How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 10 September 2016

Walioghushi wafungwe maisha na kutaifishwa


                        Baada ya kuinyaka hivi karibuni kuwa baadhi ya vihiyo vilaza na vigushi wanaanza kujiondoa kwenye ofisi za umma, nimestuka na kupaswa kutoa angalizo kama mtaalamu wa masuala yote ya uhusiano wa binadamu, elimu, jinai na madude mengine yenye majina magumu ambayo yanaweza kukutia kichaa kama si kizunguzungu na kihindihindi kama nitayaorodhesha hapa. Naona yule anatikisa kichwa akidhani ni utani. I am serious; if I jolt down all stuff that I know, you’ll lose your head dear. Hayo tuyaache.
            Tokana na kuchukia rushwa, ukihiyo na wizi wa njuluku za umma, natoa mapendekezo yafuatayo kuhusiana na vihiyo waliojazana kwenye ofisi za umma wakihomola wakati hawana sifa wala uhalali.
Mosi, washitakiwe wote bila kujali wameacha au kuachishwa au kuendelea na kazi. Hawa ni wahalifu kama wahalifu wengine wanaopaswa kuwa lupango na si uraiani wakitukoga na njuluku zao za wizi.
            Pili, kwa wale ambao wameng’ang’ania ulaji wakati wanajijua ni vihiyo watimliwe na kuswekwa ndani wakingoja kiama chao.
            Tatu, watakaokuwa wamejiachisha kazi wakidhani yamekwisha nao wafuatwe huko waliko na kusweka rumande wakati wakingojea pilato awahukumu na kunawa mikono yake. Niliwahi kusikia mlevi fulani akisema eti lisirikali limeamuru wanaojijua walighushi wajiachishe kazi kabla ya kufikishwa kwa pilato. Lisirikali linatoa ushauri huu wa kipuuzi kama nani wakati na lenyewe lilizembea kiasi cha kuajiri vihiyo. Hili nalo ni jipu linalopaswa kutumbuliwa. Kwani ndilo hilo hilo lililoruhusu kaya kuwa kaya hewa ambapo karibu kila kitu ni hewa, mishahara hewa, wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa, wanasiasa hewa, wasomi hewa, bila shaka kuna ndata na ndutu hewa hapa kayani so to speak. Uzuri ni kwamba hakuna walevi hewa. Walevi ni walevi tu; kwa vile wao ni wapigikaji nani anataka awe hewa wakati maisha hewa ya utawala hewa yalishamkamua hewa kiasi cha kubaki hana hili wala lile?
            Nne, wote watakaobainika kuwa vihiyo na vilaza lazima warejeshe mishahara na marupurupu yote waliyofaidi kwa muda wote waliokuwa kwenye ajira wakati hawakupaswa kuajiriwa kwenye nafasi husika.
            Tano, wanyang’anywe mali walizochuma tokana na kutumia vyeti feki
            Sita, wachapwe bakora hadharani ili liwe somo kwa wengine.
            Saba, kuna haya ya kujua mantiki ya vihiyo kuajiriwa. Kama ni kutokana na vimemo vya wanene, na hao wanene wawajibishwe kwani kisheria wanaitwa accomplices au accessories to committing a crime. Hii kaya si ya mama zao. Nao lazima waonje joto ya jiwe. Utakuta wengine ni vihiyo pia wanaotetea vihiyo wenzao kwa kutumia unene wao.
            Nane, hatuwezi kuzeekea na kupofukia darasani hadi tunavaa miwani ili kupata elimu wakati wengine wanaogopa umande na kutanua. Mimi hadi napata PhD zangu nilisota kwelikweli hasa ughaibuni ambako nililazimika kufanya kila aina ya kibarua halali ili kujikimu.
Pia nashauri twende mbele zaidi na kuhoji utendaji wa maafisa wetu hata kama wana shahada orijino. Maana mijitu mingine huenda vyuoni kukariri kama kasuku lakini vikija kwenye utendaji unakuta ziro kabisa. Hivi, hichi kitegemezi alichoteua mkuu hivi karibuni kilichosema eti haki za binadamu ni wendawazi kweli kimeelimika au kukariri tu? Hivi kile kidogo kilichojipiga kifua kuwa kitajenga makao makuu ya dini fulani kweli kimepiga book au ni kukariri na kubebwa bebwa na kujikomba na kujipendekeza kwa wapenda kuabudiwa?
            Tumalizie kwa kuonya kuwa katika zoezi hili kusiwe na aina yoyote ya kujuana, kulindana, kufadhiliana au kuokoana. Walioghushi ni wahalifu wa kawaida wanaopaswa kuishia magerezani hasa ikizingatiwa kuwa kwa ukihiyo na ukilaza wao wamelitia taifa hasara isiyo mithalika.
Mlevi  wa Mpigakaya Phd (Education dynamics).
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: