Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alikaririwa hivi karibuni akiahidi kulijengea Baraka Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) makao makuu yenye hadhi. Makonda alisema makao makuu hayo yatakuwa jengo la ghorofa tatu lenye thamani ya shilingi 5, 080, 155, 600. hii si pesa kichele. Wapo waliotaka kujua fedha hii Makonda inatoka wapi; na ni nani wako nyuma ya hisani hii ya aina yake katika historia ya taifa. Makonda anatoa jibu akisema “Leo nimefika hapa ikiwa ni mwanzo wa safari mpya ya serikali ya mkoa wa Dar kujenga makao makuu mpya ya kisasa ya ndugu zangu.” Hivyo wasiojua nani atajenga jengo hili wajue; ni utawala wa mkoa wa Dar es Salaam. Je kuna wanaomtuma na kumtumia kwa faida yao? Hili swali wanapaswa wajibu wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam. Sijui kama wamempa kibali cha kujenga makao makuu ya taasisi ya kidini wakati shule nyingi za serikali ni hoi kimajengo ukiachia mbali wafanyakazi wengi wa serikali kutokuwa na nyumba za uhakika. Je nini mantiki ya kufikia kipaumbele hiki na mchakato gani wa kidemokrasia umepitisha mradi huu? Je watanzania watanufaikaje na mradi huu?
Makonda aliongeza “viongozi wangu wa BAKWATA, najua watu wote wana viongozi kama baba ni kiongozi wa familia, watu wana vyama vyao vya siasa wana viongozi, watu wana makampuni yao wana viongozi lakini viongozi hawa wanatofautiana na viongozi wa dini kwa jambo moja, viongozi wa dini wanatuongoza kutupeleka kwa mola alietuumba sote.”
Kuna maswali ambayo Makonda na waliomtuma walipaswa kujiuliza.
Mosi, je makao makuu ya Bakwata ni muhimu kuliko watoto wetu wengi wanaosomea kwenye majengo mabovu au walimu wao wasio na maslahi na mishahara ya kutosha ukiachia mbali kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha na vya kisasa?
Pili, je kweli Bakwata inastahili kupewa kipaumbele hivi? Pamoja na kuwa mpokea zawadi hachagui zawadi ya kupewa, hivi kweli Bakwata ilihitaji hata msaada mchoro kweli? Wapo waliodhani; Makonda alikuwa amekurupuka kutafuta ima umaarufu au kutaka kuwatumia waislamu aonekane anachapa kazi na mtatuzi wa matatizo ya jamii.
Wapo wanaoona kama Makonda ameshauriwa vibaya kwa kuhangaika na kuwajengea watu makao ya kifahari kwa vile hayakukumfurahisha wakati anawaacha wasio na hata mlo mmoja. Wapo wanaohofia Makonda hatafanikiwa katika kupata hicho unachokitafuta. Hali inakuwa ngumu hasa mtumishi wa umma unapojiingiza kwenye mambo ya dini wakati serikali haina na haipaswi kupendelea dini yoyote. Wapo wanaodhani kuwa bilioni tano na ushei ni pesa ambayo si rahisi kuipata. Hata hivyo, inavyoonekana, Makonda anazo fedha. Maana alikaririwa akisema; anataka jengo lake likamilike ndani ya miezi 14. Huyu atakuwa na fedha. Kinachogomba ni alivyoipata na namna anavyotaka kuitumia kwenye nchi yenye matatizo mia kidogo.
Wapo wanaoona kama serikali ina fedha ya hata kujenga makao makuu ya asasi za kiraia wakati makao makuu yanaishinda, basi imekosa kipaumbele. Je serikali itapata faida gani kujiingiza kwenye biashara ya dini au kuchanganya siasa na dini? Sijui inatoa somo gani kwa watanzania wenye shida za msingi kama vile ukosefu wa maji, umeme na huduma nyingine? Je huku si kuwatumia waumini kisiasa jambo ambalo ni hatari huko tuendako? Wakati mwingine mtu anaweza kutaka kufanya jambo jema kwa njia mbaya. Hapa ndipo utata unapoanza. Huwezi kutumia fedha au nafasi ya umma kupigania haki ya kundi moja wakati ukiyaacha mengine.
Je Makonda na wanaomtuma walijua kuwa:
Mosi, Bakwata wana mali zao kama vile majengo na mali za wakfu ambazo zimetumiwa vibaya kiasi cha kuwaweka matatani baadhi ya waislam wakereketwa kama Shehe Ponda Juma Ponda. Heri Makonda angewapa Bakwata wakaguzi wa mahesabu na mali.
Pili, popote anapopata hiyo fedha, anaigawa kama nani wakati kuna matatizo kibao ya maana yanayolikabili taifa? Kama ni ya serikali ni kwa sheria gani au ni yale yale kuwa kuna watu sasa wana uwezo wa kujifanyia lolote bila kujali sheria kwa vile wako karibu na wakubwa zaidi? Je huu mradi umeridhiwa na mkoa; kwa faida gani na utajiri gani?
Tatu, kwanini hiyo pesa isielekezwe kwenye ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, maabara au kuboresha maslahi ya walimu badala ya kuwajengea wetu wenye uwezo na wajibu wa kujijengea makao yao makuu?
Nne, je Makonda na wenzake wanafahamu; serikali wanayoiongoza inaombaomba kwa wafadhili kutunisha bajeti ukiachia mbali michango kwenye madawati?
Tano, Kwanini serikali hata iwe ya mkoa tu ipate fedha ya kujenga makao makuu ya Bakwata wakati vijijini fedha inaenda kiduchu?
Sita, je lisingekuwa jambo la busara kwa fedha hiyo kuelekezwa kwa vijana wengi wanaohenyeshwa na mikopo ya elimu ya juu au zahanati nyingi zisizo na madawa au majengo stahiki? Hakika maswali ni mengi kuliko majibu.
Tumalizie kwa kuuliza maswali. Je Makonda na wenzake wanafahamu kuwa wanachotaka kufanya–pamoja na uzuri wake–kinaweza kutafsiriwa kama hongo au kishawishi kwa wahusika kwa malengo ya kisiasa hata kama si hivyo?
Saba, je Makonda na wenzake wamepata mchango wa wapinzani ambao nao wanaunda serikali ya mkoa wa Dar es Salaam hasa kwa kuzingatia mileage Makonda na wenzake wataipata kisiasa? Maana, wangefanya wao wangeambiwa wanachanganya dini na siasa.
Mwisho, je utajengea wangapi?
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.