Baada ya kugundua kuwa matapeli na wazembe wameanza kumtumia Dokta Kanywaji kama sababu ya kukwama kwao, kimeamua kutoa angalizo miongoni mwa wanakijiwe na wanakaya wote ili waache visingizio cha kuchapa kazi.
Mpemba analianzisha “yakhe kuna anayeweza nikopesha njuluku lau nkalipie pango langu baada ya Makufuli kusababisha nikose njuluku? Hata yule Shaame nlokuwankindai naye anizungusha na kusema eti hana njuluku kwa vile Dokta Kanywaji kazibana sana ati. Twateseka wallahi.”
Mbwamwitu anachomekea “kwani una mdai Dk Kanywaji au ni gea tu ya kupatia njuluku kama ambavyo sasa imeanza kuzoeleka kiasi cha kugeuka fasheni? Jamaa yangu mmoja alikwenda baa akatumbua uchache na vyangu halafu akaenda kumdanganya mshirika wa bedroom wake eti kuna mashushu walimsachi wakihofia anauza bwibwi au anakwapua bidhaa bandarini. Nadhani usawa huu kila mchovu atasema lake.”
“Yakhe wantania au undhamiria? Hivi huoni njuluku zilivyoadimika tokana na Dokta Kanywaji kubana kila idaraaa?” anajitetea Mpemba.
“Sasa nimekupata vizuri. Kumbe unaimba huu wimbo mpya wa taifa ambapo kila anayekwama anasingizia Dokta Kanywaji utadhani amemkata mikono!” anajibu Mbwamwitu.
“Yakhe tuheshimiane ati. Wewe wawezasema eti umenipata wamaaanishani kama siyo matusi ya nguoni?” Mpemba anajibu kwa hasira kidogo.
Kapende anaamua kutia guu, “kweli Dokta Kanywaji kabana lakini tusimbebeshe kila zigo wakati tunapaswa kujilaumu kwa kuzoea vya dezo. Unadhani kila mmoja analalamika kama wewe wakati akina Makondakonda wanapiga njuluku hadi kutaka kuwazawadia Bakuata mjengo wa bei mbaya tena dezo?”
Msomi Mkatatamaa anaamua kuingilia kati “wakati mwingine nakubaliana na walalamikaji tokana na mazoea ya njuluku za magutu na mazabe ila sikubaliani na kila lawama hasa ikizingatiwa kuwa ilifikia mahali kwenye kaya hii wachovu wakaua uthubutu, ubunifu na kila aina ya namna ya kujikomboa kwa kupambana. Walevi wengi walizoea njuluku chafu zitokanazo na ufisadi, rushwa, madawa ya kulevya na utapeli. Nadhani hapa lazima tukubaliane; bila kubadilika tutalaumu na kuchukia sana wakati si majibu wala nyenzo ya kutatua matatizo yetu.”
Mijjinga anakatua mic “usemayo kweli tupu. Wengi walizoea njuluku haramu ya rushwa mihadarati na mazabe mengine. Sasa kimeziba kila mchovu anamlaumu Dokta Kanywaji akidhani itamzuia kuendelea na vimbwanga vyake. Huyu jamaa namkubali sema napingana naye kubana uhuru wa kuandamana, kujieleza na kufanya siasa kwa kisingizio cha kutekeleza mipango yake. Najua ana mipango poa japo lazima afuate sheria. Huwezi kukomboa jamii bubu isiyoruhusiwa kufikiri wala kuhoji. Kwani hii kaya ni ya kifalme? Hata wafalme nao siku hizi wanahojiwa kiasi cha wengine kuanza kufuata demokrasia kama ilivyotokea hivi karibuni kule Jordan.”
Kapende anakula mic “mie namuunga mkono Dokta Kanywaji hasa nikizingatia kuwa wachovu wengi licha ya kuwa wavivu ni walalamishi. Lazima tubane upatikanaji wa njuluku za kupiga ili tuheshimiane. Siku hizi huoni hata hapa kijiweni wajivuni waliozoea kuja kutupa ofa huku wakituhubiri ujinga wametoweka. Unacheza na jamaa nini?”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe anakatua mic “mwenzenu japo nakubaliana na jamaa, naona ni kama amezidisha hasa pale ukiangalia anavyozidi kuruhusu wazito wastaafu kuendelea kulipwa njuluku kibao huku akiwaminya walaji wengine kwenye asasi za umma jambo ambalo linamtia doa. Vinginevyo, kibano alichotoa kinafaa kuungwa mkono kama ataondoa marufuku ya kuzuia wachovu kumkosoa pale anapofanya ndivyo sivyo.”
Kanji anakula mic “hii Nywaji nabada juluku hadi maisa nakuwa ngumu kama Bombei. Hata ile namiliki dukani hapana pata teja sana. Ile naishi bila lipa kodi sasa nabanwa na hizi electronic machines naleta. Maisa sasa iko gumu sana na sida nakuwa kuba sana.”
Mgoshi Machungi aliyekuwa kimya akiangalia anaamua kula mic “tiambiane ukwei jamani. Tangu dokta Kanywaji kubana upatikanaji wa njuuku za dezo kwei timeumia. Juzi niipata msiba Ushoto hadi nikashindwa kwenda kuhami wafiwa kutokana na kutokuwa na naui.”
Mheshimiwa Bwege anakwanyua mic “pamoja na uzuri wa huyu jamaa, lazima tumbane tujue anachopanga kama ni kile tunachotaka na siyo anachotaka yeye. Hapa lazima mimi niseme wazi. Kuna dalili za kaudikteta ambako sitakaunga mkono. Huwezi kuendesha kaya kama kaya yako. Hii ni kaya ya kidemokrasia ambapo haki na mawazo ya wachovu yanapaswa kuheshimiwa. Maana anapotokea yeyote akataka kufanya haki za wachovu kuwa hisani ndipo tunapoanza kujengeana ukuta na kutiliana mikwara ya hapa na pale kiasi cha kutishia mstakabali wa kaya.”
Mzee Maneno anaamua kupoka mic “huyu mtani wangu kweli noma. Hata nimeshindwa kumcheza binti yangu tokana na kutokuwa na njuluku. Hata hivyo, silaumu kwa vile kama hali itatengamaa kila mchovu akaanza kula haki yake badala ya kulana kama wadudu, hali itakuwa swali. Hali ilikuwa mbaya sana. Napendekeza arejeshe maadili ya utumishi wa umma ili kuondoa takataka zote ambazo hajasafisha. Hatuwezi kuwa kaya ya majambazi na mafisadi tukawa salama. Lazima ifikie mahali kila mchovu aeleze alivyochuma huo ukwasi ambao wahalifu wengi wanautumia kutukoga wakati ni haramu tupu.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si tukamuona Dokta Kanywaji akija kunywa kahawa nasi!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.