisika kimikakati, kimbinu
na kimaadili–tokana na kuwa vigogo mafisadi, wazee, wachovu na wachafu–kama iliwahitaji
wahusika lau kuweza kupata mtu safi wa kuinasua kwenye mitego iliyomo. Kudhani hivyo ilikuwa kosa. Kwani, wapo
walioona kuwa wageni hawawezi kuaminiwa madaraka makubwa kama haya wakati
wakubwa wa chama wakiwa na skandali kibao ambapo wangetaka mwenzao wa kuwalinda.
Nani–kwa mfano–angemwamini mwanajeshi–tena mwenye wa cheo cha juu na
mwanasheria jaji–urais ili awaumize wenye maskandali yao?
Sasa jogoo –sijui bata –limewika
Dodoma. Walioonekana kuwa safi wameenguliwa, waliovuma kadhalika. Badala yake,
wameletwa wengi ambao hawakutarajiwa. Kwa kuwakatas wasafi, CCM imeonyesha na
kuziweka wazi hisia kuwa haiwezi kuhitaji watu wa namna hii kwa kuogopa
kuigeuka kuwa kweli. Kwa kuwaengua
makada wake wenye ushawishi mkubwa, si ajabu CCM ikajikuta mahali ilipoishia
KANU nchini Kenya kama makada hawa kama vile Edward Lowassa, Fredrick Sumaye na
wengine wataamua kujiunga na upinzani kwenye uchaguzi ujao chini ya makubaliano
fulani. Je kwa siasa za Tanzania hili linawezekana? Nina shaka nalo.
Pia ukweli
kuwa mgombea mmojawapo aliyepenya, John Pombe Magufuri si mwenye mawaa mengi,
linafanya kambi zote mbili yaani CCM na upinzani kupata wakati mgumu. Kama
mitandao ya CCM itaunganisha nguvu, upinzani utakuwa na kibarua kikubwa japo
inategemea kati ya watano waliovuka kihunzi cha kwanza atachomolewa nani. kama
tulivyosema hapo juu, CCM itakuwa na kazi ngumu ya kuja na mtu anayeuzika
ambaye katika watano waliopita
anajulikana kutokana na utendaji kazi wake.
Tukirejea juu
ya ni kwanini Mahiga na Ramadhin wasingepita, walikuwa na sifa moja kubwa ya
usafi tofauti na wenzao. Maana, zaidi yao, wote waliojitokeza walikuwa wachafu
bila kujali sifa ndogo ndogo walizojipa ili kuwazuga na kuwaingiza mkenge
wananchi na wapiga kura. Wapo
waliochafuliwa na uroho, tamaa, au udokozi kama mwenzao alivyowahi kuwananga.
Wapo waliochafuliwa na uongo yaani kusema hili wakatenda hili. Wengine walikuwa
na sifa ila umri uliwatupa mkono hasa ikizingitiwa kuwa wengi walianza na awamu
ya kwanza na sasa wako na tano. Wapo wababaishaji waliokuwa wakitafuta sifa na
namna ya kuwa karibu na atakayepitishwa au kushinda ili wapate mlo wao. Hawa
kimsingi, ni waganga njaa au wachumia tumbo wanaotafuta ulaji mdogo na si ulaji
mkubwa kama urais. Walikuwapo waviziaji wanaotegemea kubebwa ima na jinsia zao
au makundi na upuuzi mwingine. Walikuwapo akina Uvuruge waliolenga kuwakwamisha
wenzao kama si kutumiwa na mahasimu wao. Walikuwapo wasaka umaarufu wa shilingi
mbili na upuuzi mwingine kama huo, pia wapo wasiojua hata kilichowasukuma
kugombea.
Kwa mfano unajiuliza mantiki ya
kapuku aliyetegemea michango ya hisani kugombea tena kwa kutoa milioni moja
aliyoomba. Je huyu kweli alikuwa serious? Je alikuwa akitafuta nini kama si
umaarufu na wengine kuondoa ushamba kwa kupata fursa ya kuchangiwa waizunguke
nchi? Hata ukiwauliza wote waliokuwa wamejitokeza nini sera zao, utaambulia
maajabu. Wengi hawakujinadi kwa sera zaidi ya sifa binafsi.
Wageni
walikuwa bora. Lakini kuwaamini ilikuwa vigumu kwa kuhofia hatari ambayo wengeweza kusababisha wakiwa madarakani
hasa kufumua uoza uliopo ambao ndiyo njia kuu ya ulaji kwa walio wengi
madarakani.Hivyo, hawa walifaa kwa umma lakini walikuwa hatari kwa mafisadi. Pia upo upande
wa pili. Sasa CCM imeonyesha wazi kuwagwana na kutowaamini wasafi. Je upinzani
utalitumiaje hili kubadili upepo?
Kama watanzania wataamua kutorudia
makosa, hawana sababu hata moja ya kuichagua CCM tena. Kwani licha ya kuzeeka,
kuchoka, imeishiwa na kuisha kiasi cha kustahiki kupumzishwa lau ijifunze. Na
hakuna haja ya kuogopa kuiwajibisha CCM. Kwani, haitakuwa ya kwanza. Tuliona vigogo
wenzake kama KANU (Kenya) MCP (Malawi), UNIP (Zambia) na vingine vingi
vilivyolizwa na nchi zikasonga mbele. Hivyo, kupata wagombea kama watajawa hapo
juu bado si dawa kwa CCM ambayo haina tofauti na sikio la kufa.
Kimsingi
Mahiga na Ramadhani wanaonyesha uoza wa CCM ambao hawawezi kuundoa kutokana na
kanuni na ushawishi wa ndani ya chama. Hivyo, hata kama mmojawao angepitishwa
wasingebadili lolote zaidi ya kubadilishwa. Kwa majina yaliyopitishwa, bado CCM
ina kazi hasa kama waliotemwa wataamua kuiadhibu kwa kujiunga na upinzani kama
ilivyotokea Kenya mwaka 2002.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 19, 2015.
No comments:
Post a Comment