Sasa ni Dhahiri. Muhimili mmoja wa dola, mahakama, nchini si huru na salama tena. Tokana na hukumu iliyokuwa itolewa hivi karibuni kabla ya serikali, kwa kuogopa aibu na kuweka precedent, kuchomoa kesi yake ni ushahidi tosha na usio na shaka. Hivi karibuni, mahakama kuu Kanda ya Arusha, ilifanya kitu ambacho wengi hawakukitegemea hasa wakati huu ambapo siasa za ubabe na woga zimetawala. Hii ni baada ya kumwachia kwa dhamana mbunge wa Arusha Mjini , Godbless Lema ambaye alikuwa ameshikiliwa kwa miezi minne kinyume cha sheria. Licha ya kitendo hiki kurejesha heshima ya Mahakama, kinatoa onyo kwa serikali kuwa mambo yanaenda yakibadilika ukiachia mbali kuonyesha kuwa bado kuna watanzania wenye udhu ambao wako tayari kwa lolote kutetea hadhi na taaluma zao.
Katika kukalipia kilichotokea, Jaji Amir Manento alikaririwa akisema “…kumekuja mambo ya kisiasa mno, nadhani yule hakimu akasahau ule uhuru wake wa kimahakama kuwa hata akitoa dhamana hataweza kuchukuliwa hatua za kisiasa.” Hili licha ya kuwa onyo, ni ushahidi kuwa bado kuna mahakimu ima wanaotumiwa kwa kujipendekeza, kuhongwa au kutishwa; kukandamiza haki za watanzania.
Kama haitoshi, jaji Salma Magimbi naye hakubaki nyuma. Kwani alikaririwa na vyombo vya habari akisema “nashangaa hakimu aliruhusu vipi mtu asimame wakati wa mwenendo, hivyo nakubaliana na hoja za wajibu rufaa na mahakama ilipaswa kusubiri mpaka mwisho ikague wadhamini na ninakemea mahakama za chini zisimamie madaraka yake kwa sababu isiposimamia madaraka yake vizuri itachezewa na watu hawatapata haki zao.” Hili ni onyo jingine si kwa wanaotumia madaraka yao kuiingilia Mahakama bali hata kwa wale wanaotumika kufanya kazi hii ya aibu na chafu tofauti na taaluma na viapo vyao. Ni aibu kiasi gani kwa taifa linalojinakidi kuwa la kidemokrasia na lenye kufuata utawala bora na wa sheria?
Mbali na majaji, wanasiasa hawakubaki nyuma. Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi alikaririwa akikaripia udhaifu huu wa kuingiliwa mahakama akisema “ili Mahakama iheshimike, haina budi kutoa haki kwa wakati bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote. Mahakama inatakiwa kudumisha nidhamu na kuzingatia maadili ya uhakimu na ujaji.” Nadhani onyo hili ni Dhahiri. Kwa vile Mwinyi ni mwanasiasa na rais mstaafu, wahusika watakuwa wamepata salamu zao hasa ikizingatiwa kuwa anayetoa karipio na onyo hili licha ya kuwa mwenzao, ana uzoefu kuliko wao.
Mwanasiasa mwingine aliyeudhiwa na najisi hii ni Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) aliyekaririwa akisema, “mahakama inatakiwa itetee haki za wanyonge siyo kuibeba serikali, tutafika mahali watu watapoteza imani na vyombo vya sheria na hapo ndipo watakapojitosa kuchukua sheria mkononi.” Na hii si mara ya kwanza kwa Lissu kuudhiwa na uchafu wa uingiliwaji mahakama iwe na serikali au kuwekewa majaji na mahakimu wasio na udhu. Aliwahi kutoa orodha ya majaji mafisadi na vihiyo walioteuliwa na utawala wa hovyo uliopita. Ajabu baadhi ya wathumiwa bado wako kazini wakiendelea kusaidi kuinajisi mahakama. Je hawa wanaongoja nini wakati majina na sura na uchafu wao vinajulikana?
Kimsingi, mahakimu au majaji waliopoteza udhu kiasi cha kujirihusu kutumika kisiasa na kuminya haki za wananchi ukiachia mbali kudhalilisha mahakama wachunguzwe, kuadhibiwa ikiwamo hata kufukuzwa ili kuonyesha namna mahakama isivyovumilia unajisi huu wa utukufu wake.
Niliwahi kuandika chanzo cha mahakama kuingiliwa kwa kutoa mifano michache ya majaji walioteuliwa wakati hawakuwa na sifa za kutumikia katika wadhifa huu. Nilitoa mifano ya majaji ima walioteuliwa kutokana na kujuana, dini, jinsi na hata kutumiwa wakati walikuwa wachafu kama vile wasio na elimu ya kutosha, watoa rushwa na wazembe. Nadhani hawa ndiyo chanzo cha kuingiliwa kwa mahakama hasa ikizingatiwa kuwa majaji au mahakimu kama hawa hawawezi kushikiria maadili wakati waliingia kwenye mfumo bila maadili zaidi ya madili.
Jaji Bernard Luanda aliliona hili. Kwani, alikaririwa hivi karibuni akisema “tunaomba ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikai (AG) muwe makini sana maana mnatufanya wanasheria wote hatuna akili na mnachafua Mahakama.” Kwa vile mahakama inajua watumishi wake wa hovyo na ina uwezo wa kuwawajibisha, inangoja nini? Kama itawaondoa wachafu wote, heshima na imani yake kwa wananchi vitarejea na hivyo kufanya kazi bila ulazima, wasi wasi wala woga wa kumkwaza au kumponza au kumpendelea yoyote.
Tumalizie kuwataka wanasiasa waache kuingilia mhimili mwingine wa dola. Kwani, kufanya hivyo, kunalikwamisha taifa nao wakiwamo. Isitoshe, uonevu utokanao na uingiliaji huu unaweza kusababisha vurugu huko tuendako. Pia tuchukue fursa hii kuwaonya mahakimu na majaji wanaojirahisi kutumika wakao chonjo. Kwani tunawajua; na wakiendelea na mchezo wao mchafu, tutawafichua na kuwaaibisha kabla ya kushinikiza mamlaka husika kuwachukulia hatua zinazostahiki.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
No comments:
Post a Comment