The Chant of Savant

Wednesday 9 February 2022

Barua kwa Dk Tulia Ackson: Hongera na Pole

Mheshimiwa Daktari Tulia Ackson, Naibu Spika na Spika mtarajiwa,
Nakusalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sema, kazi iendelee.Nakuandikia kwa mara ya kwanza kukupongeza na kukupa pole kwa kuteuliwa kugombea kiti cha Spika wa Bunge kilicho wazi baada ya aliyekuwa akikikalia kulikoroga na kulinywa.  Sina ugomvi na mawazo ya Ndugai.  Nani anataka taifa kopakopa? Je tunakopa kufanya nini? Nadhani Mheshimiwa Rais alitoa majibu ya kina. Je angeweza kutetea msimamo wake dhidi ya chama chake akaendelea kuwa ndanimwe? Naamini unakumbuka yaliyotokea na utajifunza tokana nayo ili usirudie kosa. Sina sababu ya kuyarudia.
         Nakupongeza kutokana na kukubalika kwenye chama chako kilichokupitisha peke yako kugombea kiti husika hata kama kufanya hivyo, kunaonyesha kukosekana kwa demokrasia. Kwanini wewe peke yako tena bila kushindanishwa na wengine? Hilo tuliache. Nakupa pole kutokana na kugombea kiti kilichojaa utata kama siyo uchafu tokana na kilivyotumiwa vibaya na aliyekitema. Nitatoa maelezo. Spika wa zamani Job Ndugai, pamoja na kupitishwa na kuchaguliwa kukalia kiti hicho alipwaya ukimlinganisha na magwiji kama Hayati Adam Sapi Mkwawa Spika wa kwanza Mzalendo, rafiki yangu Pius Msekwa na Hayati Samuel Sitta mzee wa viwango.
            Katika waraka wangu, nitakushauri baadhi ya mambo kadhaa kama ifuatavyo ambayo ni masomo tokana na anguko la Ndugai ambalo lingezuilika kama angekuwa anamudu vyema nafasi husika. Hivyo, nakupa yafuatayo kwa ufupi na haraka. Naomba tulia, kujituliza na kuangalia yafuatayo:
    Mosi, nakushauri ujiepushe na ubabe katika wadhifa wa umma ukiachia mbali kupayuka. Siyo siri. Ndugai alikuwa mbabe na mwenye kujiona asijue cheo ni dhamana. Ni bahati mbaya, pale alipopayuka, wengi walimshambuliwa bila kujua chanzo cha tabia hii hatarishi katika utumishi wa umma. Alizoea kujisemea kila alilotaka kusema bila kujali lini, nini na wapi alisema hilo au hayo. Alizoea kuwa-bully wenzake asijue siku yake itafika kama ilivyofika. Nakumbuka majibizano yake na baadhi ya watanzania waliomkosoa au kukosoa Bunge. Badala ya kutumia busara, alitumia ubabe ‘kumalizana nao’ au tuseme kuwanyamazisha baada ya kuwatisha.
        Pili, alionyesha upendeleo usio na sababu wala faida kwa chama. Mfano, alipowabeba wabunge wa CHADEMA wanaojulikana kama Covid-19 baada ya kutimliwa na chama chao tokana na ukosefu wa nidhamu na kutokuwa na imani nao tena. Je hawa wanamwakilisha nani kupitia chama gani au ni CCM B? Je Bunge, chama na Ndugai walipata nini tokana na ukiukwaji huu wa sheria ambao umesababisha uvujaji wa mabilioni ya shilingi wanazolipwa wabunge hawa waliofurushwa na chama chao?  Kwa wanaojua namna Ndugai alivyohalalisha wabunge haram una kusababisha upotevu wa mabilioni, walishangaa alipopata mshipa wa kupinga kukopa wakati walaji wengi wa fedha za umma ni pamoja na hawa Covid-19? Ama kweli, nyani haoni nonihino lake walisema wahenga.
        Tatu, nakupa pole sana.  Kwani, watanzania watataka kujua hatua utakazochukua kukomesha matumizi haya mabaya ya fedha za umma na madaraka ukiachia mbali kuwa ni ufisadi wa kimadaraka hata kama umefumbiwa macho na wakubwa wetu. Namna utakavyoshughulikia kadhia hii na utakavyoendesha bunge, vitaamua hatima yako. Na ndipo hapo nitakupa hongera au kuendelea kukupa pole na kukukosoa.
        Nne, kwa sasa Bunge letu linahitaji kurejesha hadhi yake ya utukufu. Chini ya magwiji niliwaowataja hapo juu, Bunge kweli lilikuwa tukufu. Chini ya Ndugai, kulianza kujitokeza utukutu kama huu wa kujipayukia badala ya kushauriana na chama na serikali hasa ikizingatia kuwa alikuwa akitoka chama tawala.
        Dk Tulia, najua wewe ni mwanasheria mbobezi mwenye shahada ya juu katika fani. Hata hivyo, kuwa na shahada ya juu na utendaji uliotukuka wa viwango vya juu ni vitu viwili tofauti.  Nasema hivi kwa kujikumbusha viongozi waliokuwa na shahada za juu kama vile marais wa zamani wa Ivory Coast (Laurent Gbagbo), Guinea (Alpha Konde), Senegal (Aboulaye Wade) ambao licha ya kuwa maprofesa tena wengine wa sheria, walishindwa kuongoza nchi zao vilivyo pamoja na usomi wao.
        Tano, nakukumbusha ujikumbushe namna baadhi ya wabunge marafiki wa Ndugai tena wenye mabaka kuliko yeye kama yule askofu wa kujipachia walivyomgeuka na kumtaka aachie ngazi wakijipendekeza kwa Mheshimiwa Rais wakati nao walikuwa wakimpiga madongo kwenye suala la Ukovi-19. Nadhani unawafahamu. Hivyo, uchukue tahadhari dhidi ya vidhabu hawa ambao wako tayari kumtumikia yeyote hata kwa kuwatosa marafiki zao ilmradi tonge liende kinywani.
        Leo ujumbe wangu utakuwa mfupi sana. Nitaandika mengi baada ya wewe kukalia kiti na kukitendea haki au vinginevyo. Kazi inayokungoja ni kubwa kweli kweli. Inahitaji busara, weledi, uvumilivu na unyenyekevu. Nashauri usiwe mbali na gwji Msekwa ambaye uzoefu wake kwenye mhimili huu wa dola umetukuka. Pia, waheshimu walio chini yako. Kwani, wanaweza kukupandisha hata kukushusha kama ambavyo walionyesha wangemfanyia Ndugai kama asingetuma ulaji. Unyenyekevu ni silaha namba moja na kutenda haki ni silaha ya pili. Muhimu, usiwabebe Covid-19 tena kama alivyofanya mtangulizi wako chini ya kisingizio au sababu yoyote viwavyo. Licha ya kuwa hasara kwa taifa, ni mfano mbaya wa matumizi ya madaraka ukiachia mbali ubinafsi na ufisadi kwa wahusika ambao wengi wanajua wanachofanya siyo lakini kwa tamaa ya mishiko wanajifanya hakuna kilichotokea. Naomba Daktari uponye Bunge letu majeraha yaliyosababishwa na mtangulizi wako.
Kila la heri katika wadhifa wako mpya ilmradi uutendee haki mkuu wa mhimili muhimu wa dola.
Chanzo: Raia Mwema.

No comments: