Tunaandika haya kumtaka rais John Magufuli kujipanga kutumbua majipu mengine makubwa yatokanayo na mfumo mbovu aliourithi ambapo watu wasiostahiki wanalipwa stahiki wasizostahiki. Mfano mzuri ni Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani aliyeachia madaraka si kwa kustaafu, bali kutokana na kuwajibika tokana na kujiridhisha kuwa alishiriki kwenye kashfa iliyopoteza mabilioni ya shilingi za umma. Wapo wanaoamini kuwa Lowassa –kisheria –hapaswi kulipwa marupurupu ya kustaafu kama waziri mkuu, kwa vile hakustaafu kwa mujibu wa sharia bali kulazimika kuachia ngazi tokana na ushiriki wake kwenye kashfa ya Richmond. Wanaoamini hivyo wanadhani Lowassa analipwa mafao asiyostahiki ima kutokana na mfumo mbovu wa kulindana au urafiki wake na rais wa mstaafu, Jakaya Kikwete.
Kadhalika, kuna haja ya kuwa na sheria inayozuia mstaafu ambaye yuko active kwenye siasa kama Lowassa na Fredrick Sumaye, kulipwa mafao ya ustaafu wakati bado anafanya siasa. Hivyo, si vibaya kumshauri rais kuwachukulia wahusika kama majipu yanayopaswa kutumbuliwa ili kuokoa fedha nyingi za umma na stahiki kama vile walinzi, wafanyakazi wa nyumbani, matibabu, na mengine wanavyopata kinyume cha sheria. Huu nao ni wizi wa kimfumo ambapo mtu analipwa mabilioni asiyostahili.
Lowassa –japo amejitofautisha na mafungamano na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuingia kwenye upinzani, anapaswa kuangaliwa si kwa sababu ni mpinzani bali mtu aliyeachishwa kazi kwa kashfa tena ya upotevu wa fedha za umma sawa na wahusika wengine waliosimamishwa kazi kutokana na kosa au makosa kama haya. Hivyo, tuweke wazi. Hatumshauri rais kutumbua jipu hili kwa vile Lowassa yuko upinzani. Tunasema hili wazi kwa vile –ikitokea Lowassa akanyima marupurupu anayofaidi kwa sasa –bila shaka atakuja na utetezi hafifu kuwa anafanyiwa hivyo kwa vile yuko kwenye upinzani. Hata angekuwa ndani ya CCM , bado asingestahili kulipwa marupurupu anayopewa –kama sheria na kanuni zitafuatwa bila kulindana na kuangalia u-mwenzetu.
Sumaye –kadhalika –anaangukia kwenye mkumbo huu wa kufanya siasa –japo kisiasa analipwa kama mstaafu. Huwezi kustaafu na ukaendelea kufanya shughuli zile zile bado ukastahiki kulipwa marupururup. Tunadhani, huu nao ni uchochoro unaowagharimu walipa kodi bila sababu. Hivyo, si vibaya majipu haya nayo yakatumbuliwa sawa na majipu mangine.
Kwa vile sera ya Magufuli ni kubana matumizi yasiyo ya lazima, kuna haja ya kuangalia hata haya malipo ya viongozi wastaafu. Kwani nayo yanakula na kupoteza fedha nyingi bila sababu wala stahiki.
Kitendo cha kuendelea kumlipa stahiki za ustaafu Lowassa wakati hakustaafu ni moja ya vikwazo kwa uwajibikaji kwenye ofisi kubwa za umma. Analipwa kwa lipi wakati hakuleta tija bali hasara? Kinachofanya Lowassa asistahili kulipwa marupurupu ni ukweli kuwa alifanya maamuzi magumu na kuamua kuachia ngazi mwenyewe baada ya kujiridhisha kuwa alikuwa na kesi ya kujibu ingawa hakufikishwa mahakamani. Kama kweli tunataka kuwajibishana na kuonyesha mfano, mtu kama Lowassa alipaswa kufunguliwa kesi mahakamani na kusafishwa huko huko badala ya kuendelea kupoteza fedha ya umma kumlipa marupurupu asiyostahili.
Marupurupu anayolipwa Lowassa, angalau yangeelekezwa kwa familia ya marehemu Edward Sokoine aliyefia ofisini baada ya kulitumikia taifa kwa uwajibikaji na ufanisi mkubwa. Haiingii akilini serikali kusema kuwa atakayevuruga asihamishiwe sehemu nyingine bali kufukuzwa halafu kwa upande mwingine ikaendelea kuwalipa fedha watu waliofukuzwa kama wastaafu wakati hawakustaafu. Lazima itungwe sheria kuwa: Ili kiongozi mstaafu astahiki kulipwa marupurupu ya ustaafu aishi kama mstaafu badala ya kuwa mwanasiasa active na kuendelea kupokea fedha ya umma. Pia sheria itamke wazi kuwa atakayefukuzwa –kama ilivyo sheria kwa watumishi wengine wa umma –anapoteza stahiki zake kwa vile hakutimiza masharti ya utumishi wake kwa umma. Hata Lowassa mwenyewe anajua fika kuwa anafaidi marupurupu anayopewa kwa vile mfumo wetu ni wa kifisadi, kulindana na kupendeleana ukiachia mbali kuzawadiana kutokana na ukuruba na usuhuba.
Kwa kuweka sheria inayowataka viongozi kuwajibika ndipo walipwe marupururupu ya ustaafu, tutaweza kutoa motisha kwa viongozi hawa kuwajibika kwenye ofisi za umma badala ya kuzitumia kwa maslahi binafsi na waondokapo –ima kwa kustaafu –au kuwajibishwa wakaendelea kupoteza fedha za umma. Mfano mzuri ni waziri mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Olmet aliyehukumiwa kwenda jela kwa kosa alilotenda akiwa meya wa jiji la Jerusalem.
Tumalizie kwa kushauri kuwa Lowassa asimamishwe kupokea marupurupu ya ustaafu kwa vile hakustaafu, aliachia madaraka tokana na kujiridhisha kuwa alihusika kwenye kashfa ya Richmond hata kama hajafikishwa mahakamani. Vinginevyo afikishwe mahakamani na mahakama iamue ili wananchi wajue ukweli badala ya kuendelea kuwa utata uliopo. Wakati wa kuwajibishana ni sasa ili kuweka mfano kwa watakaokuja wakijua fika kuwa ofisi za umma na fedha za watanzania si shamba la bibi tena. Tunaomba kutoa hoja kwa rais Magufuli ambaye tunajua fika kuwa anawasikiliza wananchi anaotaka kuwatumikia na kuwakomboa toka kwenye kadhia ya wizi na matumizi mabaya ya ofisi na fedha za umma.
Chanzo: Dira Januari 18, 2016.
2 comments:
Salaam Mwalimu Mhango,
Kwa makala yako hii wache mm nianzie pale ulipomalizia kwa kushauri ulipoandika kuw" Lowassa asimamishwe kupokea marupurupu ya ustaafu kwa vile hakustaafu, aliachia madaraka tokana na kujiridhisha kuwa alihusika kwenye kashfa ya Richmond hata kama hajafikishwa mahakamani. Vinginevyo afikishwe mahakamani na mahakama iamue ili wananchi wajue ukweli badala ya kuendelea kuwa utata uliopo".Kwa vile umeongelea kuhusu swala la mfumo mbovu uliopo ndani ya CCM chama ambacho kimetawala kwa miaka yote 37 hadi hii leo na kumtaka Rais magufuli kuufumua mfumo huo mbovu ndani ya CCM ni kumuhukumia hukumu ya kifo kwani hayo yatakuwa ni mapinduzi makubwa sana kwa nchi yetu,japo sina uelewo wowote ule wa yeye Rais kuweza kufanya mapinduzi hayo je kwa nguvu yake kama ni Rais wa nchi au kwa kuwa Mwenyekiti ndani ya chama chake au kwa ushirikiano wa Bunge?Kwani tukikubaliana kwa hoja ya mjadala kwamba ushauri wako huo utatekelezwa unadhani kwa kesi kama ya Richmond ambayo Lowassa ametolewa kafara kama mbuzi wa hitima,hao waliomtoa kafara watakuwa tayari kumuona Lowassa anasimamishwa mahakamani?Na tukumbuke tu ilipokuwa kashfa hiyo ya Richmond ikitumika wakati wa kampeni za kinyang'anyiro cha urais kwa kumkata kasi Lowassa na kumweka katika kundi la mafisadi mbona yeye mwenyewe amekuwa mwenye kusikika tu akisema yupo tayari kusimamishwa Mahakamani kujibu shitaka hilo la Richmond,mbona kumekuwa na ukimya kuhusu kupelekwa Lowassa Mahakamani?
Mwalimu Mhango,hoja zote ulizoziweka kisheria zipo wazi aidha kwa Lowassa au kwa Sumaya na hazina mjadala lakini swali ni hili je ni nani ambaye atakaekuwa tayari kumfunga Paka kengele?Na si hilo tu bali na tuliangalie hili la Marais wastaafu kulipwa mishahara(mafao) ambayo ni sawa na 80% ya mshahara wa Rais ambaye aliekuwa madarakani ukiongezea kukidhiwa mahitaji yao yote ya maisha yao ya kila siku kuanzia matibabu,makazi,maji,umemena na watumishi,Hivi huu si aina nyingine ya ufisadi wa hali ya juu Mwalimu Muhango?Wakati wa hivi karibuni zilienea picha kupitia social media picha ambazo zinaonyesha moja ya nyumba binafsi ya JK sina uhakika na ukweli wa picha hizo,lakini endapo kama picha zile ni za kweli hivi uoni kwamba kodi za wananchi zinazohudumia makazi kama yale ni mzigo mkubwa kwa Serikali yetu?Kinachouma zaidi kuona kwamba Marais wastaafu ambao wanaolipwa mafao hayo walipokuwa madarakani hawakuwafanyia chochote kile nchi na wananchi wao zaidi ya kujinufaisha wao wenyewe,familia zao na waramba viatu vyao.Si hilo tu bali ebu na tuwageukie wabunge kwa kujipendelea kwa kujipangia marupurupu(mafao) baada ya kumaliza miaka mitano-sisemi ya kuwahudumia wananchi bungeni- bali ya kukaa bungeni marupurupu ya kujipendelea ya milioni 250 na huduma zingine zote wanazopewa wakiwa wabunge,je Mwalimu Mhango huu nao sio mzigo mkubwa kwa wananchi wanaolipa kodi na hatimae kuwa mzigo mkubwa kwa serikali yetu?
Mwalimu Mhango,kuuvunja mfumo huu mbovu nadhani wananchi wanatakiwa wawe na mwamko wa kutosha kutokana na kubebeshwa mizigo ambayo kwa upande moja au mwingine haiwahusu na hatimae kuwawekea shindikizo wabunge wao kuweza kupambana na ufisadi wa aina hii,kwa mfano wananchi tulikuwa tunajuwa kwamba viongozi wetu ni mafisadi na nchi inafisadiwa lakini hatukuwa tunajua ni kwa level ipi ufisadi wenyewe ulivyofikia au ulivyojizatiti mpaka pale Raisi Magufuli kulihutubia Bunge kwa mara ya kwanza na kutuacha midomo wazi na akili zetu kukataa kama kweli ufisadi wenyewe ulikuwa hivyo!Na baadae kufumuka mengi tu ambayo ya uoza na uvundo ambayo mvumo mbovu ulikuwa unaukambatia hadi hii leo.Na kama si kulindana,kubebana na kupendeleana nadhani wananchi ilikuwa ni haki yao kumuona Rais wa awamu ya nne anasimamishwa mahakamni,lakini hilo haliwezekani na halitowezekana katika mvumo mbovu ambao unaopiganiwa ufumuliwe au uvunjwe.
Anon, najua mfumo wetu ni mbovu. Lazim atokee mtu auvunje na kuufuma upya. Lowassa kama alitolewa kafara au la basi waliohusika wote hata kama atakuwa Kikwete wawajibishe. Hata Mkapa na Mwinyi ukichunguza madudu waliyotenda hawapaswi kuwa wanalipwa fedha ya umma. Walizoiba zinawatosha. Na wanachofanya ni kuendelea kutuibia tu.Nilifurahi kusoma mahali baada ya kuandika makala hii kuwa kuna wasomi wanapendekeza maurupurupu ya wastaafu yapunguzwe.
Hivyo, tusiangalie nani analengwa bali anayepaswa kushughulikiwa bila kuangalia cheo wala mtandao wake.
Post a Comment