The Chant of Savant

Friday 12 October 2018

MKO WAPI MLIOIMBA SHAIRI HILI?

Karudi Baba mmoja, toka safari ya mbali
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali
Wakataka na kauli, iwafae maishani.

Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali
oho naona yachinjwa, kifo kimenikabili,
kama mwataka kauli, semani niseme nini.

Yakawatoka kinywani,maneno yenye adili,
Baba yetu wa thamani,sisi tunataka mali,
Urith tunatamani,mali yetu ya halali,
Sema iko wapi mali, itufae maishani.

Baba aliye kufani, akajibu lile swali,
Nina kufa maskini, baba yenu sina mali,
Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,
Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
Akili yetu nyembamba, haijajua methali,
Kama tunataka mali, tutapataje shambani.

Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,
Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
Haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,
Kama mnataka mali mtayapata shambani.

Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,
Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Fumbu wakatafakari, watoto wale wawili,
Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,
Tangu zile za mibuni, hata zitupazo wali,
Na mvua ikaja chini, wakona na dalili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Shamba wakapalilia, bila kupata ajali.
Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,
Wote wakashangilia, usemi wakakubali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakawanunua ngómbe, majike kwa mafahali,
Wakapata na vikombe, mavazi na baiskeli,
Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,
Walikiweka kibao, wakaandika kauili,
KAMA MNATAKA MALI, MTAYAPATA SHAMBANI.

Chanzo: Ruhuwiko Blog

No comments: