The Chant of Savant

Friday 3 September 2021

Tutahadhari Utitiri wa Dini

Baada ya kupata uhuru wa bendera zaidi ya miaka 60 iliyopita, Bara la Afrika linasifika kwa kuwa na sehemu nyingi za ibada kuliko hata zahanati, shule, visima vya maji na mambo mengine muhimu. Pamoja na kupigania uhuru hata kwa kumwaga damu, wengi wa waafrika, hadi sasa, hawajui hata aliyesababisha ukoloni walioupinga hadi kumwaga damu. Historia fupi inaonyesha kuwa bila wamisionari, ingechukua miaka mingi kwa Ulaya kuitawala Afrika. Kwani, wamisionari walitumwa na mataifa yao kuwapeleleza na kuwapumbaza Waafrika tayari kwa wakoloni kuja na kuanza kuwaibia, kuwatawala na kuwatesa kama ilivyotokea.
Wamisionari walikuja barani Afrika kabla ya wakoloni. Ujio wao ndiyo uliwezesha mataifa koloni ya Ulaya kukutana kwenye mji wa Berlin Ujerumani, mwaka 1884, na kuligawanya bara la Afrika vipande vipande vilivyozaa mataifa dhaifu na ya hovyo tuliyo nayo sasa yakishindwa hata kuungana upya na kupata nguvu. Hili ni suala la wakati mwingine.
Leo nitaongelea dini kama chanzo cha ujinga, ubabaishaji, uvivu, upotezaji muda, unyonyaji na ukoloni mambo leo. Kwa waliowahi kutembelea nchi nyingi za Ulaya na Marekani, watakubaliana nami kuwa hakuna makanisa mengi. Na yaliyopo yanauzwa hata kugeuzwa kasino na mengine yapo yapo tu kama majumba ya makumbusho kwa watalii kuja kutembelea. Je Afrika hali ikoje? Kila siku kunazaliwa kanisa jipya au kujengwa msikiti mpya katikakati ya watu maskini. Tembelea vijiji vingi mikoa ya Pwani utaona namna misikiti ilivyojengwa vizuri wakati ikizungukwa na mabanda ya waumini wa miskiti hiyo. Ndiyo,tunahitaji dini, lakini si kwa kiwango tulicho nacho sasa. Je makanisa mengi na misikiti vimeleta suluhisho gani kwa watu wetu? Waingereza husema too much of anything is poisonous, yaani ukizidisha kitu chochote, kinageuka kuwa sumu.
Ili nisionekane napinga dini, napaswa niseme wazi kuwa sipingi dini bali utitiri wa asasi zake ambazo nyingi ni za upigaji tu. Mfano, mwaka 2018, nchi jirani ya Rwanda ilifunga makanisa na misikiti baada ya kugundua kuwa mji mkuu wa Kigali peke yake ulikuwa na makanisani zaidi ya 700. Katika kurekebisha mfumo mbovu wa uanzishaji wa makanisa na dini hovyo hovyo, serikali ya Rwanda, kwanza ilifunga makanisa yapatayo 6,000 na zaidi ya misikiti 100 nchi nzima (Associate Press, Aprili 4, 2018). AP ilimkariri Charles Murunzi akisema kuwa “baadhi ya wahubiri huchochewa na tamaa kuanzisha makanisa kuwatapeli wafuasi wao” jambo ambalo ni ukweli mtupu.
Hatua ya pili iliyochukuliwa na serikali ya Rwanda ni kutaka itungwe serikali ya kutaka kila anayetakiwa kuanzisha kanisa angalau awe na shahada ya kwanza ya theology kuweza kuwa mtaalamu wa kile anachofanya. Hii inaingia akilini sana. Kwanini madaktari, wanasheria, walimu na watu wengine walazimike kusome taaluma zao ndiyo wafanye kazi lakini si wahubiri wa dini wakati wote wanashughulika na binadamu hao hao? Kimsingi, watu wengi, tena wengi matapeli na wachumia tumbo wamekuwa wakijificha nyuma ya neno la Mungu kuwaibia watu wetu maskini na wale waliokata tamaa katika maisha baada ya kukwama kwenye mambo mbali mbali. Ndiyo maana, kama utafanya uchunguzi kuhusiana na madhehebu yanayoibuka kama uyoga hasa ya wale viongozi wake wanaojipachika vyeo vikubwa vikubwa kama vile uaskofu, utume, unabii na mengine, utakuta ni ujanja unjanja mtupu. Kwa ushahidi zaidi, ndiyo maana utakuta matapeli wengi toka nchi kama Nigeria wametapakaa barani wakawaibia wajinga na waliokata tamaa kwenye nchi mbali mbali. Kuna kipindi wengine walikamatwa na madawa ya kulevya huku wakijiita viongozi wa dini.
Tujiulize swali ambalo wenzetu wa Rwanda nadhani walijiuliza. Je Afrika tuna dhambi nyingi na kubwa au kiwango kikubwa cha ujinga hadi wezi wachache wanatumia mwanya wa dini kuwaibia watu wetu? Ndiyo, watu wetu wanapigwa sana hasa pale unaposikia eti nabii fulani anafanya miujiza wakati miujiza ilikwisha zama za Yesu kwa mujibu wa simulizi za kikristo?
Tukiachana na madhehebu ya kikristo, pia tungetunga sheria ya wale wanaohubiri dini ya kiislam wawe wamesoma kwa kiwango fulani. Hii itasaidia kuepuka kuwa na mashehe wasiojua chochote kwenye uislam kama wengi wanaoendesha mihadhara ambao wengi hutumia biblia tu kutangaza uislam kana kwamba quran haina maelezo ya namna ya kuhubiri uislam. Nasema hili kwa makusudi mazima hasa baada ya kipindi fulani mihadhara kuanza kujenga uhasama baina ya wakristo na waislam kichinichini. Kama taifa, hatuwezi kuendelea na uzembe huu wa kutoweka utaratibu talamizi wa kufanya mambo. Hivi ukikuta kuwa daktari, mwalimu au mwanasheria anayekupa huduma ni feki utajisikiaje na utafanyeje? Wakoloni walipoleta dini Afrika, hawakuwa na haja ya kutaka wanaohubiri wawe na elimu ilmradi walikuwa wazungu na tena walifanikisha lengo na kuwapeleleza na kuwapumbaza Waafrika. Je nani anahitaji watu wa kupumbaza na kuibia wengine usawa huu ambapo bara letu limekwama katika mambo mengi ya msingi?
Tumalizie kwa kuweka wazi kuwa––––kwa sasa––––Afrika, na hasa Tanzania ahitaji dini au neno bali kujikomboa kutoka kwenye ujinga, umaskini, maradhi na madhira mengine ambayo chimbuko lake kubwa ni ukoloni. Badala ya kuruhusu waganganjaa japo si wote wanaohubiri, tuweke utaratibu wa wahusika kusomea. Mfano, ukiangalia madhehebu kama Lutheran na Roman Catholic, husomesha viongozi wao wakaiva kweli kweli. Hata kwenye kusaidia umma kimawazo, viongozi wengi wa madhehebu haya wanasaidia kikubwa ikilinganishwa na hawa wapigaji wa kujipachika ambao kimsingi wanachofanya ni utapeli tu wa kawaida. Lazima tuwatolee uvivu kama walivyofanya wenzetu wa Rwanda ambao, si haba, nchi yao inasonga mbele vilivyo ikilinganishwa nasi. Juzi niliona kwenye mitandao watu wakihoji deni kubwa la Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kiasi cha kamati ya fedha ya Bunge kuhoji (Guardian, Agosti 30, 2021) kuhofia linaweza kufa hata kabla ya kutambaa. Nadhani, tatizo mojawapo ni ubabaishaji. Kwanini Air Rwanda, kwa mfano, izidi kupanuka sisi tuanze kusuasua hata kabla ya kuamka? Kwanini serikali iliamini shirika ambalo haliko serious kwenye biashara? 
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: