The Chant of Savant

Monday 12 September 2016

Tanzania ni zaidi ya Ukuta na CCM

Image result for katuni za ukuta na ccm
          Hakuna ubishi; taifa letu liko njia panda; hasa baada ya kujitokeza kile kinachoonekana kama uvunjaji wa katiba na upingaji wake. Kuanzishwa kwa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) ni matokeo ya serikali kupiga marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano na maandamano ambazo ni haki zao kikatiba. Hakuna kumung’unya maneno; kisheria, serikali haina mamlaka ya kuzuia vyama vya siasa kufanya shughuli zake kama zilivyoainishwa kikatiba.
Baada ya katazo hili,  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)–ambacho kilikuwa mwanachama wa Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA) hoja ambayo iliuawa wakati wa uchaguzi–ilikuja na UKUTA. Serikali kwa upande wake, haikutaka kusikia hili wala lile. Hivyo, ilivipiga marufuku. Mgogoro unaoendelea unajulikana kwa kila mmoja mwenye kufuatilia. Hivyo, hatutapoteza muda kuelezea chimbuko lake zaidi. Hata hivyo, kuna haja ya busara kutumika badala ya maguvu na kutunishiana misuli. Tanzania si mali ya wanasiasa bali watanzania. Je kwanini serikali haitaki kuja na maelezo yanayojitosheleza na kufuata sheria kufikia uamuzi wake ambao hadi sasa ni batili kwa vile haina mamlaka ya kufanya hivyo?
          Je kama taifa litaingia kwenye machafuko kutokana na kichwa ngumu ya pande moja au pande zote kama taifa tutapata faida gani? Nadhani misingi ya demokrasia ni pamoja na majadiliano, kukubali kushinda na kushindwa katika kila jambo. Nawapongeza UKUTA kwa kuahirisha maandamano yao. Nadhani hii imefanyika kutoa nafasi kwa serikali ima ifikiri upya au ijadiliane na UKUTA na kufikia muafaka. Katika mgogoro wowote, huwa kuna hatua kadhaa uzopitia. Kuna kipindi cha mihemko (flare-up) kunakofuatia na kipindi cha hasira kuyeyuka (thawing) inayofuatia na  kuanza kuuona na kuukubali ukweli (sobering) ambayo nayo hufuatiwa na kuanza kujitoa kwenye kizingo au kujifungia (getting out of the enclave) na mwisho, kuchukua hatua (addressing the conflict). kwa hatua tuliyopo sasa ni flare up kwa upand wa UKUTA ambalo ni jambo jema. Ili kusonga mbele, upande wa pili yaani serikali inabidi itoke kwenye enclave na kujibu kwa mwitikio chanya ili kumaliza tatizo. Na inapofanya hivyo, isitafute fursa ya kuwazidi kete wapinzani (time buying).
          Kitaalamu, kuna namna tofauti za kuushughulikia m[i]gogoro. Kuna kushindana (competition), kukubali yaishe (compromise), kuacha mambo yajiendee (accommodation), kutunisha misuli (confrontation), kujadiliana (negotiation) na kusuluhisha (mediation). Hapa uhitajika watu mashuhuri hasa kwenye mgogoro kama wa sasa kama vile Kofi Anan na viongozi wengine wa kisiasa wenye ushawishi na uzoefu wa kutatuzi wa migogoro. Wahusika wanaweza kuchagua nini wafuate hapa.
          Sasa nizame kwa ufupi kwenye mgogoro. Je katiba inasemaje kuhusu hiki kinachotaka kulipeleka taifa kwenye maangamizi ya kujitakia; na nani yuko juu ya katiba ukiachia mbali aliye sahihi?
          Majibu anayatoa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe aliyekaririwa hivi karibuni akisema“sisi tunataka nchi iongozwe kwa kufuata sheria na siyo matakwa ya viongozi ambayo yanakinzana na sheria na Katiba ya nchi.” Hoja hii ina mashiko na ndiyo inapaswa kuwa dira ya kuelekea mgogoro huu uliozaa UKUTA. Mbowe anaongeza “tukiamua sote kujifanya wanafiki kusema hewala, nchi haitakuwa salama; itazaa taifa la watu wenye hofu na ndiyo sababu tumeamua kamati kuu kuanzia sasa kufanya kazi kila siku kuisaidia sekretarieti.”
          Mchango mwingine unatoka sehemu ambayo haikutegemewa, jeshi la polisi ambalo msemaji wake Advera Bulimba alikaririwa hivi karibuni akisema “tutawaita na tutazungumza, naomba tujaribu tu kuvuta subira.” Kinachogomba hapa ni ukweli kuwa jeshi la polisi liko mikononi na chini ya serikali. Hivyo, halina sifa wala uzoefu wa kutatua mgogoro kama huu japo mawazo yake ni mazuri. Polisi wameonyesha ukomavu kama hawatabadilika au kutishwa na kufanya tofauti na wanavyosema kama ambavyo imekuwa ikitokea kwenye kuukandamiza upinzani nchini. Je wananchi wa kawaida wamepewa nafasi gani katika kutafuta suluhu? Wakati polisi wakipendekeza kuzungumza waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Lameck Nchemba alikaririwa akitoa vitisho kuwa serikali ya sasa si kibiriti cha njiti bali cha gesi. Hii si lugha ya mtu mwenye kutaka kujadiliana. Je jeshi la polisi na bosi wao tumwamini nani?
Waziri alikuwa akirudia maneno ya bosi wake yaani rais John Magufuli aliyekaririwa mwishoni mwa mwezi Julai akisema “wasinijaribu kwa kulazimisha maandamano siku ya tarehe moja Septemba…atakayethubutu kufanya hivyo, kitakachompata mmmh, hatasahau kamwe. Mimi ni tofauti sana, wasije wakanijaribu.”
Magufuli aliongeza “Kama wewe ni Mbunge wa Jimbo la Hai (kwa sasa Freeman Mbowe), zunguka kwenye jimbo lako hadi uchoke, si unaacha kwako unaenda Shinyanga kushawishi watu waandamane. Mimi sijazuia shughuli za waliochaguliwa kwenye maeneo yao, bali nimekataa mtu kuondoka jimboni kwake na kwenda kufanya fujo mahali pengine.” Je hapa rais aliongea kama nani wakati katiba iko wazi kuwa watanzania wana haki ya kutoa na kupokea mawazo yao, kusema watakacho na kwenda watakako bila kuvunja sheria? Kwanini serikali isijibu hoja zinazofanya wapinzani kuandamana badala ya kutunisha misuli? Kama wapinzani wanadai Tanzania inaongozwa kidikteta, wanaotuhumiwa wanapaswa kuonyesha uongo wa madai haya badala ya kutoa vitisho. Nadhani hapa ndipo hitajio la majadiliano lilipo. Kwanini rais asiwaite wapinzani akataka wathibitishe madai yao huku naye akionyesha uongo wa madai yao na mambo yakaisha kistaarabu na kwa amani? Inapaswa rais Magufuli ajue yeye ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sawa na wenyeviti wa vyama vingine vya kisiasa. Anachowazidi ni urais ambao nao ukiulinganisha na hoja na umoja wa wapinzani, inakuwa ngoma sawa. Hivyo, tunashauri wahusika wajadiliane badala ya kutunishiana misuli; haijengi bali kubomoa. Nafasi haitoshi. Ila kwa ufupi ni kwamba wahusika wote wajue kuwa asiyekubali kushindwa si mshindani; na Tanzania ni zaidi ya CCM na UKUTA na UKAWA.
          Mwisho wa yote, lazima katiba yetu iheshimiwe. Tusijiruhusu au kuruhusu ichezewe au kuvunja. Hili haliwezi kukubalika hata kidogo. Bila mazungumzo, damu itamwagika tokana na ukosefu wa busara na utumiaji vibaya madaraka. Nadhani wajibu wa kwanza kabisa wa rais na serikali yake ni kulinda katiba na siyo kuivunja au kuitumia kwa maslahi binafsi kisiasa. Wenye akili wameelewa. Tanzania ni mali yetu sote kwa sawa bila kujali madaraka ya mtu au kundi lake.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: