How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 25 September 2016

Mlevi aja na suluhu kwa hasara zitokanazo na majanga


            Baada ya kutokea tetemeko la ardhi kule kwa akina Nshomile waitu, Mlevi nimeona ni vizuri niwamegee utaalamu na uzoefu wangu ili kuepuka hasara na mateso bila ulazima. Kwanza, nawapa pole wote waliokumbwa na mkasa huu hata kama ni kilevilevi. Mie ni bora kuliko wale wanaotaka kutapeli wenzao kwa kutumia msiba huu. Hilo moja. Pili, nataka nitoe baadhi ya maangalizo kwa wahanga hata wasio wahanga.
            Tatu, kama umebomokewa na ubavu wa mbwa wako au hekalu lako, usitegemee lisirikali kukujengea. Hiyo si kazi ya sirikali. Bahati nzuri rahis ameishafafanua hili kwa uwazi kabisa. Kwa hiyo wale waliokuwa wakiota mchana kuwa sirikali itawajengea mahekalu, waanze kushughulikia tatizo bila kulikuza. Nadhani hii imeleweka.
            Nne, najua hili gumu kidogo si kwa wahanga tu bali kaya nzima. Napendekeza sirikali itunge sheria ya kulazimisha kila mchovu kulipia mali zake kama tutakavyoziainisha hapa chini.  Hapa mlengwa ni sirikali na walengwa kuhakikisha hili linafanyika badala ya kuacha wahusika wapige politiki. Nadhani haya ndiyo masuala wapinzani wanapaswa kushupalia.
            Tano, kama kuna utaratibu wa bima ya mali inayohusisha mijengo, basi, hakikisha kila mwezi unalipia bima ya ubavu wako wa mbwa au hekalu. Kwa wenye mikweche, mashangingi na ngwalangwala au mikangafu wasisahau kulipa bima. Maana, hujui nini litakukuta na lini na wapi na kwa namna gani.
            Sita, napendekeza pia iwepo bima ya mke, mume na watoto ili kitokea mmojawapo akanyotoka roho kama ilivyotokea kwenye tetemeko au ajali nyingine lau familia ipate kifuta machozi. Najua wengi wasiozoea wataona ama hizi na bangi, ulabu au nawanga. Nope, siwangi; huu ndiyo ukweli hata kama ni uchungu. Kul nafsi zalikatu maut yaani kwa kiarabu, kila nafsi itaonja mauti. Kwa wale wenye nyumba ndogo wala wasipoteze njuluku kuzilipia bima; kwani, kisheria, hazipo. Hapa itabidi wahakikishe wanawabana wawakilishi wao kutafuta namna ya kuweka nyumba zao ndogo kwenye utaratibu mzima wa kulipa bima ya maisha na kifo.
            Saba, bima isiishie kwenye nyumba, mikangafu, mbavu za mbwa. Mahekalu na mashangingi. Kwa wale wanaomilki bunduki, mapanga hata tunguli lazima wayalipie bima. Naona yule anasonya kusoma tunguli. Kama bunduki yako ni silaha ya kukulinda, ina tofauti gani na tunguli wakati vyote vinafanya kazi ile ile japo kwa staili tofauti? Kwenye kaya za hovyo zinazosemekana zimeendelea wachovu wanalipia hata tattoo we unashangaa tunguli! Hiyo tuiache watu wasije kuanza kulipia hata makovu. Hata mie ile kitu navuta sijalipia bima kwa vile ni haramuni! Pia wanasiasa wasilipiwe bima kwa vile hawaaminiki. Unaweza kumlipia ukidhani yuko upinzani akaishia kuingia kwingine kama Lyatongolwa na Joni Choyo.
            Nane, shamba lako ilmradi lisiwe la bangi lazima ulilipie bima. Hapa lazima uhakikishe linapimwa na kupata hati. Kwani, bila hati ni sawa na halipo hata lingekuwa kubwa kama Bongo yote.
            Tisa, tokana na kashkash za kuzidi kughushi vyeti vya kitaaluma, sharti wenye vyeti kuanzia vya kuzaliwa, shahada, vitambulisho na nyaraka nyingine muhimu shurti zilipiwe bima hasa usawa huu vihiyo na vilaza vinahaha kupata vyeti ili viendelee kutanua badala ya kutanuliwa na kutumbuliwa.
            Kumi na mwisho, sirikali lazima ihakikishe inakuja na mfumo safi wa ulipaji bima ili kuepuka usumbufu, ucheleweshaji na utapeli yanapotokea maafa kama haya ya tetemeko. Pia tetemeko la utumbuaji lisimezwe na la ardhi. Pia epukeni matapeli akina Rweyependekeza, Rwebukanyia na akina Rweyetapelila.
            Tuonane wiki ijayo inshallah.
Chanzo: Nipashe Jumamosi jana.

No comments: