Pamoja na ukweli kuwa mimi ni mlevi, chokambaya tena wa kunuka, wakati mwingine nashangaa kukuta kuna walevi kuliko mimi wawe wa kanywaji au maulaji kwa tajiriba zao. Hivi majuzi nilistuka nusu ya kuacha kanywaji. Baada ya kunyaka uchache niliombomu kigogo fulani anayeogopa nisimlipue akatumbuliwa si niliingia kwenye internet café lau nionekane wa kisasa–si wa kisasi–sukiachia mbali kujitafutia umbea na maarifa lau nipate cha kulonga kwenye kanywaji. Bila kutarajia, si nikatua kwenye wavuti uliosheheni tuhuma za Gwajimmy dhidi ya Poo dogo Maanaconda aka Bashiit akimtuhumu kughushi vyeti vya kitaaluma! Sikujua. Kumbe ulevi na ulaji vikizidi vinaweza kusababisha kichaa na upayukaji. Akitokwa povu, Gwajimmy anamwaga ugali baada ya Mako kumwaga mboga kwa kumtuhumu kuuza bwimbwi. Si anadai eti alighushi vyeti vyake vya sekondari. Kukoleza mambo, anadai anavyo vyeti halisi vya dogo vyenye sifuri ambavyo anasema anavyo japo haelezi alivinyakaje iwapo wanaopata sifuri huwa hawapewi vyeti na kwanini sasa. Baada ya kusikiliza inshu nzima nahoji na kufikiri kuwasaka jamaa hawa niwahoji wavitoe au kutoa utetezi kwa wanaotuhumiwa huku nikitaka wahusika kuchunguzwa na kutumbuliwa. Inaonekana. Jamaa wanajuana vilivyo kiasi cha kuvuana nguo hadharani bila woga wala simile. Ama kweli, kama ni kanywaji, inaonekana wanapiga kale kakali. Maana, unashangaa kwa mlevi aliyesema hawezi kushitaki wala hana kinyongo kuwa na visasi hivi. Je huu si uongo wa wazi?
Mtoa tuhuma anadai chanzo cha ugomvi wa wawili hawa ni uheshimiwa wa jimbo wanamotoka. Anaendelea kusema kuwa hawezi kugombea cheo chochote cha kisiasa hata urahis. Kwani, kufanya hivyo ni kujishusha utadhani kweli. Nani autaki urahis? Mbona mnatumia madhabahu kisiasa kama hamtaki siasa? Hili ni tusi kwa wanene wa kisiasa. Sijui kama mlevi aliyejipachika uchungaji na uaskopo kama kweli ana thamani kuliko hao aliowakandia. Sijui aliongea kwa hasira au ulevi kama siyo ujinga. Sijui. Pamoja na tuhuma hizi kuwahusu wawili hawa, hata kama nafasi zao ni za kujipachika au kuteuliwa, kama jamii, tunapaswa kufikia mahali tukiri: tumehalalisha kughushi iwe ni wa nyaraka za kitaaluma, uraia hata kuzaliwa ukiachia mbali kuruhusu kila tapeli kujipachika cheo anachokata kwa makusudi anayotaka. Hapa lazima tusutane kama walevi wenye mila hii ya kutoogopana wala kuoneana aibu. Hakuna anayesingiziwa na kutumiwa vibaya kama Bwana God. Kila anayekuja anajiita mtumishi wake hata kama vitendo vyake ni vya kishetani. Sijui ni ujinga au kutojali. Tunampokea na kumuacha aendesha shughuli haramu. Haiwezekani walevi kuendelea na mfumo na tabia hii chafu. Kama Kaya, lazima tukemee na kutokomeza jinai hii ya kujipachika madaraka ukiachia mbali kutumika kuwaibia walevi wetu wengi wajinga na waliokata tamaa.
Siku hizi wamezuka kila aina ya wasanii, wazushi na wasakatonge wakijiita maaskopo na wachungaji wakati wachunaji kana kwamba siku za mwisho alizotabiri mwana wa Adamu ndo zinakaribia. Haiwezekani kuendelea na wasanii hawa wanaotumia kila mbinu kuanzia vyombo vya umbea, madhabahu, mitandao na njuluku zenye kutia shaka kututia aibu na hasara. Kaya ya walevi imegeuka ya kishirikina kiasi cha waganganjaa na wa kienyeji kutapakaa kila kona huku wakitoa matangazo yao ya kupotesha kwenye mabango hata kwenye vyombo vya hovyo vya habari. Hatuwezi kuendelea hivi tukawa salama kama Kaya. Imefikia mahali hata matapeli toka Kaya nyingine wamevamia Kaya yetu eti kuhubiri dini. Hivi kweli walevi wanahitaji dini usawa huu? Ukitaka kujua kuwa uhubiri si mali chochote, jipachike cheo uende majuu ukitaka kuhubiri uone watakavyokutoa mkuku. Inakuwaje Bongolalaland inageuzwa shamba la bibi na chaka la matapeli kila aina huku li siri kali likaa kimya kana kwamba halijui madhara ya kadhia hii?
Tukirejea kwa wawili hawa, hali ni mbaya. Vyombo vya nguvu vinapaswa viingilie kuwachunguza na kuwachukulia hatua ukiachia mbali kuwaonya wakati wakichunguzwa waache kusambaza umbea. Kwanini Poo asionyeshe vyeti vyake mambo yakaisha jamani au kuna namna? Tiambiane tafadhali. Kama wana ushahidi waende kuhusikapo badala ya kutuzengua na kutupigia mikelele. Kwa mfano, unajiuliza: Kama jamaa alijua mwenzake anatumia vyeti feki ilhali akijua ni jinai ambayo kisheria, kama mlevi anapaswa kuliripoti kwenye vyombo husika, alingoja nini hadi alipotuhumiwa kujihusisha na bwimbwi? Je madai haya ni uongo unaotokana na chuki binafsi dhidi ya wawili hawa au kutaka kulipiza kisasi au ni ya kweli? Kupata jawabu hapa dawa ni kuwachunguza wote wawili na kutumbua wale watakaokutikana wana hatia wanayotuhumiwa nayo. Kumbe wakati mwingine walevi wazima hovyo isipokuwa mie!
Inakuwaje walevi wengine wakituhumiwa kutumia vyeti kanyabwoya wanatimliwa wakati hawa wanene wanakula pini? Nani mara hii kasahau wale wanene vihiyo waliodai wana PhD wakati ni kanyabwoya tupu? Hakuna aliyenichekesha kama yule meya wa mjiji aliyejiita dokta na wajinga wakapenda kumuita hivyo wakati hakuwa na hata cheti cha form six. Nani amesahau wasfu wake wakati wa msiba wake ulivyomuumbua? Buriani Mr Makalio kwani uliondoka na siri kubwa ya udaktari wa kughushi. Je ni vihiyo wangapi wako hai ima wakitumia vyeti feki au kujipa vyeo feki?
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
No comments:
Post a Comment