The Chant of Savant

Thursday 21 April 2022

Makonda, Ukitenda Ubaya Upokee Ukikurudia

 

Kwanza, kwa wasomaji, wangu, mtakubaliana nami kuwa siku hizi siandiki kama nilivyozoea. Wengi mmeniandikia barua kuuliza kunani. Naomba mnisamehe sikuwajibu–––si kwa sababu niliwadharau. Hapana, sikutaka kutoboa siri zetu za ndani kama waandishi na wachambuzi wa habari. Siri ya mtungi aijuaye kata. Fumbo mfumbie mjinga, mwelevu ataang’amua. Sitaki niwambie yasiyowahusu wala mambo ya ndani. Hivyo, nikiadimika au kuandika, msishangae. Yana mwisho kama yalivyo na mwanzo.
   Bwana Makonda, nianze kwa kukusalimia na kukupa pole kwa unayopitia na yanayokupata baada ya kujikuta nje ya ulaji. Nimeona kwenye magazeti na mitandaoni ukilalamikia a) kunyang’anywa kiwanja na b) kutishiwa kuuawa. Najua, kwa mujibu wa andiko lako kwenye instagramu ulisema kuna makundi matano yanayotaka kukuangamiza. Je, kwanini hukutaka kwenda polisi kulipoti kama sheria inavyotaka na siyo kuomba? Je ukweli ni upi? Uongo ni upi?  
        Bwana mdogo Makonda, japo mimi si muumini wala mtumiaji wa mitandao, naomba nikupe busara ya bure kama binadamu na mtanzania mwenzangu.Ukitenda ubaya utalaumiwa na ubaya utakurudia. Kwani, hicho ndicho ulichopanda. Na busara inasema kila mtu atavuna alichopanda. Huwezi kupanda mbigiri ukategemea uvune maua. Hii ni busara ya kawaida tu. Usitegemee kujipaka kinyesi uambiwe umejipaka manukato. Ubaya ni ubaya ila si uzuri na uzuri ni uzuri ila siyo ubaya hata kwa hayawani.
        Ukiumiza utaumizwa hata ukimuumiza inzi lazima aliyemuumba akuumize. Dini ya kiislamu inatuasa kuwa hata ukitembea, usionyeshe vikumbo kwani, ima unaweza kuumiza viumbe wa Mwenyezi Mungu visivyo na hatia au kuonyesha ushufaa juu ya ardhi ambayo siku moja itakumeza na kukuhifadhi. Hivyo, huwezi kuumiza watu­­­­, tena wasio na hatia––––tena kwa imani yako ya kikristo wameumbwa kwa mfano wa Mungu­­­­––––ukategemea uonewe huruma. Huwezi kuua ukategemea usiuawe jamani.  Mbona wahenga walisema kuwa aishiye kwa upanga atakufa kwao upanga. Ukifanya ubaya utalaumiwa na ubaya utakurudia utake usitake.
        Najua ulivyokuwa madarakani ulijiona mkubwa usijue mawenge. Hili si kosa lako. Yawezekana ni kosa la wale waliokuamini au uwezo wako wa kuelewa mambo ukiachia mbali kiasi cha busara na utauwa ambayo ulipaswa kuwa navyo ukiachia mbali ujuzi wako wa histori na hofu ya binadamu aliyejaliwa ubinadamu. Hukujua kuwa ukubwa ni wa Mungu tu.  Mkubwa nyangumi na tembo kwa vigezo vya binadamu tukilinganisha na ukubwa wa miili yetu. Bwana Makonda, kama utaweza, naomba ujirelekeze kwenye historia za watu kama Isaac MaliyaMungu, kiraka wa nduli Idi Amin au Bob Astles waliolewa ukubwa uchwara wakafa wakiwa si chochote si lolote. Pia, unaweza kutembelea historia za kiraka wa Adolf Hitler, Hinrich Himmler, Hermann Göring, Joseph Goebbels,Martin Bormann, Wilhelm Keitel, Eric Raeder, Karl Donitz, Albert Speer, Joachim von Ribbentrop, na Walther Funk.
        Bwana Makonda, sipendi nikulaumu. Kwani, wahenga husema: ngoma ya watoto haikeshi. Isitoshe, ukiwa kwenye mabega ya mtu mzima hata mzee, usijione unaona mbali kuliko yeye wakati yeye anaona mbali hata kama amechuchumaa kuliko wewe ukiwe umepanda kwenye mti mkubwa. Maisha–––tumeambwa na wahenga––––ni mtihani. Hatujui yajayo hadi yaje kama ilivyo kwenye sakata lako na wengine kama wewe. Wapo waliopata ukuu wakatukana udogo walikotokea wakaishia kurejea kule. Maji huchemka, lakini hurudia kwenye ubaridi. Kwani, ndiyo asili yake.
        Bwana Makonda, japo unaweza kulalamika––––jambo ambalo ni haki yako––––kuwa unaonewa. Je, kwanini wewe na si wengine? Je unavuna ulichopanda au ni somo kwako na wengine kama wewe? Je ushawahi kujiuliza maswali haya yenye kuudhi na kuumiza lakini yenye busara na masomo makubwa? Aliyeko juu mgojee chini wahenga walisema. Sasa, uko chini baada ya kutoka juu. Unajua kadhia na madhara yake. Je unawashauri nini walio kwenye viatu ulivyowahi kuvivaa?
        Bwana Makonda, najua unastahiki kumilki mali sawa na yeyote. Je ulizipataje mali hizo ambazo, kwa sasa, wapo wanaotaka kukunyang’anya kama ni kweli au nawe hukuwanyang’anya wao au wengine. Je unaweza kutoa maelezo ya namna ulivyochuma mali husika ndani ya muda mfupi na kwa namna gani na vipi? Je ulinyang’anya, uliiba, ulidhulumu au kutumia madaraka yako vibaya? Haya ni maswali azimu na muhimu kujiuliza. Kwani, wahenga walisema: cheo ni dhamana. Ulipopewa madaraka, kirahisi na haraka, ulisahau maisha bila madaraka. Uliwatenza ambao hawakuwa na madaraka vibaya. Sasa hunayo madaraka. Ukitenzwa vibaya, usilaumu bali kukumbuka ulivyotenda na kuwatenza wengine.
        Ulipota ulaji ulisahau njaa na umaskini. Shukuru. Je yangekupata yaliyowapata akina Sabaya? Shukuru Mungu. Hutendwi wala kutenzwa kama ulivyowatenda uliowatenda kwa upofu na upogo mdogo wangu. Wako wapi akina Adolf Hitler, Benito Mussolini, Idi Amin, Joseph Desire Mobutu, Sani Abacha na wengine wengi waliojisahau kana kwamba dunia hii ni makazi ya kudumu kwao wakati ni mapito. Wewe bado ni kijana mdogo, tafuta shule ukajielimishe kuhusu maisha na unyenyekevu halafu uombe msamaha hadharani. Uliegemea mti ukadhani umeegemea mwamba. Sasa, umekatwa. Unaanza kulalamika.
        Bwana Makonda, sitaki niseme mengi hadi nikakufuru. Wahenga walisema. Usiache mbachao kwa msaala upitao. Achana na yaliyopita na ugange yajayo kwa kufanya kitubio na kukubali matokeo. Kwani, malipo ni hapa hapa duniani. Isitoshe, hapa chini ya jua, kila kitu ni ubatili mtupu, ubatili mtupu. Binadamu ana nini na nini hadi ajione bora wakati ni dhaifu kuliko hata mahayawani? Huo ndiyo ushauri wangu bwana mdogo Makonda.
        Bwana Makonda, kama kweli kuna wanaotaka kukunyang’anya mali zako, kama umezipata kihalali au kutishia kukuua, nenda polisi. Watakusaidia. Nadhani, kama kiongozi wa zamani wa serikali, utakuwa unajua sheria inasemaje yanapotokea hayo. Vinginevyo, utachekwa na kuwapa faida wabaya wako. Muhimu, usipande miiba ukategemea kuvuna maua. Ukipanda ubaya utavuna ubaya. Ukiishi kwa panga, utakufa kwalo. Na ukidhulumu, utadhulumiwa.  Malipo ni hapa hapa duniani tena le oleo. Mungu wa sasa ni wa mtandao. Analipa haraka usivyotegemea. Nani alijua kuwa wenye vifua wangemezwa na ardhi waliyokuwa wakiikojolea na kuinyea sawa na watepetevu? Duniani tunapita na madaraka na ukubwa ni sawa na umande kwenye jani. Vitayeyuka haraka tena bila kutegemea.
Chanzo: Raia Mwema J'mosi.
      

No comments: