The Chant of Savant

Tuesday 20 September 2016

Kijiwe chawalilia wahanga wa tetemeko


           Image result for photos of waathirika wa tetemeko kagera
            Baada ya kupokea kwa mstuko taarifa za kutokea kwa tetemeko huko mkoani Kagera, Kijiwe kilikaa na kutathmini baadhi ya mambo ikiwemo kuomboleza na kutuma salamu za rambirambi ambazo mzee Mzima niliteuliwa kuzifikisha baada ya kukusanya uchache wa mchango.
            Tokana na uzito wa suala lenyewe, Mheshimiwa Bwege ndiye alianzisha mjadala akisema “nadhani kila mmoja amesikia yaliyowasibu wenzetu kule kwa akina Nshomile very Much mulangila Rweyesimamia, Rwabukoba, Rwabuganda na wengine wengi.in fwact it was very very eavy staff.”
            “Hata mimi nilishangaa kusikia kuwa tetemeko limepiga tena Bukoba. Hatukuzoea mitetemeko zaidi ya ili ya kutumbuana majipu na ukiachia mbali yale ya zamani yaliyotokea Kagera zama za kizungumkuti cha ukimwi. Rafiki yangu Rwakatongo alinipiga simu akilalamika kuwa his mansion did not see the right of the day,” anajibu Mijjinga ambaye ndiyo anamkabidhi gazeti Mchunguliaji.
            Kapende anakula mic “hapa lazima nasi tuchangishane lau tuwatumia kidogo cha kuweza kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu. Sijui mnaonaje wenzangu? Maana ukiangalia ukubwa wa janga lenyewe, lazima hapa tupigane jeki tena haraka sana. Leo kwao; kesho hujui ni kwa nani au vipi?”
            Mipawa anakula mic “umetoa wazo jema njomba sema usawa huu wa kugufulishana inakuwa vigumu hasa ikizingatiwa kuwa wazee wa kijiwe si waajiriwa wala mission town. Hata hivyo, mimi nitajitahidi kuchangia chochote kile nitakachoweza kujinyima. Tena nikitoka hapa lazima nende kumuona jirani yangu Kajuamlo nijue anapanga nini na kama ndugu zake wameathirika.”
            Mbwamwitu anauliza “nani atakuwa mweka hazina wa uchache utakaochangishwa?” Kabla ya kuendelea, da Sofia Lion Kanungaembe anamchomekea “uchache wenyewe haujachangishwa unaanza kuulizia mtunza mfuko! Unadhani uchache huu utapigwa nini wakati hapa hatuna mafisadi wala majizi?”
            “Dada huna haja ya kushangaa hasa kwenye kaya ya kuibiana. Hukusikia juzi juzi kuwa idadi ya wanafunzi hewa inazidi kutuna huku hata madawati yaliyochangishwa hivi karibuni mengi hayafikii kiwango tokana na wajanja kupiga njuluku. Unacheza na kaya hii ya Danganyika!” anajibu Kapende.
            “Usawa huu si wa kuaminiana hasa ikizingatiwa kuwa sisi hatutumbuani kama wao waliokula kitu wakatuacha apeche alolo. Hivyo, si vibaya kujua nani mshika fuko hasa ikizingatiwa kuwa dokta Kanywaji amebana kila kitu au vipi,” anachomekea Mkurupukaji.
            Mgoshi Machungi anakula mic “Si vibaya kujua atakayetunza njuuku hasa ikizingatiwa kuwa kwa nijuavyo kaya yetu, mnaweza kumpa mtu asiye mkwei akaamua kwenda kuoea hasa usawa huu wa kubaniana.”
            Msomi Mkatatamaa baada ya kuona mjadala unaamia kwenye njuluku anaamua kuokoa jahazi. Anakula mic “japo kuwachangia wenzetu ni wazo jema, sidhani kama wachovu kama sisi tuna haja ya kujibana na kubanana na kushikiana wakati lisirikali linajisifu linavyokusanya kodi na kuwa na njuluku kibao hata kutaka kuwajengea matajiri wengine makao makuu kama alivyosema hivi karibuni dogo Po Makondakonda. Nadhani huu ndiyo wakati wa sirikali kuonyesha mwelekeo na kuwajali wana kaya wake.”
            Kabla ya kuendelea Mpemba anamchomekea, “yakhe hapa unnena kitu mujarabu wallahi. Unkumbusha. Hatuna haja ya kubanana bali tuiambie sirikali iwajibike kuwaauni watu wake ati. Nijuavo mie ni kwamba kazi ya sirikali ni kushughulikia kadhia kubwa kubwa kama hizi ambazo wana kaya haweza kuzifutu binafsi. Sirikali ishakiri kuwa ina njuluku za kutosha kiasi cha kununua hata ndege mpya kwa npigo.”
            “Hiyo njuluku wanayoringa nayo iko wapi wakati nao wanachangisha na kuwaomba wafadhili wawasaidie kujisaidia kana kwamba hawawezi kujisaidia wenyewe? Nakubaliana na Msomi; mhatuna haja ya kuchangishana wakati sirikali ipo na ina minjuluku kibao. Ninachoweza kusema hapa ni kwamba tuhakikishe njuluku zinazochangishwa ziwafikie walengwa na siyo kuishia kuliwa na mafisadi wenye ulaji tayari,” anajibu Mipawa huku akibwia gahawa yake.
            Msomi anarejea “nashauri sirikali itumie fursa hii kuanza kuwatajirisha wachovu wetu ili wajenge nyumba bora imara na za kudumu zinazoweza kuhimili tetemeko lijalo. Pia napendekeza tuishauri sirikali itumie zile njuluku za kujengea Bakuata zielekezwe Kagera na siyo Kinondo au vipi?”
            Kanji anakula mic “hii tetemeko naleta huzuni kubwa hadi nalia chozi kuba sana mimi. Mimi iko panga kwenda ona Konda kuambia yeye ile juluku nakwisatenga jengea Bakata peleke Bukoba haraka sana.”
            Mzee Maneno anachomekea “hapa Makondakonda lazima achanganyikiwe. Maana kila mmoja anataka kusikia atakakuja na ipi. Wengi watampima hapa kujua anachotaka ni nini kati ya kaya na umaarufu. Maana haiwezekani akajengea Bakuata mjengo wa mabilioni wakati wanakaya maskini tena waliokumbwa na balaa la kimaumbile wanaendelea kulala chini tena kwenye msimu huu unaokuja wa mvua na baridi kali.”
            Kabla ya kumaliza Mijjinga anamchomekea “nimesikia wanene na wakwasi wengi wakitoa michango ila sijawasikia mabilionea kama akina Ni Ziro Kadamage, Jimmy Rugemalaya, Anna Kajuamlo Tiba na wengine wengi wenyeji wa kule au wao kazi yao ni kupiga njuluku na kutumia peke yao?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapatia tapeli mmoja aitwaye Mulokozi akijidai kuchangisha njuluku ya kutuma kwa waathirika wakati tunamjua alivyo tapeli la kutupwa. Wafia poleni sana. Wanaochagia maafa, chunga sana.  Nahisi ardhi ikitetemeka! Kumbe ni pancha!
Chanzo: Tanzania Daima Kesho.

1 comment:

Anonymous said...

Hakuna chenji ma-lock ameondoa ile ulaji yetu hivyo hautna cha kucngia tena