The Chant of Savant

Thursday 1 May 2008

Barua kwa Mkapa

MZEE Benjamin Mkapa,

Shikamoo! Pole kwa maisha ya ustaafu, uzee na zigo la kashfa mzee wangu.

Sisi hatujambo japo tumechanganywa na kuchanganyikiwa kutokana na matokeo ya vitu vyako. Lengo la waraka huu ni kutaka kukutia moyo ujitokeze uhesabiwe.

Kauli ya juzi ya waziri mkubwa kuwa watakuchunguza si ya kukalia.

Ni kaa la moto. Najua wenye wivu wa kike walikuwa wakitupia nondo na mawe nawe uliamua kula jiwe. Sasa mambo si mambo.

Wadanganyika wanataka chao hasa ule mgodi wa makaa ya mawe kule Kiwira.

Kuna kipindi wanoko walikushikia bango eti usulubiwe we bibi mkubwa, kitegemezi chako, mkamwana na swahiba yako wa kutisha tisha eti kama tuna ubavu asijue tunazo mbavu mia kidogo.

Kabla ya kusahau, nilikusikia ukingurumia Kisarawe mwaka ule. Wanoko wanadai hukujibu hoja zaidi ya kutoa utetezi mwepesi na kuwasingizia wapinzani kuwa kukuandama wewe ni kuiandama CCM!

Eti hawakukuelewa kwa kuwafanya wote wapinzani. Nadhani wanaotaka ujieleze wanatumiwa na wapinzani. Nikirejea mada, sikujua kuwa uwazi ukweli ni maudhi kwa Waswahili ambao kama ulivyosema wana uvivu wa kufikiri na wivu wa kike.

Nilidhani kuweka mambo hadharani ndiyo kutendeana haki kumbe wapi!

Wakati wakimwandama mjusi sebuleni hawajui kumbe chumba cha kulala mna mamba! Lahaula! Baada ya kukaa na kusukuti nawalaumu wanaokulaumu peke yako, wakati kumbe mlitutumikia wengi!

Ila, hata hivyo, inabidi ujipongeze kunipata kijana mwenye ujasiri ninayetetea wakubwa. Hawa wanapaswa kukuomba msamaha ingawa kufanya hivyo haimaanishi haki zao zisahauliwe.

Kuanzia leo nitahakikisha natenda haki kwa kuwahusisha "wasafi" wenzako.Nimegundua hukuwa na roho mbaya. Nikiangalia vitu vyenu, nagundua kumbe kikulacho ki nguoni mwako!

Sikujua kuwa Jakaya angeamua kukutetea. Eti anajitetea kinamna! Hayo si yangu ni ya wanoko na wambea.

Wapo wanaosema. Wewe ulilaumiwa kwa kumteua waziri mkuu aliyeshutumiwa na Mchungaji kuwa ni mwizi.

Naye alimteua aliyeshutumiwa kuwa mwizi na Mchonga! Bahati panga la daktari Mwakiwembe limeishamnyoa.Kwanza kuna ubaya gani iwapo wote ni watoto wa Mirerani?

Wajanja husema kwa mwizi haibi mwizi na mchawi muachie mtoto. Ila wachawi wengine unamuachia mtoto na anamroga!

Si hilo tu. Wale wote waliosimamia uwekezaji eti wanaitwa vidokozi na makuadi wa wawekezaji! Hivi majuzi wamepukutishwa kama kupe kwenye mgongo wa mbuzi mchovu.

Eti walijitengenezea wakizungukwa na jehanam ya umaskini unaonuka; waliimba ukombozi wakatembeza maangamizi!

Kingine, mke wa mdogo wako amemranda Bi Mkubwa wako. Ameishaanzisha ka mradi kake ka NGO kuukomboa na kuukoma ulaji mgongoni mwa mzee. Pia kwenye ziara za matanuzi ya mumewe habanduki!

Kila siku ni ziara majuu. Kama ukifanya utafiti utagundua kaya hii ndiyo yenye dingi anayeshika rekodi kufanya ziara majuu. Wazungu huita global trotter.

Naomba mzee unisamehe sana. Nimegundua kuwa kuendelea kukuchokonoa ni kutaka kuvuruga kisiwa cha amani.

Leo kuna amani sana. Wanafunzi wa vyuo na elimu ya juu wameacha fujo na uchaguzi wao ulikuwa huru. Hawana na uvivu wa kufikiri.

Sasa tuna wasomi na tunao wa kutosha. Huoni wanavyoshinda vijiweni wakinywa kahawa? Isitoshe wasomi wa siku hizi hawana adabu.

Wanapenda kuwachokonoa wakubwa. Na kama ni kusoma nadhani watoto wenu yaani wako, Kikwekwe, Salimuni Amri, Karumekenge, Makambagosi, Luwasha, Kigodani, Miramba na wengine wanatosha maana wamesoma nje na wanaweza kusimamia mabenki na makampuni kama Richmond kwa uaminifu mkubwa kama wale watoto wa shemeji zako walivyofanya kwa Net Problems.

Pia baadhi ya wasomi wetu wapumbavu. Wanadai pesa nyingi. Hawajui pesa iliishia kwenye mikopo ya mashangingi ya waheshimiwa?

Hawajui si busara kulipia elimu kabla ya magari ya wakubwa? Hawana adabu. Hawajui mambo yamebadilika. Zamani wakati wa kula ilikuwa ni watoto kwanza. Siku hizi huo ushamba nani afanye?

Ni wakubwa kwanza vichanga baadaye.Nimegundua kuwa kumbe kasi mpya ni uwazi na ukweli! Inasema hili na kutenda lile! Hata ulaji ni ule ule.

Wakati wako ponjoro mmoja anayependa kujipendekeza hata kukufuru kudai atasomesha Watanzania chuo kikuu alijishindia bilioni 85 za mashirika ya NSSF na PSPF, akanunua majengo ya sirikali kwa bei ya kutupa na kuyauza tena kwayo kwa bei ya kupaa.

Katika awamu hii ponjoro mwingine naye kachomoka na bilioni 12. Hivi maponjoro waliowaonjesha nini hadi mkawasahau ndugu zenu ndugu yangu?

Una habari safari ya Kanani imeanza kwa kasi mpya na nguvu mpya?

Kitu kingine kabla sijasahau. Je, Fred alilipa ile milioni 50 aliyoponyoa NPF au nacho ni kiinua kifua? Mtahadharishe aweke mambo vizuri maana hana kinga kama bi mkubwa wako.

Hayo tuyaache. Kweli mzee ulisema ukweli. Waswahili ni wavivu mno kwa kufikiri. Leo wakati watoto wao wakihangaishwa kuhusu mikopo, wazito wanazidi kufichuliana maulaji ya mabilioni! Wao wanashikilia kelele badala ya kufanya kweli?

Kwanza nani aliyewaroga wazazi wao wakawa maskini badala ya kuchangamkia ulaji? Hawajui mtaji wa maskini ni nguvu yake!

Wasingekuwa wavivu wangepitisha azimio la shinikizo kwa serikali kuitaka ima itimize wajibu wake au ikitoe. Ndiyo maana serikali isiyowasikiliza wananchi hawapaswi kuisikiliza.

Serikali isiyotekeleza ahadi zake haiwataki wananchi na wananchi hawaitaki. Kwa nini wasiiambie serikali ifunge virago mapema?

Au wanaogopa kusema hata ukweli? Kwa nini wasiseme 'enough is enough' na upuuzi huu wa kungoja mtu afanye upuuzi wake miaka mitano ukakoma?

Haya hakika yangekuwa mapinduzi mapya ambayo yangesaidia nchi nyingi toka kwenye uvivu wa kufikiri. Ila serikali ya Jakaya inawajali sana watu.

Angalia walivyo wa ajabu badala ya kuibana serikali, wanabanana wao kwa wao kwenye nyumba chafu, shule zisizo na viwango, walimu wala madawati, hata kwenye makaburi wanabanana!

Mie naona hawa ni hamnazo. Kwa nini kikundi cha wajanja wachache tena chenye kashfa kibao kiwababaishe kama kweli wangekuwa na akili?

Kwa nini wasishuke mitaani hadi kikaeleweka? Kwa nini wasiachane na ukondoo na upunda wakatimuana kikaeleweka?

Bahati mbaya wanasalitiana. Maana hata wale waswahili wenye virungu na mbwa na makarandinga maisha yao nayo ni ya kipunda na kijungu jiko lakini bado wanatumiwa kuwahujumu wachovu wenzao!

Kweli wajinga ndiyo waliowao. Au tuseme si rahisi mbwa kumuasi aliyemfuga? Hayo tuyaache.Mie naamini kuwa kuna tatizo kwenye wabongo ambao bongo zao nadhani ni bongo lala.

Kwa nini kila mwaka wadanganywe kama mataahira? Hebu angalia wenzio walivyoshindwa kiasi cha kushikilia ,ahadi ngonjera na danganya toto!

Tena wana bahati. Wana Mkuu ambaye yuko bize na matanuzi yake.

Waswahili wapuuzi sana. Wanadanganywa mchana kweupe wanakubali! Hebu waone wale wendawazimu wanaojiita wapingaji.

Kwa nini mmoja wao asiondoe shilingi kwenye makadirio ya bajeti na genge zima likaporomoka kama kweli hawatuzugi? Lakini wana shida gani iwapo wanakatiwa pochi zito?

Je, hilo ndilo jibu?

Nisikuchoshe mzee wangu. Kuanzia leo nitakutendea haki. Sitakusakama peke yako bali nyote kuanzia Fred, Jaka, Edu, Basi, John Manywaji, Mapuya, Chwenge, Bi. Mkubwa wako na wake, Anna Abdu, Dk. Kistuli, Jona na walaji wengine hadi wawajibike.

Eti wapo wanaoandaa waraka kuwataka wote walioshiriki neema chini ya sera yako ya kula utakacho utakavyo (KUU) wajiuzulu bila kujali ni wakubwa kiasi gani. Eti nchi hii ni ya wananchi siyo yao!

Hivi hawa wana akili? Nchi siku zote ni ya wakubwa. Ipo siku nitaandaa semina za kuwafundisha kufikiri waswahili wenye uvivu wa kufikiri.

Nataka pia niwafundishe wivu wa kiume ambao siku zote ni kumchakaza mbaya wako hata kumtoa roho hasa ukimfumania.

'So' mzee jiandae usiseme umevamiwa au kuandamwa peke yako.Naomba unisalimie rafiki yako kipenzi Fred, Bi. Mkubwa na wenzake wa Economic Opportunities and Trusts For the First Lady (EOTFL).

Waambie kuna kipindi nilitaka kujinyonga. Lakini baada ya mshirika wangu wa 'bedroom' kutishia kuwa naye angejinyonga na watoto wetu wabaki wanahangaika, nimeamua kuwakabili ili nisionekane mwoga.

Hivyo, waambie bado nipo na mapambano yataendelea inshallah tutakutana. Ila mzee ningeshauri uwe mkweli. Naomba sana mzee wangu visingizio tuviweke pembeni. Ukanushe shutuma moja baada ya nyingine badala ya kujibu kwa hoja nyepesi.

Watu wanaweza kudhani umegeuka mwoga. Idumu Kasi mpya ya Uwazi na Ukweli na ukale uitwao usasa.
Naomba unisalimie walaji wenzako na uwaulize kama nao wana kinga. Maana mambo yanaanza kuingia nyongo.

Wako Mtiifu, Mpayukaji mwana wa Msemambovu, mjukuu wa mzee Wambie.

Source: Tanzania Daima Aprili 30, 2008

No comments: