Akifungua kiwanda cha Salim Bakhresa huko Mkuranga hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli alikaririwa akitoa zawadi ya ardhi kwa Bahkresa. Hili halikubaliki kwani nchi si mali ya Magufuli; ni mali ya watanzania tena wale maskini.Unampaje ardhi bure mfanyabiashara tajiri bure wakati alishatengeneza faida aendelee kutengeneza faida wakati kuna watanzania wengi hawana ardhi na ni maskini?
Haiwezekani kila anayemfurahisha rais lazima amzawadie tena kwa mali ya umma? Bakhresa si ombaomba wala maskini. Leo atatoa zawadi ya ardhi kwa Bakheresa kwa vile kamfurahisha. Kesho atatoa kwa Singasinga huku watanzania wakiendelea kuwa maskini. Japo mimi si mshauri wa uchumi wa rais, wazo lake halina tija kiuchumi. Hiyo ardhi yenye ukubwa wa hekari maelfu aliyomzawadia Bakhersa kwa sababu anazojua lazima inunuliwe na si vinginevyo. Nasema haya kama msomi na mtu mwenye kujua uchumi na mtanzania mwenye uchungu na nchi yangu na mkereketwa wa utawala bora na wa sheria unaozingatia usawa na kanuni za uendeshaji wake. Kwanza, si fikra za biashara kutoa kitu chenye thamani tena mali ya umma maskini bure. Pili, ardhi husika si mali binafsi ya Magufuli. Tatu, ni ubaguzi kwa wawekezaji wengine ambapo wengine wanalipia ardhi wakati wengine wakipewa bure. Rais Magufuli ajitahidi kufanya mambo kutokana na jazba au mihemko itokanayo na matukio.
Nne, rais hana sababu ya kuwabembeleza wafanyabiashara wawe wawekezaji wa ndani au nje. Badala yake ajenge mazingira safi na wezeshi ya uwekezaji. Chema chajiuza na kibaya chajitembeza. Najua Magufuli ni binadamu na si malaika, ana mapungufu sawa na binadamu yoyote. Kwa hili la kugawa ardhi ya umma amekosea; lazima abadilike na kukubali ushauri wa kitaalamu. Na hili si suala la kupenda wala kujiamria. Lazima tujifunze kufuata sheria. Hata kitendo chake cha kuachia sukari ya Bakhresa kinatia shaka. Je kwanini sukari husika ilikamatwa? Je ilikamatwa kwa sababu Magufuli alitaka ikamatwe au kuna sheria na tararibu zilivunjwa? Je rais hapa anatoa mfano gani kwa walio chini yake? Hii maana yake ni kwamba afisa wa ukaguzi mpakani au bandarini na TRA akifurahishwa na mtu aliyefanya mambo kinyume, anaweza kumwachia kwa sababu amemfurahisha. Leo rais atafurahishwa na Bakhresa kiasi cha kumfutia madhambi yake. Je itakuwaje pale rais atakapochukizwa na yeyote na akatumia staili hii ya kufanya mambo? Lazima taifa letu liendeshwe kisheria bila kujali ukubwa wa cheo cha mtu wala ukaribu wake na yeyote.
Ni kweli; Tanzania inahitaji uwekezaji ili kutengeneza ajira na kulipa kodi. Lakini hatujafikia hali ya kujigonga kwa wawekezaji tena matajiri ukiachia mbali kuwa na madudu kama ilivyo kwenye kukamatwa kwa sukari ya Bakhresa.
Siamini kama Magufuli, mtu mwenye shahada ya juu kitaaluma haoni haya. Sitaki nijenge imani kuwa kuna namna kwenye ukuruba na usuhuba huu wa Magufuli na Bakhresa. Kama tutakuwa wakweli, kitendo cha rais kugawa ardhi ya umma kwa mtu binafsi tena tajiri ni cha kwanza katika historia ya taifa letu. Japo hili ni suala tofauti, tabia ya viongozi kufurahishwa na kutoa mali au fedha za umma inaanza kuwa aina mpya ya ufisadi. Rejea kitendo cha mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutoa zawadi ya kujenga makao makuu ya Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) huku akiacha wanafunzi wa mashuleni wakisomea chini ya miti. Ni busara gani hii? Hatuwezi kuendesha nchi na kutumia fedha na raslimali zake kama mali binafsi tukafika tunakotaka kufika. Ardhi si maua wala mvinyo wa kugawa kienyeji kwa vile mhusika ana madaraka na amefurahi. Sijui kama Magufuli alipata ushauri wa kitaalamu hadi akijiridhisha na kufikia uamuzi huu wa ajabu kidogo kiuchumi na kisheria.
Sioni tofauti kati ya wale viongozi wastaafu waliojimilkisha mashamba ya umma na hili la kugawa ardhi kwa mtu binafsi.
Leo sitaki niseme mengi. Ninachoweza kusema ni kwamba nimetoa ushauri huu tokana na utaalamu wa uchumi na sheria na mapenzi makubwa kwa rais Magufuli ambaye naunga mkono harakati na uzalendo wake wa kutaka kuiondoa Tanzania kwenye umaskini. Na hili liko wazi. Katika kitabu changu kilichotoka hivi karibuni cha Africa’s Best and Worst Presidents: How Neocolonialism and Imperialism Maintained Venal Rules in Africa, Magufuli ni rais pekee aliyeko madarakani aliyepata sura nzima kama kiongozi bora pamoja na kuwa mpya madarakani ukiachia mbali Mwl Julius Nyerere, Samora Machel, Kenneth Kaunda, Nelson Mandela na wengine. Tunajitahidi kumsaidia rais wetu ili afanikishe ukombozi vilivyo na si kuishia aibu na lawama. Nimalizie kwa kumfahamisha rais kuwa wafanyabiashara si watu wa kuamini kwa vile lengo lao si huduma wala nini bali faida. Hili anaweza kuliona toka kwa wenzake waliostaafu. Nani amesahau jinsi wafanyabiashara walivyokuwa wakichangamkia kununua picha, leso hata soksi za Mwinyi? Je baada ya kuachia ukanda, yupo anayeweza kununua hata suti yake? Pia angalia NGO za wake zao ambazo zimedoda kwa kukosa wafadhili baada ya kuachia madaraka. Nimalizie kwa kumtaka Magufuli abatilishe nia na uamuzi wake wa kugawa ardhi ya watanzania kwa mtu ambaye ni tajiri wa kutupwa. Anachofanya hakina tofauti na kutoa misamaha ya kodi kwa matajiri huku maskini wakimuliwa kama ilivyokuwa kwenye utawala uliopita ambao umepoteza sura na mvuto kwa watanzania tokana na madudu uliotenda.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili jana.
2 comments:
Duh.......Huko anakoelekea sasa Rais wetu sipo kabisa mahala pake,huko ni kujidhalilisha mbele ya matajiri hata akijivichia hoja ya uwekezaji na kuzalisha ajira na pia hiyo ni aina ya rushwa kwa pande zote mbili kwa Rais alietoa ardhi bure ambayo sio mali yake ni kutoa rushwa kwa Bakheresa.Na Bakharesa nae atajikuta analazimika kuwa mfadhili mkubwa wa CCM katika harakati zote za kisiasa.Na hivyo ndivyo ilivyo inapokesana kamuni ya sheria na utawala bora matokeo yake ni hayo kwa Rais kujipendekeza kwa wenye mapesa.Kama wanavyosema wasemaji kwamba "fedha ni mwana wa haramu popote pale anaingia aidha kwa kuharibu au kutengeneza"Na tunaliona hili hata katika uchaguzi wa Marekani Mr. Trump na mapesa yake amekosa maadili yote ya mwana siasa anaongea atakavyo, analotaka,wakati anao taka na sehemu anayotaka bila kujali au kujiuliza kwamba wasikizaje wake kama wana akili timamu.
Anonymous umenena. Sina la kuongeza zaidi ya kuomba watanzania tupate ujasiri kumkosoa Magufuli asije kulewa madaraka akaishia pabaya kama Mkapa.
Post a Comment