Baada ya kushuhudia
vimbwanga na vibwengo, visa, visasi, mikasa na makosa, kijiwe kimeamua kutia
timu kwenye jiji la Koromije kule kwenye nchi ya Kusadika na Kuburuzika.
Kinakwenda kule kumsaka mbaya wake aitwaye Bushit. Yote hii ni kutaka kuweka
mambo sawa ili kaya iwe sawa iondokane na kubebana, kupatilizana na kuburuzana.
Akiwa amevalia kanzu yake
na kofia ya tarabushi vya bei mbaya, Mgoshi Machungi leo kaja kinomi. Hata
kabla ya kuamkua, Mbwamwitu anamchokoza “Mgoshi unaenda kuongeza jiko nini
mbona leo umetisha hivi?”
Mgoshi anajibu “kama unaye
mwai sina neno. Niko ai kamii. Si minaona niivyouamba. Isitoshe, napendeza na
kuvutia kwa kia kinda na jiko au vipi jamani.si minipigie angau makofi kwa
niivyojikwatua.”
Kama ada, anaamkua
‘asaamaeku jamia.” Tunajibu na anaendelea kula mic “wagoshi, hivi tinasemaje
kuhusi hiki kitatange na kimbembe vinavyoeendee kwenye kaya?”
Mchunguliaji anajibu “yapo
mengi yanaendelea kuanzia sanaa za kuwasaka na kuwanyaka wauza bwimbwi ambazo
hata hivyo zimefunikwa na Bashiiit na Nipe Mapepe aliyetimliwa baada ya kutaka
kuwagusa watakatifu hasa mwana wa pekee wa mfalme. Je unamaanisha lipi kati ya
haya na mengine mengineyo?
“Mgoshi hapo umepiga
kwenyewe. Ni kama uikuwa kwenye akii yangu! Kusema ue ukwei, hii kadhia ya kutishia
vyombo vya umbea na kuindwa kwa Bashiiit vimenikea kiasi cha kuja na wazo kuwa
tihamie huko Koomije tukakoome na kuchunguza ii tijue ukwei. Maana,
inachanganya na kuudhi,” anajibu Mgoshi huku akimpa kikombe muuza kahawa
ammwagie.
Mijjinga ambaye anatokea
karibu na jiji la Koromije anakula mic “unadhani kuwa hata ukienda Koromije
kusaka ukweli utapokelewa na kufanyiwa kazi? Mbona mkuu amesema atakufa na mtu
wake na kumpatiliza yoyote atakayemgusa mwanae mpendwa? Hujitaki nini?
Kamuulize Nipe Mapepe ndiyo ufanye hayo unayotaka kijiwe kifanye.”
Kapende anampoka mic na
kuronga “nadhani wengi hawakumuelewa mkuu; wanamlaumu bila sababu. Kama
nimemwelewa ni kwamba, hataki umbea na mambo ya kwenye mitandao. Anataka
ushahidi wa kisayansi ndipo atumbue au vipi?”
Mipawa anamchomekea Kapende
“nadhani hukumuelewa mkuu. Alichomaanisha ni kwamba wateule wasisemwe wala
kukemea as long as yeye anawapenda na kuwakubali. Hivyo, hata tukienda kule na
kuja na magunia ya ushahidi, tutazodolewa tu hasa ikizingatiwa kuwa mwenye
mapenzi haoni. Mbona kwa Nipe Mapepe hakungoja kuletewa huo ushahidi wa
kisayansi unaodhani ndiyo anaoutaka?”
Kanji anakatua mic “mimi
ungana na veve. Kuu hapana taka hii teule guswa hata kama naua. Kuna kweli gani
hapa natakiwa kama vote nasitaki yeye nasema kweli yote? Kama Kuu iko taka
shahidi scientific kwanini nafukuza Pepe bila soma ripoti yake?”
Msomi anakatua mic
“kimsingi, hapa Mkuu amefanikiwa kuua ndege wengi kwa jiwe moja. Kwanza, ametoa
kauli za kuchanganya hata kuchanganyikiwa ikizingatiwa kuwa alifanya tofauti na
anachohubiri. Pili, alitumia fursa hii kutoa vitisho kwa wote wanaodhani
wanaweza kumkosoa wakati anajua kila kitu. Tatu, amethitibitisha ukweli kuwa
ile sera ya kulindana ya chata lao bado ipo. Nne, amethibitisha kuwa maji yanaanza
kuzidi unga kiasi cha kuchanganya. Tano, amemvua Nipe Mapepe gamba wakati
akimwacha Bashiit mwenye magamba manene kibao ambayo kwa msemo wa mzee wa
Vijsenti yanahitaji shoka na si kalamu. Je atamvua yule ampendaye?”
Kabla ya kuendelea,
Mbwamwitu anadakia “chonde Msomi. Amvue ili iweje?”
Msomi anampuuzia na
kuendelea “japo wazo la kijiwe kuhamia kufanya uchunguzi kule Koromije ni jema,
je ukweli utakaopatikana utakubaliwa au kusulubiwa kama ule wa Nipe Mapepe? Je
kuna masikio ya kuweza kuusikia wakati yaliyopo yameishajazwa vijiti? Nadhani
hapa la kufanya ni ima kuingia mitaani ili kujua hii kaya ni ya nani,
kunyamaza au kwenda kwa pilato kumshitaki mtuhumiwa. Vitendo vilivyotokea
vimenikumbusha shujaa Chris Mtikisa. Angekuwa hai, kesi zingeishajaa mahakamani.”
Mheshimwa Bwege anakula mic
“mie leo sichangii mengi. Ninachoona ni kwamba tunaanza kugeuzana mabwege kwa
ubwege bwege tu wa mabwege wengine. Haiwezekani mhalifu mmoja alindwe kwa
mitutu na mamlaka kaya iwe salama. Tunafanya vitu kana kwamba hatuna ubongo wa
kukumbuka historia za waliopita waliowahi kulewa maulaji kiasi cha kujilisha
pepo wakaishia kuumbuka. Wako wapi wababe kama Saddam Hussein au Mwamali
Kaddafi? Si walipigwa teke na kutokomea wakasahaulika? Hakuna ubwege kama
kukinzana na ukweli na mambo yaliyo wazi. Hivyo, mwende Koromije au msiende,
haisaidii. Majibu yako hapa hapa kama tutaamua kama jamii ya wachovu
wanaochukia na kuchoshwa na ubangaizaji, kubebana na kupatilizana kwa sababu
binafsi.”
Sofia Lion aka Kanungaembe
anakwanyua mic “siungi mkono wazo la kwenda Koromije. Kwanini mnatka kufukua
makaburi ambayo mtashindwa kuyafukia? Kwanini suala hili limepewa uzito kuliko
mambo mengine? Kama mmesahau makaburi kama Escrow, EPA, IptL na sasa Symbiosis
ambayo juzi ilishinda kesi ya kuibia mabilioni kaya, kwanini msijisahaulishe na
hili ili msiumize mioyo yenu? Sioni kama kuna haja ya kuendelea kuwapigia mbuzi
gitaa zaidi ya kuacha wakati ufanye kazi yake. Naungana na Mheshimiwa Bwege.
Tuache ubwege na mambo ya kibwegebwege kwenye mambo ya umma.”
“Du, da Sofi hapa umefunga
nyama na kufumba!”
Kijiwe kikiwa kinapita si
akapite Bashiiit! Kama siyo kuzungukwa na ndata na mitutu mbona tungemfanyia
kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment