How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 25 March 2017

Mlevi kuliambia na kulikolomije taifa

Baada ya kushuhudia namna taifa letu linavyogeuzwa shamba la bibi na matapeli kila aina, nimeamua kuja na kuwapa vipande vyao bila kujali kama watachukia, kukoma au komaa. Acha niwakolomee kana kwamba natojea Kolomije kwa akina Bashite kuja kuwapasha wapashike. Hata hivyo, sitawakolomea kwa uongo, visa na visasi kama wale waliokwisha kujima wakaishia kugwajima na kugwajimkaga kiasi cha kugeueza Kolomije kuwa aina fulani ya dini ambayo siku hizi wsanaihuribiri kila wiki kana kwamba mahubiri yamekwisha. Nitakoromea kikolomije na si kitapeli. Wala sitajificha nyuma ya Bwana wala neno lake kama wale. Nawakolomea kama mlevi mwenyewe asiyechelea wala kuogopa chochote. Kwani, naona matapeli wa ndani na nje waliojificha kwenye majoho wakitaka kutuingiza mkenge mchana kweupe wakifikiri hatuna akili ya kuwastukia na upuuzi wao. Kila anayekuja ni kuliombea taifa. Kwani taifa limekufa na kuishiwa hadi kuombea na matapeli waganganjaa na wasakatonge? Wanyong’onyee na kushindwa. Pamoja na ulevi wangu, nimechoka na mikelele ya wasakatonge hawa wanaolenga kuliibia taifa kwa kujifanya wanalipenda; hivyo kuliomboea. Najua wengi hawana kazi. Basi katafuteni pengine pa kuiba lakini si taifa letu. Nimeona wengine wakitoka Nigeria hata Zambia eti wanakuja kuliombea taifa letu. Kwa upendo gani?  Kama kuombea taifa ni dili basi kaombeeni mataifa yenu. Hatuwahitaji wala maombi yenu uchwara na kitapeli. Wapi Yesu aliombea taifa? Mnapata wapi huu upuuzi wenu wanahizaya nyie?
Tofauti na wao, mimi sitaliombea taifa. Kwanza, taifa langu ni hai. Pili, hata kama ni kuliombea taifa, sitafanya matangazo wala kugeuza sala kuwa sera. Tatu, nitaliambia taifa letu kuwa liondokane na ufisadi, ubangaizaji, ukandamizaji, uombaomba na kuchapa kazi kwa bidii huku walevi wakitendeana haki.
Kila anayekuja kuomba kuomba, nenda mkaombee wazazi wenu waliozaa matapeli tena watu wazima wasio na aibu. Rais mnayelenga kutapeli ashasema “Hapa Kazi Tu”, mmeshikilia kuomba. Kwanini hamtaki kujua kuwa hakuna aishie kwa mkate tu? Tangu lini fisi akawaombea wanakondoo zaidi ya kutamani awararue? Badala ya kuliombea taifa jiombeeni muondokane na dhambi ya utapeli na uganganjaa vinavyowasumbua. Kwani mnadhani walevi hawajui kuwa mnajifanya kuliombea taifa ili muwe karibu na wenye madaraka muwatapeli? Kama kuomba mali, mbona hatukuwasikia mkiwaombea waathirika wa tetemeko Kagera? Kama kuomba mali, kwanini hatujawaona mkiombea mateja na mafisadi au ni wale wale waliolala kitanda kimoja na wezi wa Escrow bila kujali dhamana na vyeo tena vya kiroho walivyopewa? Kama waliopewa vyeo kihalali wamechafuka itakuwa nyinyi mbwa mwitu mnaotaka kuwararua wanakondoo? Mshindwe na kunyong’onyea!
Nichukue fursa hii kumshauri rahis asiwasikilize. Awape vipande na kutoa amri kwa mageshi yetu kuwashughulikia kama alivyoshangaa mijitu michafu iliyojificha nyuma ya majoho eti kwenda Central police station na kwaya na isikatwe mitama. Nampongeza kwa kusema kuwa hata migari yao iwekwe lockup na kuchomolewa mitairi yake. Mnadhani hajui mlivyochuma ukwasi kwa kuwaibia na kuwadhulumu wajinga walioshindwa kutatua matatizo yao kisayansi mkawaaminisha kwenye ushirikina na miujiza wakati ni utapeli mtupu. Kumbaff kabisa!
Kila anayekuja anajiita mtumishi wa Bwana. Mkimuona huyo Bwana mtamjua? Kama mna bwana si mwingine bali utapeli, tamaa na uongo. Hivi kweli kaya yetu inahitaji kuombewa na wanigeria au wazambia? Shame on you all!
Acha niongee na walevi. Jamani, taifa lenu halihitaji kuombewa bali kuambiwa kuwa mambo si mambo. Iko wapi katiba mpya? Kuko wapi kutekeleza sheria kwa haki na usawa? Sijibu. Kawaulize akina Godbless watakwambia namna sheria zinavyopindwa kama alivyosema jaji wa magimbi ukiachia mbali jaji Manentie. Mlevi anawekwa ndani miezi minne kinyume cha sheria hamsemi wala kuwaombea wanaotena kufuru hii kwa vile wana madaraka. Go tell it to the birds na maombi yenu uchwara. Nawaambia walevi tena kwa kinywa kipana. Waambie matapeli wafu wa kiroho wakawaombee wafu wenzao waliolala katika ufisadi na uganganjaa. Tangu lini wafu wakawaombea walio hai? Tangu lini manabii wa uongo wakaombea taifa likapata baraka zaidi ya laana ya kuendelea kuburuzana, kudanganyana, kulindana hata kuchuuzana kama ilivyo? Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi! Hivi kweli nchi ya mzee Mchonga ni ya kuombewa na wenye mizigo ya dhambi? Ama kweli paka akiondoka mapanya hujitawala! Angekuwapo simba mwenyewe mzee Mchonga mngesema mnayosema? Go to hell! Hawa matapeli wa majoho na akina Bashite wanatukwaza.
Kwa vile sijapata kalaji, acha nikitoe nikapige mma tayari kuwaza la kusema wiki ijayo. 
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: