Hukumu ya mahakama kuu huko Arusha kwenye shauri la rufaa la mbunge wa Arusha, Godbless Lema imetufungua macho na ni ya kupigiwa mfano na kupongezwa dhidi ya uingiliaji wa mamlaka ya mahakama. Huu ni ushahidi kuwa mihimili yetu sasa inaingiliana kiasi cha kutumika kisiasa kwa faida ya kundi moja dhidi ya jingine. Ni kitendo cha kinyama, uvunjaji katiba na cha kulaaniwa. Rejea karipio la jaji Salma Maghimbi aliyekaririwa akisema “nashangaa hakimu aliruhusu vipi mtu asimame wakati wa mwenendo, hivyo nakubaliana na hoja za wajibu rufaa na mahakama ilipaswa kusubiri mpaka mwisho ikague wadhamini na ninakemea mahakama za chini zisimamie madaraka yake kwa sababu isiposimamia madaraka yake vizuri itachezewa na watu hawatapata haki zao.” Huu ni ushahidi tosha, tena toka mamlaka za juu kisheria, unaoonyesha kuwa mahakama yetu inaingiliwa na kutumika kisiasa.
Ukiachia mbali uingiliwaji wa mahakama, pia kuna matumizi mabaya ya vyombo vya dola kama vile jeshi la polisi ambalo siku za nyuma lilisifika kwa kutumika kuwakandamiza hata kuwaua wapinzani. Rejea mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi mnamo Septemba 2, 2012. Huu si uzushi hata uchochezi. Ni ukweli mtupu. Kwani, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe alikaririwa hivi karibuni akisema “huyu ni mbunge wa watu lazima watu wampokee, ila polisi wanapotumia mamlaka yao na silaha zao kuumiza raia hili halikubaliki, nitamtafuta RPC na RCO kwani wajibu wao katika mkoa huu ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na si kuonea raia.”
Unapomuonea mwakilishi wa wananchi, unawaonea, kuwahujumu na kuwadhalilisha wale anaowawakilisha. Hili halina utata wala halihitaji kuombewa msamaha wala kuzungusha. Kama jamii na nchi ya kidemokrasia, tunapaswa kulaani uvunjaji huu wa katiba ambao kisheria ni uhaini na utovu wa nidhani na matusi dhidi ya dhana nzima ya uongozi bora na wa sheria.
Katika nchi yoyote inayofuata demokrasia ya kweli na misingi ya utawala bora na wa sheria, kukosoana ni haki ya kikatiba. Na isitoshe, ndiyo kazi pekee inayofaya uwepo upinzani. Hatuwezi kuendelea na mfumo unaokandamiza haki za kiraia bado tukajidai tunataka kuleta maendeleo. Nani asiyekosolewa huyu anayejifanya Mungu? Watawala wanakuja na kupita. Lakini taifa na taasisi zake zitakuwapo siku zote. Wako wapi majuha kama akina Blaise Compaore (Burkina Faso), Daniel arap Moi (Kenya) na Yahya Jammeh (Gambia) waliojigeuza katiba wakawatesa watu wao bila kujua kuwa kuna mwisho tena wa aibu? Tanzania ni mali yetu sote kwa usawa. Hakuna mwenye kuweza kutupangia nini cha kufanya bila kufuata utaratibu tuliojiwekea. Kama jamii na taifa, tutasimama na kupinga ujinga na uimla huu watake wasitake.
Nchi huendeshwa kwa misingi na utashi wa katiba bali si misingi na utashi wa mtawala, watawala au chama fulani. Inakuwaje tufikie mahali hapa wakati tuliopata uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita? Hali ni mbaya. Imefikia mahali watu wanatuhumiwa kughushi vyeti vya kitaaluma wananyamaziwa wakati wenzao wakituhumiwa kwa kosa hilo hilo wanafukuzwa kazi? Hivi tuhuma zinazomkabili mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda zingekuwa zinameelekezwa kwa mbunge au kiongozi wa upinzani serikali ingekaa kimya kama inavyoendelea kufanya? Imefikia mahali hata bunge linaingiliwa kiasi cha kutumika kama mhuri wa kubariki mambo ya ajabu kama vile kukamatwa mbunge kwa sababu za kuokoteza halafu linakaa kimya. Hivi Lema angekuwa mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) angesoteshwa rumande kwa miezi minne kinyume cha sheria? Wako wangapi walituhumiwa kupokea rushwa toka kwenye baadhi ya serikali za mitaa na wakaishia kupandishwa vyeo na wengine kuteuliwa wakuu wa mikoa?
Rais John Magufuli amekuwa akisikika akisema kuwa yeye habagui watanzania kutokana na imani zao za kidini wala kisiasa, rangi zao, wala kule wanakotoka. Ajabu ya maajabu, ukandamizaji wa wapinzani na wakosoaji unafanyika chini ya utawala wake kiasi cha kumfanya aonekana anahubiri maji na kunywa mvinyo. Hili nalo haliwezi kunyamaziwa. Lazima watokee watu wenye ujasiri wamkabili rais na kumkosoa wazi wazi kuwa anachofanya ni tofauti na achosema. Pia rais Magufuli amekuwa akisema kuwa ni heri achukiwe kwa kusema ukweli kuliko kupendwa kwa kusema uongo jambo ambalo linapingana na kinachoendelea dhidi ya wakosoaji. Kama tulivyosema hapo juu, Tanzania ni mali yetu sote bila kujali dini, vyama, cheo wala ushawishi. Rais na washauri wake wanapaswa kulijua na kulikubali hili huku wakiweka maneno yao kwenye matendo ili wasionekane wanafiki ambao rais Magufuli anasifika kuwananga tokana na kuwadanganya wananchi.
Tumalizie kwa kumshauri rais Magufuli kuwa kukosoana ni nyenzo muhimu katika maendeleo yoyote ya kweli. Pia ni haki ya kikatiba ya raia katika nchi yoyote inayofuata misingi ya kidemokrasia, uwajibikaji na utawala bora. Hivyo, badala ya kuwachukia na kuwaadhibu wakosoaji, serikali yake inapaswa kupokea michango yao na kuipima na kuifanyia kazi. Kufanya hivi, kutaepusha kuingiliana na kudhalilishana kwa mihimili mitatu ya dola yaani Bunge, Mahakama na Utawala. Huu ndiyo ukweli hata kama unaweza kuwa haupendezi.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
2 comments:
Salamu Mwalimu Mhango,
Kwa makala hii ambayo ni moja ya makala yako inayostahiki kusomwa na kila Mtanzania kuanzia vongozi wa ngazi za juu hadi mwananchi wa kawaida wa barabarani na hasa wanafunzi wa sayansi ya kisiasa bila kujali chama au itikadi.Nimejaribu kuyatafuta ya kuyaandika kwa kuongezea mchango wangu lakini nimejikuta sina cha kuongeza kwani makala yako hii imekusanya,imetosheleza na imefunga KADHIA nzima.Nifungie tu kwa kukupa pongezi kwa kazi kunbwa na njema ya kulitoa taifa letu na wananchi wake kutoka katika kiza kinene na ujinga wa kisiasa na kutuingiza katika nuru,mwongozo,busara na hekima za kisiasa.Ukweli utabaki ni ukweli tu hata kama watakasirika wenye kukasirika na watanuna wenye kununa.
Anon.,
Shukrani kwa pongezi zako. Tunajitahidi kuwapa elimu ya bure ingawa wengi wanatuchukia tokana na upogo wao. Hatuwezi kuendelea na kujenga taifa ambalo wao wanalibomoa kwa kulindana na kugeuza nchi yetu kuwa mali yao binafsi.
Post a Comment