Baada ya wana mama karibu dunia nzima kuendelea kunyonywa na mfumo dume, juzi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake ulimwenguni, mlevi niliteua mke wangu bi mkubwa almaaruf Salama Chinga Domokubwa kuwa mjumbe wa kigwena cha walevi aka Bunge la walevi. Hii ni baada ya kugundua kuwa kumbe walevi wengine huwateua bi wakubwa wa marafiki zao kuwa wanene. Mie sikungoja nistaafu ili atakayechukua kiti changu ameteue bi nkubwa wangu. Kama mzee K M7 pale Ug, nimeamua kumpa bi nkubwa ulaji wakati nikiwa kwenye ulaji.
Tofauti na wale walioteuana na kuzusha gumzo, walevi waliridhika nauteuzi wa bi nkubwa wangu kwa vile wananiamini. Na isitoshe bi nkubwa wangu ni kapuku ambaye hana cha NGO wala kipato cha ustaafu. Tofauti nyingine ni kwamba bi nkubwa wangu amepiga shule hadi akaambiwa no more class go to your husband and cook and do other things for him. Yeye hategemei unene wangu kuteuliwa bali kisomo chake ambacho ni wanawake wachache wanacho kwenye kaya ya walevi. Hii sitafsiri ili wale walioghushi vyeti au kuogopa umande kama siyo kubashite waipate. Hapa lazima mtembee na kamusi. Mbali na hiyo, tokana na mfano uliowekwa hivi karibuni kule kwa Joji Kichaka na Trumpet, si vibaya nikaanza kupiga mahesabu ya nke wangu kugombea hata urais wa walevi.
Walevi ni viumbe poa sana kama ukiwaelewa. Wanachotaka ni wewe kuwaonyesha kuwa u mnyenyekevu na asiyejitia kujua kila jambo. Wao hata ukimteua mbwa wako kuwa mjumbe hawajali ilmradi uwape kanywaji na mapupu pale Uwanja wa hyena au vipi? Wala hawana visa na visasi kama wale wachunaji ninaowasikia wakihanikiza kupambana na wabaya wao wakimsingizia God utadhani wanamtumikia kweli. Hata hivyo, walevi si kama wadanganyika wala wabongolalalanders. Hakuna kitu wasichokubali kama kuwaburuza au kuwatisha. Kwa mfano, ukimweka lupango mwakilishi wao, hawangoji kipaza sauti anchomoe. Watakutokea wenyewe na utamwachia bila kungoja mapilato wenye adabu, heshima na udhu kumchomoa baada ya wewe kuchemsha kama nilivyoshuhudia hivi karibuni. Ukitaka maulaji yao yakushinde jifanye imla. Ukitaka kukosana na walevi wadhulumu au kuwakingia kifua waliowadhulumu au kuvunja sheria zao. Watakutokea na michupa ima wakutie ngeu au utoke mkuku kama mbwa aliyefumwa akiiba nyama kama si paka aliyeiba maziwa. Kama ukifanikiwa kuwaburuza walevi ujue zako zesha. Kwani, watakulia pini hadi msimu mwingine wa uchakachuaji wakupige chini. Pamoja na ulevi wao, walevi wana sifa nyingine. Wana kumbukumbu kama tembo. Unaweza kuwaudhi ukajishaua na kujifanya wewe muungu mlevi kwa wakakushiti. Ila siku ya siku ikifika, utaona visasi vyao.
Turejee kwenye uteuzi wa bi nkubwa wangu. Guess what. Mwaka jana niliteua wajumbe wengine wa dezo. Kwa sheria za kilevi, lazima uteue angalau asilimia ya akina mama kwenye kila uteuzi. Kwenye uteuzi ule nilijitia ubabe na kuteua vidume wengi kuliko akina mama. Acha akina mama waanze kunung’unika. Si walikwenda kwa bi nkubwa ambaye wananchukulia kama shoga yao na kumpa onyo kuwa asipoteua mwanamama kutimiza matakwa ya sheria za walevi asahau ukuu mhula ujao. Kuona hivyo, si nikaamua kumteua bi nkubwa wangu ingawa yeye ni tofauti na hao mashoga zake hasa ikizingatiwa anatoka kwenye ukoo ule ule wa wanene wa walevi kama wale wa kule Idodomya. Baada ya baadhi ya walevi na wavuta bangi kuanza kulalamika kwanini nimemteua bi nkubwa wangu, sikunyamaza zaidi ya kuwapa kanywaji na kesi kuishia hapo. Wengine walizidisha unywanywa. Kuwakata ngebe niliwaambia kuwa bi nkubwa wangu ni bonge ya supu yaani ni msupu au mzuri kwa wale wasiojua Kiswahili cha walevi.
Kimsingi, waliokuwa wakinitia taabu ni akina mama. Kwa vile wanaweza kudanganyana na kuwekana sawa, nilishangaa kuona walivyoridhika na mimi kumteua bi nkubwa wangu utadhani atawawakilisha makapuku waliokuwa wakinibana niteue ili kuleta uwiano wa kijinsia kwa mujibu wa katiba ya walevi. Sasa kwa vile nshamteua bi nkubwa. Next time, nanteua kitegemezi chetu kiitwacho Riziki ili kaya yangu yote iwemo njengoni. Isitoshe kama kitegemezi kitakuwa na mama yake njengoni, wale vishoka wanaosifika kunyemelea vya wenzao wataogopa kwa vile kipo. Hii nayo dili hasa usawa huu ambapo nasumbuliwa na malazi ambayo ni siri kuwaambia walevi hata kama wanayajua. Isitoshe mimi kwa cheo changu kama dingi wa kaya ya walevi si mjumbe wa kigwena chetu. Hivyo, sirahisi kuwapo kule kuhami mali zangu zisiliwe na vishoka, mafisi na vispring chickens vya kirume kama alivyofanyiwa nzee Madiba alipokuwa lupango. Hayo tuyaache. Kwanini tusiagane?
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
No comments:
Post a Comment