The Chant of Savant

Tuesday 20 May 2008

Mbona Mkapa alizomewa zamani!


Hivi karibuni kuliripotiwa habari za kuzomewa kwa rais mstaafu, Benjamin Mkapa kulikofanywa na vijana wenye hasira tokana na uchungu kwa nchi yao .

Inasemekana. Wahusika walikamatwa na polisi. Lakini hii ni haki yao kidemokrasia na kikatiba. Je polisi na serikali wameamua sasa wazi wazi kumbeba Mkapa na mafisadi wengine dhidi ya umma? Huku siyo kupotea kwa kura zao walizoipa CCM na kuunda serikali iliyoko madarakani ikimbeba wazi wazi Mkapa?


Laiti tungekuwa na Mwanawasa wa Tanzania haya yasingetokea hata kidogo.

Hivi kati ya Mkapa na wale vijana na serikali hata polisi nani anastahili kuzomewa, kukamatwa hata kuadhibiwa?

Kama kuzuia Mkapa kuzomewa ni big deal basi serikali ingerejesha mali za umma zilizopo mikononi mwa Mkapa na watu wake ndipo kuzomea kuache.

Kuzomea kama kukieleweka siyo jambo baya; ni kuwaambia watawala kuwa sasa basi. Ni dokezo la hoja ya wananchi kuwa wameishiwa na subira na imani baada ya kuona mambo hayaendi kama walivyotarajia.

Vijana waliozomea hawakupaswa kukamatwa. Ni tamko kuwa vijana wamechoka kuwa vibaka wakati mibaka ikiendelea kutesa. Ni taarifa rasmi kwa serikali kuwa amani haiwezi kuwapo bila kutendeka haki. Vijana wa Pemba hawawezi kuacha kuzomea. Hata wale wa Buzwagi, Tarime na kwingineko hawawezi. Kama watu watazuiwa kumzomea Mkapa nafsi yake na Mungu vitamzomea.

Kusema Mkapa anastahili kuzomewa siyo kumchukia wala uchochezi. Kwa aliyofanya na jinsi alivyoyafanya, anapaswa kulaumiwa na hata kuzomewa. Hivi aliyofanya Mkapa ambayo ni ya kitoto yangefanywa na Lipumba au Mrema angekuwa wapi?


Tatizo linaloanza kuitafuna nchi yetu ni kugeuza kila kitu suala la kisiasa kiasi cha sheria kupindwa ili kulinda hata waharifu. Mkapa hana la maana la kuimbiwa nyimbo za sifa. Hana tofauti na Yuda aliyemsaliti Bwana sawa na Mkapa alivyowasaliti wananchi na Mwalimu Nyerere.

Yanayomkuta Mkapa siyo ya kwanza wala ya mwisho. Yeye siyo wa kwanza wala mwisho. Yaliwakuta afriti walioogopewa kama Surhato wa Indonesia , Nicolae Causecu wa Romania na wengine wengi.

Watu watasema. Unaweza ukawafunga miili yao . Huwezi kufunga mawazo na imani zao. Unaweza ukawapiga, huwezi kuupiga ukweli wanaosema. Hata hawa wanaowakamata na kuamuru wateswe roho zao zinawasuta.

Kama kumzomea Mkapa lingekuwa kosa na kumdhalilisha mbona anazomewa kila siku na vyombo vya habari! Au kwa vile waliozomea Masaki ni watu wasio na taaluma au ofisi ndiyo basi wapatilizwe? Tutamzomea Mkapa hadi haki itendeke.

Jibu siyo kuwakamata wanaomzomea Mkapa. Jibu ni Mkapa kuwatendea haki watanzania akarudisha mali zao alizoiiba. Hili liko wazi. Watanzania wanataka mali zao. Basi. Jibu ni serikali kuwajibika kwa umma na si kwa watawala wezi wa zamani.

Laiti vyombo vyetu vya dola vingekuwa na macho na masikio hata ubongo, vingewakamata waliowashangilia mafisadi waliotimuliwa kutokana na kubainika ufisadi wao hivi karibuni.

Yalitokea Monduli na Bariadi. Yaani watu wanalaani balaa wanakamatwa na kuachwa wanaoshangilia balaa! Nchi yetu inakwenda na kupelekwa wapi?

Tumekuwa hovyo kiasi hiki! Tumefikia kwenye umbwa wa kumwabudia kila mwenye nyama hata kama ni ya mwenzetu! Ni hatari na aibu sina mfano.

Kwa kuwakamata vijana waliomzomea Mkapa tunataka kujenga jamii ya matutusa na mbumbumbu wasiojua hata kufikiri! Mbona kufikiri ni haki ya kuumbwa ya binadamu? Kama hatufikirii tusidhani na vijana hawafikirii kama sisi. Kama hatuoni, vijana wanaona tena mbali. Hawa ni mashujaa. Walipaswa kupewa nishani na siyo kutolewa nishai.


Mbona Wazambia wanamzomea Chiluba na hawakamatwi? Au tunataka kujenga Zimbabwe nyingine kabla hata ile ya Mugabe haijazikwa?

Sijui habari kuwa Mkapa, mkewe, mwanae, mkazamwanae, kivyele na rafiki zake waliiba Kiwira ni za kushangiliwa!

Kwanza, hawa vijana walifanya ustaarabu. Maana tulipofikia, wangekuwa siyo watoto wa amani, wangeokota mawe. Au tunangoja mawe yaseme ndipo tuzinduke kwenye usingizi wa kifisadi?

Tulizomea mawaziri waliokwenda mikoani kutudanganya ili waibe pesa zetu. Tutamzomea hata Mkapa. Ikibidi hata Kikwete tutamzomea akifanya upuuzi.

Mkapa alizoea kuwapa somo la kupenda na kujenga taifa. Yeye mkewe, wanae na marafiki zake wakalibomoa. Sasa tumfanye nini Mkapa kwa jinai hii?

Kuna hekima toka kwa katika dini ya kiislamu kuwa ukiona baya litoe kwa mkono wako. Kama ukishindwa basi kemea na ukishindwa zaidi basi chukia. Hakuna haja ya kufanya haya mawili ya mwisho kama walivyofanya vijana waliozomea baada ya kushindwa kutoa kwa mkono. Laiti tungekuwa na viongozi na siyo watawala, Mkapa na wenzake wangekuwa Ukonga hata Segerea wakilipia makosa yao .

Mkapa hana tofauti na mfalme juha aliyedanganywa na waganga (mkewe na washauri wake) kuwa alikuwa amevaa vazi la heshima wakati ukweli ni kwamba alikuwa uchi wa mnyama. Wakubwa kutokana na woga wao waliogopa kumwambia ukweli. Lakini mtoto ambaye siku zote ni malaika alimwambia yu uchi tena wa mnyama.

Hata hawa vijana wamefanya alichofanya mtoto malaika. Wanapaswa kulindwa badala ya kupatilizwa. Wamejitenga na unafiki kusifia wanapopaswa kulaumu kuheshimu wanapopaswa kudharau. Hivi Nyerere angekuwa hai Mkapa angekuwa na hali gani jamani?

Nyerere alituachia kujiamini ambako kumeonyeshwa na vijana waliozomea. Tukiwazomea watenda maovu wanaozitumia ofisi na taasisi zetu kujineemesha kesho wajao wataona aibu. Na kuzomea ni mwanzo wa kutoa kwa mkono. Hivyo ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono maana nchi inayonajisiwa na kuibiwa ni yao hasa vijana.

Tusingekuwa na mfumo na jamii inayoangalia tumboni ikifiria usawa wa pua vijana hawa walipaswa kupewa motisha na siyo vitisho. Huku ndiko kukomaa na kujikomboa kifikra.

Kama Mkapa angetekeleza sera yake ya uwazi na ukweli haya yasingemkuta. Vijana wanajua kuwa alichomaanisha Mkapa alipokuja na kamba za uwazi na ukweli ilikuwa kinyume yaani uongo na ufichi. Alitudanganya kwenye mikataba na kutuficha kwenye kuliibia taifa ukiachia mbali kuondoka kwa kificho wakati aliingia mchana kweupe.

Mkapa ni mmoja wa marais wa Afrika waliofeli sana kiasi cha kuwaacha wananchi kwenye utumwa mikononi mwa wawekezaji wake alioshirikiana nao kuliibia taifa. Mbona Mkapa hajitetei hadi ageuke kichanga cha kulindwa na mama yake kila uchao?

Huyu siyo Mkapa tuliyenadiwa na Nyerere. Maana Mkapa wa Nyerere alikuwa Mr. Clean tofauti na huyu wa Kikwete ambaye ni Mr. Mess. Mkapa wa Nyerere asingezomewa wala kuishi maisha ya kujificha ficha. Au ni yale yale ya kipya kinyemi japo kidonda?

Mkapa niliyemjua enzi hizo ni tofauti kabisa na huyu wa sasa. Nani atamheshimu Mkapa aliyetengeneza EPA-Ballali na Net Group solution madudu yaliyoiingiza nchi yetu utumwani?

Nani atamheshimu Mkapa aliyechafua patakatifu pa patakatifu kwa kufanyia biashara Ikulu kiasi cha kugeuka kile Nyerere aliita Pango la wevi? Piga ua linda funga, Mkapa ni wa kuzomewa ili liwe somo kwa wajao na waliopo kama hawana nia mbaya na nchi yetu. Kuzomewa kwa Mkapa ni funzo kwa Kikwete kuwa yaishapo madaraka kila jiwe hugeuzwa na zawadi hutolewa.

Yanayompata Mkapa ni matokeo ya kutoona mbali na ulafu na ufisi visivyopaswa kutendwa na binadamu tena kiongozi wa watu.


Source : Dira ya Tanzania Mei 20, 2008.

No comments: