Wengi wa wapenda demokrasia, haki na usawa nchini watakuwa wameshangazwa na
hata kuchukizwa na yaliyojiri hivi karibuni. Ni kuhusiana na sakata la
kughushi; mbali na la uvamizi wa vituo ya Clouds. Hii ni baada ya
kuachishwa kazi kwa aliyekuwa waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo,
Nape Nnauye. Hata hivyo, kosa lake halikuwekwa wazi ukiachia mbali kujengeka
hisia kuwa kadhia hii ilitokana na Nape kuunda tume ya kuchunguza uvamizi wa
vituo tajwa hapo juu. Japo rais hapaswi kuingiliwa kwenye mamlaka yake ya
uteuzi au utenguzi, kuna haja umma kujulishwa hasa, ikizingatiwa mhusika
alikuwa ameshikilia madaraka ya umma. Je kweli kosa la Nape ni kuunda tume
kuwachunguza wateule wasioguswa?
Japo ni haki na mamlaka ya
rais kuteua na kutengua, kuna haja, wadau yaani wananchi, kujulishwa
kinachoendelea jikoni; kuepuka kujengeka dhana ya udikteta, upendeleo na
upatilizaji kwa wenye mawazo tofauti. Umma unapaswa kujulishwa nani wanapaswa
kuguswa na nani hawapaswi kuguswa hata watende makosa makubwa kiasi gani.
Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kuendeshwa kwa haki, kanuni, sheria
na usawa bila kusahau katiba inayotamka wazi kuwa watanzania wote ni sawa na
wana haki sawa.
Mengine yaliyoibuka kwenye
kadhia tajwa ni matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Inakuwaje mtu mmoja, tena
asiye na stahiki kisheria kutumia vyombo hivi kwa maslahi binafsi na katika
mambo binafsi kama ilivyokariri taarifa ya uvamizi wa Clouds? Mbali na hili,
inakuwaje, kama taifa, tunaanza kuminya na kutishia vyombo vya habari ambavyo
viko kikatiba na si kwa mapenzi ya mtu hata awe na mamlaka kiasi gani?
Inakuwaje; wahusika wanashindwa kujua vyombo vya habari ni sauti ya wasio na
sauti au voice of voiceless dhana nyepesi kabisa kujua? Rejea namna rais
alivyokaripia na kutishia vyombo vya habari kuwa kama vinadhani vina uhuru, it
is not to that extent au si kwa kiwango hicho. Haya si maneno ya rais
anayefuata na kulinda katiba wala kuheshimu uhuru wa kiraia.
Katika kutishia na kuonya
vyombo vya habari, rais alisikika akijigamba kuwa yeye ni rais anayejiamini na
ambaye utawala wake hautokani na ushauri, usaidizi wala ushirika wa mtu yeyote.
Kwani alipokwenda kuchukua fomu za kugombea urais, licha ya kutoshauriwa na
yeyote, alikwenda peke yake. Hii ni kweli; japo sijui kama alijipigia kura na
kushinda. Isitoshe, rais wa nchi anapaswa kuwa rais wa wananchi wote bila
kujali tofauti zao. Hili, hakika, ndilo ambalo rais amekuwa akilihubiri; japo
anaonekana kutolitenda. Kwa maneno ya rais, ni kwamba utawala wake ni
wake binafsi. Je inawezekana taasisi kubwa na muhimu katika taifa ikadhibitiwa
na mtu mmoja hata awe mjuaji kiasi gani? Urais kama, taasisi ni mkusanyiko wa
vyombo vingi. Hivyo, unahitaji maelfu ya wananchi ili uweze kufanikisha malengo
uliyokabidhiwa na wananchi. Hata wafalme huwa hawatawali peke yao pamoja na
ufalme kuwa sawa na mali ya familia.
Japo simuonei huruma Nape
kwa yaliyompata hasa ikizingatiwa alichangia kikubwa kuyaunda, nampongeza kwa
kufia ukweli. Socrates (469 B.C. to 399 B.C), mwanafalsafa wa zamani wa
Kigiriki aliyesifika kwa kupenda ukweli aliwahi kunena “do not be angry with
me if I tell you the truth” yaani usinichukie ninapokwambia ukweli. Yesu
naye alisema ‘tuitafute kweli; kwani itatuweka huru.’ Hii maana yake ni kwamba
mtu anayechukia na asiyependa kweli si huru. Anahitaji uhuru hata kama ana
uhuru wa kisiasa. Je hatuhitaji uhuru utokanao na kweli hata kama unawaudhi
wenzetu tena wenye madaraka? Je kadhia inayomkabila mkuu wa Mkoa wa Dar Es
Salaam, Paul Makonda ya kughushi vyeti vya kitaaluma na kuvamia Clouds si
ukweli tunaoutaka kama jamii ili, licha ya kutendeana haki kwa usawa, utuweke
huru? Nani huyu mtumwa asiyependa kujua kweli imuweke huru? Je tunaweza
kushindana na kweli na kuishinda tukawa salama kama jamii na taifa? Leo
tutakwenda na falsafa ya Socrates tokana na mfano bora alioacha wa kuitafuta kweli
hata kwa gharama ya maisha yake kama ilivyomtokea pale aliposhitakiwa kuwa
alikuwa akiwaharibu vijana kwa mafunzo yake. Baada ya kuhukumiwa kunywa sumu
aina ya Hemlock au Conium maculatum, Socrate alisema “yapo
maarifa ya kweli na katika kujua hili hujui kitu.”
Tukirejea kadhia zetu hapo
juu, nani hajui kuwa mengi yaliyojitokeza ni ya kweli? Nani hajui kuwa tumeanza
kujenga taifa la watakatifu wasiokosea, wanaojua kila kitu na taifa la wasio na
haki wala maarifa ukiachia mbali stahiki na haki ya kueleza mawazo yao? Nani
huyu fedhuli anaweza kufunga mawazo? Je inawezekana? Ukijua hili jua hujui na
kama hujui kuwa hujui basi hujui na utajua,
Tumalizie kwa mfano wa
Socrates kuwa tusiogope kusema ukweli kwa kuhofia kufukuzwa, kunyamazishwa au
kutishwa. Ukweli utabaki kuwa ukweli kuwa mambo yanavyokwenda, licha ya kuwa
tofauti na mategemeo yetu, sivyo ndivyo. Uhuru wetu kama wana jamii una thamani
na gharama ambavyo hakuna anayeweza kuvipoka huku nasi tukiangalia. Ama!
Tanzania imefikia hapa!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
5 comments:
Salaam Mwalimu Mhago.
Ikiwa moja ya ufafanuzi wa maana ya demokrasia ni utwala wa watu,utakanao na watu kwa ajili ya watu kama alivyosema rais wa zamani wa Marekani Abraham Lincon,ikiwa wengine wanafanua maana ya demaokrasia ni kuheshimu misingi ya hadhi,heshima,usawa,haki,uadilifu,imani kwa utawala wa wengi na kuzitambua kuziheshimu na kuzilinda haki za wachache bila ya kujali jinsia,rangi ukabila na dini.na kuheshimu uhuru wa kutoa maoni na kujieleza.Ikiwa dunia hii leo imekubaliana na ufafanuzi huu wa maana ya demekrasia linapotekeaa taifa kama letu ambalo linalosema linapigania kujenga demokrasia na linatawaliwa kwa mfumo wa demokrasia ambayo haioani kabisa na ufafanuzi wa maana ya demokrasia yenyewe inayojulikana na inavyostahiki iwe,je ni sifa gani ambayo tutaliitaje taifa hili au ni mfumo gani wa utawala wa taifa hili kama sio taifa linalotawaliwa na mfumo wa kidikiteta?
Inapotokea rais wa taifa hili kusema kwamba yeye anajiamini kama ni rais kwani hao marais waliopita hawakuwa wanajiamini kama ni marais je adhani na kutambua kwamba kwa msemo huo ni kuwatukana na kuwadhalilisha marais waliopita kabla yake?Ikiwa rais aliekuwepo madrakani anasema kwamba utawala wake hautokani na ushauri, usaidizi wala ushirika wa mtu yeyote,Je rais huyu katika nchi zenye demokrasia za kweli atakuwa na sifa gani kama sio ya udikiteta?Ikiwa rais anatawala kwa matamanio yake anavyoona yeye na anavyotaka yeye bila kujali ushauri wa walikuwa nae karibu na hata kufikiria maamuzi yake au misemo yake itapokelewa vipi na wananchi waliomweka madarakani,je raisi kama huyu atakuwa na sifa gani kama sio ya udikiteta?Ikiwa rais aliekuwa madarakani amefanikiwa kuwatia hofu viongozi ambao alie wachagua kushirikiana nae katika utawala na viongozi hao wakaikubali hofu hiyo na ikawatawala na wanaishi nayo ili walinde masilahi y vyeo vyao,je rais huyu atakuwa na sifa gani kama sio sifa ya ukikteta?Ikiwa rais huyu ambaye aliekuwa madarakani ananyangánya haki ya wananchi wake kujieleza na kutoa maoni yao kwa uhuru unaostahiki kwa ajili ya masilahi ya nchi yao,je atakuwa na sifa gani kama sio sifa ya udikiteta?Ikiwa rais huyu amekuwa ni ngo'mbe mtakatifu asieguswa mbele ya mihimili yote mitatu ya dola,je rais huyu atakuwa na sifa gani kama sio sifa ya udikiteta?Ikiwa rais aliekuwepo madarkani anafanya kila njia ya kuhakikisha kwamba hakuna vyama yva upinzani ambavyo vina haki ya kutetekeleza haki yao ya kisiasa katika nchi na kuviona kama vinaleta vurugu nchini,je rahis huyu ana sifa gani kama sio sifa ya udikiteta?
Mwalimu Mhango,nimalizie kwa kusema kwamba ninachokiona mimi kama ni ukweli wa wazi siasa ya nchi yetu wanasiasa na viongozi wa CCM ni watu ambao wanalinda nafasi zao za kazi na kulinda vyeo vyao na hatimae kuwa wanafiki na nafsi zao na wanafiki kwa wananchi wao na tumeuona unafiki huu kwa Nape akimsifu rais wake na kumtii kama mbwa anavyomtii bwana wake.Na kamwe hakutokuwa na ushujaa wa aina yoyote ule ndani ya CCM wa kumweleza ukweli kiongozi wao wa chama kwamba huko anakowapeleka kutasababisha chama chao kupoteza nafasi ya kuitawala nchi.Tunaona katika nchi zilizoendelea kidemokrasia rais wa nchi au chama anavyoambiwa ukweli,kusahihishwa,kupingwa,na hata kutakiwa ajiuzulu pale tu wanapoona muelekeo wake wa kisiasa au tabia zake binafsi anaweza kulizamisha jahazi.Na tunaona pia wananchi wa nchi hizo kutokaa kimya na kutoka barabarani kujielezea hisia zao na maoni yao dhidi ya rais wao katika mfumo wa demokrasia ya kweli,mfano hai wa karibuni ni joto la kisiasa analoishi nalo rais wa Marekani Donald Trump kiasi cha kutabiriwa kwamba nafasi yake ya kurudi madarakani kipindi kijacho ni ndogo sana.Mwalmu Mhango umemuongelea Socrates Filosofia mkubwa kama ni shahidi wa ukweli ambae hakutaka maelewano ya aina yoyote dhidi ya kusimamia ukweli,hakuwa muoga kwa kile alichokiamini japo alikuwa na uwezo wa kuchagua uhamisho au kuwaomba majaj wamsamehe kwa kuwanafiki kukiri kosa lake,lakini kwa ajili ya ukweli na ukweli ni haki daima aliamua kuchagua hukumu ya kifo kwani alijua kifo hicho kitamfanya kuwa shahidi wa ukweli katika historia.Watanzania kama wasipoangalia kwa rais huyu aliopo madrakani anaweza kuwafikisha pabaya zaidi kabla ya kuwafikisha kule alipokuwa akiwaahidi kwamba anataka kuwafikisha katika ardhi inayotoa maziwa na asali!Daima wakati ndio unaoengea na 2020 haupo mbali tunataka kuiona CCM ikivuna mbigili ambazo alizowapandia Magufuli.
Anon.,
Kwanza shukrani kwa mchango wako wa kina. Ni kweli Tanzania sasa ni nchi ya kidikteta kwa vile hakuna mwenye ubavu wa kumkabili rais ukiachia sisi wachambuzi wachache tunaojaribu kuukumbusha umma haki na wajibu wake. Sina shaka unaposema rais wetu ni dikteta. Naweza kusema ni dikteta kweli kweli.
Pili, nashauri watanzania wengine waige mfano wetu kwa kutokubali kuogopeshwa wala kunyamazishwa. Kwani Tanzania ni nchi yetu kwa usawa na hakuna anayeweza kubadili hili.
Tatu, nikushukuru kwa michango yako ya mara kwa mara kwenye blog hii. Naithamini sana na kuisomaa na kujifunza.
Mwalimu Mhango,
Ukweli usiopingika ni kwamba kazi unayoifanya ni kubwa mno na kwa kiasi gani unavyoipenda nchi yako na kwa uzalendo wa hali juu ambao hauna mfano.Na baadhi ya sisi wasomaji wako tunaoifuatilizia kazi zako tunahisi fahari ya kiasi gani kuwa na mwandishi mzalendo kama wewe.Tunajuwa wazi kwamba wapo baadhi ya wengi tu ambao hawapendezewi na ukweli wa wazi,busara za wazi hekima za wazi,nasaha za wazi ambazo hunazitoa daima,na hata kama hawapendezewi lakini wapo ambao wanajua kwamba ni ukweli ambao haupingiki hata kama wanachukia,na wapo wale ambao wanafaidika daima na kuelimika zaidi tukiwemo sisi wasomaji wako.Endelea daima kuyaeleza yale yanayostahiki kuelezwa hata kama kizazi chetu kilichokuwepo kwa wakati wako wakikusoma hawataki kuelewa,hawataki kufahamu hawataki kusikia lakini kizazi kijacho kitafaidia na kuvuna matunda ambayo mbegu zake unazipandikiza kwa wakati wako huu.Na sisi baadhi ya wasomaji wapo tutakuwa daima tunashiriki nawe kutoa michango yetu kwa kadri tunavyoweza.Tatizo kubwa liliopo tu kwa kizazi cha sasa hususa sisi watanzania ni wavivu wa kujisomea na hasa ukizigatia zama hizi za habari za "fast food and take away".Japo wahenga wetu walisema kamba kwenye miti hakuna wajenzi na kwenye wajenzi hakuna miti lakini hupatikana tu wajenzi wachache katika hiyo miti mingi na kujua nini cha kujenga na kama vile inavyopatikana miti michache kwa wajenzi wengi na wakajua nini cha kujenga.Safari yako ni ndefu Mwalimu Mhango na wahenga walisema safari ndefu uanzwa na hatua moja na we hatua hiyo umeshaianza utafika tu pamoja na vikwazo vyote vya njiani.
Anon.
Umenilazimisha kurejea kukushukuru kwa changamoto, msukumo na pongezi ulizonipa. Sitaacha kuandika as long as ninaishi. Sijui kazi nyingine zaidi ya kuandika na kufundisha na kujifunza. Hivyo, nazidi kuimarika kwa kugundua kuwa kumbe mchango wangu si haba. Shukrani sana kwa kuzidi kunipa moyo.
Post a Comment