The Chant of Savant

Wednesday 2 February 2022

Mheshiwa Rais uwe mkali kuzuia jinai hii ya mauaji

Mheshimiwa Rais, nakusalimia, kama kawaida, kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Najua utajibu hata kama ni kimoyomoyo kwa furaha salamu hii adhimu uliyoianzisha na kuishikilia bila kuchoka kwa maneno na matendo. Pia, hata kwa kuchelewa, nikutakia siku ya kuzaliwa. Niende kwenye mada. Hivi kariubuni kumeripotiwa mauaji ya kila aina nchini kuanzia yale yatokanayo na ajali zinazoweza kuepukika, wivu wa mapenzi, ujambazi, ugomvi juu ya mali, na baina ya wakulima na wafugaji huko Tanga kwa uchache. Japo hii ni sehemu ya maisha ya kila siku ya karibu jamii zote duniani ikiwamo Tanzania, sisi siyo taifa la malaika wala mashetani. Tunajivunia sifa yetu ya kisiwa cha amani. 
        Je kwa wingi wa mauaji haya ya mara kwa mara, bado sisi ni kisiwa cha amani kweli? Je ni kwanini tumeharibikiwa kiasi hiki kiasi cha kufanya yale ambayo hayajawahi kufanyika nchini? Kwanini baadhi ya wenzetu wameanza kuwa wanyama kuliko hata wanyama? Tatizo liko wapi?
        Mhe. Rais, leo nitakuomba uwe mkali kama pilipili kama siyo tindikali. Usiwe na huruma na jinai hii inayotishia kulimega na kuliangamiza taifa letu. Tulizoea kusikia watu wakifanyiana unyama kwenye nchi ambazo kwazo amani ni msamiati adimu. Hivyo basi, kurejesha heshima yetu, lazima ukali, hata ukatili ikibidi kuujibu huu ukatili na unyama ambao hata wanyama hawawezi kuwatendea wenzao.
        Mhe. Rais, leo nitadurusu sababu zifuatazo, kati ya nyingi, ambazo ndizo chimbuko la mauaji haya ya kikatili na kinyama yanayoanza kuzoeleka nchini tokana na yanavyojirudia na kuongezeka. Sitaingia kwenye undani wa visa vya mauaji japo kwa uchache yanajulikana kama vile yale yatokanayo na ujinga na upuuzi. Naomba nidurusu yafuatayo:
        Mosi, ni ushirikina na imani za kijinga na kishenzi. Wengi wa watu wetu wameaminishwa kuwa imani bila hata kazi inaweza kuleta utatuzi wa matitizo yao. Nao bila kufikiri kwa kina wameamini. Hata mamlaka zimewaaminisha hivyo. Imani bila matendo ni bure.  Kuna kipindi tuliaminishwa kuwa Tanzania ilikuwa imekingwa na Ukovi-19 wakati mataifa mengine, kama si yote, yakiteketea. Je kulikuwa na ukweli? Hilo sijibu leo. Tuliona usanii ukiendekezwa kama njia mubadala ya fikra. Viongozi wa kidini, wa feki na wa kweli, walipanda chati wakawa sehemu ya serikali. Matamasha ya kisanii yalitamalaki kuliombea taifa badala ya kuliambia ukweli kuna kuna tatizo.
         Wengi wa watu wetu wamezidiwa kiasi cha kuamini kuwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinaweza kuwapa utajiri. Wengine wameharibikiwa hadi kuwachukia wazee kana kwamba wao hawatazeeka. Mauaji ya vikongwe yanaanza kurudi taratibu. Nitaje kisa cha hivi karibuni ambapo mjinga mmoja anatuhumiwa kumuua mamamkwe wake eti kisa watoto wake wanaugua mara kwa mara.
        Pili, ujinga umechukua nafasi ya maarifa siku hizi. Watu wanataka kuishi maisha wasiyo nayo uwezo. Watu wanataka kuukata wasiohofie kukatwa. Kila mtu anataka kula kuku bila kuwa na kuku wala fedha. Watu wetu wamegeuka malimbukeni wapwakiayo mila za kigeni tena za kipuuzi bila kufikiri. Wanajivunia na kusherehekea ujinga. Wanaghushi vyeti na shahada za juu wakati hawana hata vyeti vya kidato cha nne. Watu wanaabudia ujinga na kuchukia maarifa. Watu wetu wengi ni wajinga sina mfano. Hata baada ya kuja kwa teknolojia ya mawasiliano ya kisasa, kupitia mitandao mbali mbali, wengi huitumia kuangalia mambo ya hovyo badala ya kutafuta maarifa. Ujinga umevamia taifa letu. 
        Nadhani sisi ndiyo taifa pekee ambapo waganga wa kienyeji wanaweza kujiita madaktari na maprofesa wasikaripiwe kuwa waache kujipachika na kudhalilisha vyeo vinavyopatikana kwa kutoa jasho. Ni Tanzania pekee ambapo matapeli wa kawaida wanaweza hata kuaminiwa kuwa wawakilishi wa wananchi. Ni Tanzania pekee ambapo kuna utitiri wa mabaa, nyumba za ngono chapchap na makanisa ya kitapeli kuliko hata Nigeria nchi inayosifika kwa utapeli wa kila aina.
        Sababu ya tatu ni umaskini kulhali iwe ni wa mali au maarifa. Tuna watu wengi maskini ambao hawajui namna ya kujiondoa kwenye umaskini hata pale wanapojua kuwa umaskini wao ni wa kutengenezwa na kundi la watu wachache wenye roho mbaya na tamaa.  Fisadi anayejulikana si tangia jana wala juzi anaweza kuachiwa na mahakama baada ya kuvurugwa ushahidi akaenda kanisani kujifanya mtakatifu wakati ni shetani wa kawaida.  
        Mtu–––tena mjinga na mvivu­­­­–––analala maskini na kuamka tajiri bila kuulizwa namna alivyopata utajiri. Hili huwa nalirudia ili siku moja likupendeze na kukushawishi uanzishe sheria ya maadili.
Sababu ya nne ni tamaa. Japo tamaa ni hulka ya binadamu, sasa inaanza kuzidi hasa pale tunapojenga mfumo unaoruhusu ufisi na ufisadi ambapo kinachoangaliwa ni kupata na siyo namna ya kupata. Hili ni balaa ambalo litatufikisha pabaya tusipoangalia. 
        Inakuwaje, kwa mfano, mtu anachukua mifugo yake kulishia kwenye shamba la mwenzake kama siyo tamaa ya fisi? Jibu ni rahisi. Kama mfumo unaruhusu mwenye nguvu amnyanyase mnyonge, kwanini mchungaji asimdharau na kumhujumu mkulima. Kwa waliokulia chini ya utawala wa awamu ya kwanza, mambo ya wakulima kulishia mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima ni mageni kwetu. Je tumekuwa wa hovyo kiasi cha kushindwa kugawanya watu wetu kulingana na shughuli zao? Wanapata wapi hii jeuri na unyama wasiogope vyombo vya dola kama hakuna uhovyo na uoza sehemu kimfumo hata kijamii?
        Tano, kuna ulegelege kisheria. Sheria zetu zinatumika si kwa ukali unaotakiwa. Mfano, mdogo ni ule wa mafisadi kukamatwa na kuachiwa kwenye mazingira ya kutatanisha. Imefikia mahali eti tunajadiliana na wezi kwa kuwataka warudishe fedha au mali walizotuibia? Seriously? Mbona hawa wanaoiba kuku na mikoba hatujadiliani nao au ni kwa sababu hawatokani na kundi letu?
        Mhe. Rais, tumalizie kwa kukuomba tena. Chonde chonde uwe mkali kweli kweli kurejesha nchi kwenye mstari hasa kuhusiana na mauaji ya kinyama yanayoanza kuzoeleka. Tuzibe mianya inayomotisha au kupofusha watu wetu kutenda unyama iwe ni kwa kutafuta utajiri au kulipiza visasi na mengine kama haya.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: