The Chant of Savant

Wednesday 20 December 2023

Hakuna RIP kwa Fyatu Mfyatuzi Hata Nisipoonekana au Kusomeka

 

Mwenzenu, juzi nilipata taabu. We acha tu. Si baada ya kupotea kwa mwezi mmoja kijiweni. Mwenzenu nilienda kwa sangoma wangu kujitibia. Wacha mafyatu wafyatuke. Walinifyatua sina hamu. Wapo waliofurahi nimefyatuliwa na kurejesha namba. Kwani wataishi milele? Wapo walioiniombea. Hawa nawashukuru. Sijui kama walifyatua hizo dua kwa upendo au kusherehekea kufyatuliwa kwangu na kuufyata hapa duniani. Maana, mafyatu wanaweza kuja msibani kujiliwaza wakisingizia wanawaliwaza wafiliwa. Wengine walinipa maagizo na salamu nimsalimie fyatu jiwe tukionana. Mradi kila mmoja na lake. Hata hivyo, msishangae. Ndiyo mafyatu wanaofyatuliwa kwenye mambo ya muhimu na makubwa wasifyatuke na kufyatua lakini wakafyatukia mambo ya hovyo kama kunitakia mie kifo. Kwani nilikuwa peke yangu kwenye kujitazamia? Kamuulize braza Phil Mipango au Abdi Kinamna na wengine ambao huenda kujitazamia tena kwa njuluku za mafyatu hawa hawa wasenzi na wavivu wa kufikiri kabisa.

            Nikiwa natafakari, namlaumu sana bi mkubwa wangu na yule mkubwa zaidi. Sijainyaka kwanini walificha ugonjwa wangu kwa mafyatu? Fyatu yoyote. Mnene au kapuku anaweza kuugua hata “kukata moto.” Kwani, mie ni nani? Kama majogoo walitetemesha dunia walifyatuliwa na kukata moto, mie nani yarabi?

            Hakuna kitu kilinifyatua kama kuona baadhi ya mafyatu wakiweka picha yangu na kamshumaa na RIP utadhani nilishakata moto! Jamani, sijakata moto. Kuweni na subira. Siku moja nitakata moto. Hata nyinyi na wanene wenu nikiwemo mimi na bosi wangu tutaka moto kama jiwe alivyofanya. Hakuna haja ya kuharakishiana mauti.

            Baada ya kufyatuka kwa stone, wapo wanaodai kuwa lazima aliyeko juu aangalie wa kuteua ima kwa kuzingatia afya yake au ukubalikaji au kiherehere chake ili asijemfunika bosi wake au akawa mzima kuliko yeye. Mafyatu hawa laanifu wazushi kweli. Eti wanadai kuwa kama namba wahedi si mgonjwa, basi nambari bee anaweza kuwa mgonjwa kama mimi. Hatutaki kurudia kilichotokea kwa stone ambapo alikuwa ameishafyatuliwa na ndwele na kumfyatua maza ili akifyatuka afyatue ulaji kama ilivyotokea. Wapo wanaosema kuwa nami ni mgonjwa utadhani wao ni madaktari wangu. Kumbaffuni sana.

Hata hivyo, siyo kosa wala ufyatu vyenu. Ni usiri uliotawala kukosekana kwangu kijiweni. Basi ngoja niwafyatulieni bure. Mwenzenu nilichegama kwa Sangoma kujiangalizia na kujitibia baada ya kujisikia vibaya. Hata hivyo, sikuweza kufyatua taarifa za ugonjwa wangu. Badala yake niliamini wenzangu wangezifyatua kama wasingekuwa waoga wanaojidanganya kuwa unene unamfanya fyatu awe malaika ajiwe asiyeugua wala kukata moto. Kama mashine zinakata moto, mafyatu ni nani?

            Baada ya kugundua kuwa kumbe baada ya kufyatuliwa na ndwele, wenzangu walifyatua rongorongo ili kuwawafyatua na kuwazuga mafyatu wasianze rongorongo japo haikuzuia, inabidi niwafyatue kuwa, baada ya kugundua kuwa kulikuwa na rongorongo, nilikuwa sionekani mwezi mzima kwa sababu nilikuwa ‘nafatyua kazi maalum’ aka kutibiwa. Sijui kwanini mafyatu hawajui kuwa kujiangalizia au kutibiwa ni kazi maalumu ambayo inatumia njuluku zao kibao! Huna haja ya kucheka na kudhani nakufyatua. Kwani, kutibiwa siyo kazi maalumu? Kama siyo mbona mafyatu wananilipia utadhani sipati mshiko mkubwa mwisho wa mwezi?

            Hakuna kilichonistua na kunisikitisha kama kusikia wenzangu eti wanataka kuwafyatua wale mafyatu wa umbea waliofyatua cover yangu. Kwani kazi ya mafyatu wa ‘umbea’ aka bahari sorry khabar kwa kimanga, ni nini kama siyo kufyatua ‘umbea’ bila kujali nani wanamfyatua? Nimemsika bwana Nipe Mapepe Ninaye akiwakamia wale waliovujisha na kufyatua cover yangu kwa sangoma kule majuu. Ni ajabu kidogo. Kwanini fyatu huyu aliyepewa ulaji tokana na jina kubwa la dingi wake asiwafyatue wale wanaochafua maadili, kufyatua njuluku za mafyatu, au wanaowanyima mafyatu wa ‘umbea kwa umbea’ wa kufyatua kwenye vyombo vyao vya ufyatuzi wa khabar ambao ni haki yao na ya mafyatu kikatiba.

            Kama wanataka kuficha, basi hawana haja ya kuwafyatua mafyatu wa ‘umbea’ wanapowafyatua. Waende mjengoni kwa yule bi Kidude asiye na subira wafyatue sharia ya kuzuia mafyatu kuwafyatua mafyatu wanene wanopokumbwa na zali kama mie. Sheria iseme wazi kuwa kufichua cover ya MAwaRA aka Makamu wa Rai..we koma usifyatuke ukafyatuliwa kwa ufyatu wako.

            Hata hivyo, mtusamehe sisi mafyatu wanene. Tuna katabia ka kujihadaa kama mbuni amuonaye adui akaficha bichwa mbawani akidhani na adui ni bwege kama yeye hatamfyatua. Huwa tunataka mjue kuwa hatuugui hadi kifo kituumbuwe. Tunataka muamini tumeumbika kwa mawe tusijue hata mawe yanafyatuliwa na kupotea. Kwa kutaka kulinda ulaji wetu, sisi mafyatu wanene huwa hatutaki kujulikana kama tuna ugogoro iwe kwenye afya zetu hata ndoa. Tunapenda kujidanganya tukidhani na mafyatu ni kama sisi nao watadanganyika kama Wadanganyika kumbe siyo! Nisingependa kilichotokea jiwe alipofyatuka kijirudie kwangu au mwingine.

            Kumbe sijakata moto!
Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: