“Kifo, kifo, kifo hakina huruma”, alijiibia fyatu Remi Ongaka asikje bila kuwepo kifo haki isingetendeka. Juzi mafyatu walipopokea msiba wa Eddie Luwasha aka Richmonduli yero ambaye hakutumia ole kuonyesha kuna kitu siyo, walikuwa na mawazo mchanganyiko. Wapo waliochekea na kufurahia utadhani wao hawafyatuliwa siku moja tena wakiwa makapuku waliosikinishwa. Wapo waliochanganyikiwa kwa unafiki wa waliomtimua uwaziri mkubwa akificha siri zake na pacha wake kuwa alikuwa kiongozi bora. Kweli? Kwanini baadhi ya mafyatu ni wanafiki waliojipachika uwezo wa kuhukumu na kusamehe dhambi wakati wote ni walewale japo si wote? Luwash9a alikuwa fyatu kama wengine alikuwa mazuri na mapungufu yake. Isitoshe, mafyatu wanapata wanene wanaofanana nao. Usitegemee mafyatu mtoe malaika japo wapo wachache wenye matendo na sifa japo wapo kinyume. Luwasha amefyatuka tuachane na kumchunguza kuku! Hii ajabu! Mnaomsifia na kumtukuza ni walewale mlimnyanyanyasa baada ya siri zake kufichuka akikimbia chata na kujiunga na upingaji hadi mlipoingia makubaliano ya kukipa kitegemezi chake ulaji.
Tuuombee aende salama na kuutambua mchango wake kama kiongozi wa juu wa kaya ambaye bila shaka yapo mema na mabaya aliyotenda kama fyatu yoyote wewe na mimi.
Mimi kama rahis wa mafyatu, nitachukua hatua kali dhidi ya wanaoshangilia kufyatuliwa kwa Luwasha na wanaomsifia. Sisi tunashukuru kwa muda aliopewa kufyatua maana miaka 70 si haba wala nchezo. Kweli Luwasha kapigana vita na kuikamlisha safari huku akilinda imani ya chata lake la walaji. Hajaacha vitegemezi vyenye kuvaa nepi wala vinavyolala njaa. Hajaacha mjane kapuku bali anayenuka ukwasi hata kama umepatikana kinamna. Kwa upande wa pili, niliuza mafyatu kwanini walikuwa wanachelekea na kushangilia kufyatuliwa kwa mwenzao. Bila aibu walisema kuwa wanalilia njuluku zao zilizozamishwa na Richmonduli bila kuwasahau akina Kagoda ambao siku hizi wameshika kani wakitesa na kutanua wasijue kuna mwisho. Hata wale habithi wa IPTel kuna siku watafyatuliwa tu kwa kuwafyua mafyatu na kuwadhulumu kimasomaso mbali na kuwaletea adha zisizokwisha. Hivi yule karasinga Habith Setii aliishia wapi au ashachomolewa kwa mlango wa nyuma?
Mafyatu walisema wanakumbuka mateso wanayoendelea kuyapata kwa migao ya umeme iliyosababishwa na madudu kama IPTel na Richmonduli, na mengine manene ya wanene kama haya ya juzi ya akina Riz One. Mmoja alisema bila hata aibu na woga kuwa wanakumbuka namna walivyopigwa changa la machoni kwa kufanyiwa usanii wakati kama alivyosema Luwasha, aliachia ngazi kulinda maslahi yake, chata lake, pacha wake na lisirkal lao. Hivyo, wa ufisi na ufisadi, alikuwa Yeshu wao.
Mafyatu si vichaa wala katili kiasi hicho ikizingatiwa kila jambo huwa mantiki na sababu zake viwe sahihi au vya hovyo kama kushangilia kufyatuliwa kwa mwenzetu. Nilipofoka na kuwatuhumu ukatili, unyama, na ukosefu wa utu, mmoja alijibu hadi nikaishiwa kalaji. Bila aibu na kujali kuwa mimi ni rahis wao alijibu ‘ni wapi Yeshu alimsamehe Yuda?” Swali hili, licha ya kunichanganya, liliniacha hoi. Pamoja na udoktari na uprofesa emeritus wangu, niliona niliweke hapa ugani japo tuliangalia kwa undani na kujifunza kitu kama njia ya kufundishana na kuonyana tusipende njuluku hadi mafyatu wanashangilia kufyatuliwa kwetu. Wiki mbili zilizopita, nilipowafyatua akina Riz One kuhusiana na upigaji wao wa Mirirani nilionya kuwa ngurumbili hana haja ya kuhangaishwa na njuluku hadi anadhulumu au kuwauza wenzake au kulewa madaraka hadi anawatapeli na kuwatesa wenzake kama kile kibashiti na waliokifufua. Siku moja ulikuja siku moja utaondoka. Ni kanuni ya kimaumbile. Ndiyo maana namlilia Luwasha kwa vile alikuwa mwanasiasa mahiri aliyewafia wenzake. Aliweza kuhama chata lililomtengeneza japo baadaye aliramba matapishi yake akarejea kwa sababu zilezile za ulaji.
Kupenda ulaji kupita kiasi ni sawa na uchangu wa aina fulani. Kwani, akili huacha kufikiri na tamaa huchukua nafasi yake. Wakumbuke magwiji waliotesa sana kayani lakini wakafukiwa kwenye pembe nne ambayo haweza kuingia hata ng’ombe tokana na udogo wake. Wako wapi zaidi ya kuwekwa kwenye kaburi la sahau? Wako wapi wapigaji kama David Balalii, Muhdun Ndongala, Guramaali, Bazil Moneymbili, Beno Ndururu, Jose Munguy, Stansie Ben Makuliko na wengi wengi? Je kwa falsafa hii, fyatu ni nani hadi ajivune na kuwahujumu au kuwatesa wenzake? Huwa napenda kutembelea kisa cha fyatu mmoja aitwaye Tunda Lishe. Jamaa alishindiliwa shaba mia kidogo akapona na waliotumika au kuamrisha afanyiwe kitu mbaya wakafyatuliwa na virusi viduchu visivyo na umbo lionekanalo kwa macho wakaacha mamlaka yote waliyotumia kutesa wenzao. Je mafyatu manjifunza nini? Tusamehe na kusahau au tusamehe na kukumbuka? Tusilishane pepo na kudanganyana wakati nyoyo zikinyatuka au tupewa ukweli japo utuweke huru? Je kweli Luwasha alikuwa shujaa au kinyonga kwa waliomjua vizuri? Je alikuwa msafi kama anavyopambwa na waliomchafua au msafi anayeoshwa kwenye umauti na walewale aliotenda nao waliyoyatenda? Je tunapompamba fyatu ambaye yuko uchi na aliyekwishafyatuka, tunamdanganya nani zaidi ya sisi wenyewe?
Mafyatu wataomboleza kwa siku tano kikaya. Je anafanyiwa hivyo kwa kustahiki au kuna nguvu nyuma ya pazia inayosababisha haya kujikosha au nafsi na roho zao kuwasuta? Kwanini mlinghasi hasi akakimbia chata na mkaendelea kumghasi hadi akarudi? Je hiki hakiwezi kuwa chanzo cha mauti yake ikizingatiwa kuwa mlimfanya awe na presha kwa kutishia ulaji wake. Je wanaopenda kuishi maisha ya amani wanajifunza nini katika mashindano haya ya ukwasi mauti na maisha ya usafi hekima na heshima?
Nenda kapumzike Eddie Luwasha mie nimekusamehe. Na nitakuenzi. Kweli kifo hakihongeki!
Chanzo: Mwananchi leo.
No comments:
Post a Comment