How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 14 May 2008

Ufunuo Nakula vichwa vya watu

MSOMAJI naomba unisamehe kwa utakayosoma hapa. Japo yanachukiza, yapo na yalikuwapo na yataendelea kuwapo. Tupo mpo na wapo kama mimi. Huu ni ufunuo wa Mpayukaji.

Baada ya kunusurika kugunduliwa kuwa mimi ni mwanga, nilianza kujiimbia wimbo niupendao.

"Neema neema, neema imefunguliwa. (Rudia tena mara tatu).

Hata makanisani, neema imefunguliwa
Hata misikitini, neema imenguliwa,
Hata maofisini, neema imefunguliwa."
(Rudia hadi uzimie).

Nikiwa kwenye ofisi yangu ya bei mbaya mtaa wa Makakani nikijipongeza kwa kunusurika, mara nilisikia sauti ikiniita tena kwa mitusi.

Ilisema: "Ewe uitwaye mtukufu mchafu, mtakatifu shetani, juha wa majuha na mbaya wa wabaya, japo umejaliwa sura nzuri na kauli tamu za kuwapumbaza watu wangu, u mchafu upaswaye kuchomwa kama kibaka."

Nikiwa nimechanganyikiwa na kuchukia Maana mimi mtu mkubwa, mara sauti inaendelea.

"Japo wajoli wako hawajui kuwa unakula nyama zao hasa vichwa na mioyo kwa vile ubongo ni mtamu, sisi tunajua kuliko ujuavyo. Tazama uroho na tamaa yako vinazidi kuwamaliza watu wangu.

Hata huo unaokunywa kwenye bilauri ukijipongeza siyo mvinyo bali damu ya wajoli wangu. Kumbuka. Siku zako zinazidi kuisha. Kwani u machukizo ya machukizo na kufuru ya kufuru. Unajisifia ufalme wa majuha kiasi cha kunisahau mimi! Tubu na kulia. Kwani zako zinakwisha."

Nilikaa vizuri ili nisikie ufunuo huu. Sauti iliendelea. "Japo wao wakuita mtukufu, twakujua wewe ni El-janabi baba wa machafu. Japo wajoli hulia haki kwao, wewe ni dhulumati mkuu wa madhulumati. Unavuna usipopanda na kula bila kufanya kazi. Kazi yako ni uongo, uuaji na dhuluma. Tazama wajoli wangu wapumbavu wanavyokuimbia kwa vinanda na vinubi wasijue wewe mla nyama yao!

"Umenawiri kwa jasho na damu vyao.Umewapumbaza kwa kauli tamu ilhali ndani ni machukizo. Huna tofauti na kaburi ling’aalo juu ndani likafumbata uoza. Waonekana nadhifu kwenye suti za bei mbaya. Jua u uchi wa mnyama sawa na kichwa na roho yako. Wajoli wangu wamefanya makosa makubwa karibu na machukizo kujikabidhi makuchani mwako.Mbona kiongozi na mwalimu wako Musa hakuwa fisadi? Alikusomesha na kukufundisha vita. Ajabu umegeuza ujuzi wake kuwamaliza watu wake!"

Niliinuka kwenye kiti changu cha enzi kutaka kukimbia lakini miguu ilikosa nguvu huku moyo ukinienda mbio. Nilijistukia nakaa huku sauti ikiendelea:

"Huwezi kunikimbia. Mimi ni ukweli wa ukweli na nguvu ya nguvu. Nakuonya na kukupa muda utubie. Umewatesa sana watu wangu. Unawanyonya damu. Unaoga jasho lao. Unawakoga na kuwahadaa. Tazama maisha yao yamekosa maana kama yako.

"Usijiinamie. Tia akilini. Zako zaisha kama hutaacha kula nyama za watu. Naona mikono yako laini. Haijawahi kushika jembe. Haijawahi hata kufungua mlango. Unalishwa kama kupe. Hata huo mvinyo ulio nao mezani umewekewa na kigori utakaye kumharibu. Huna tofauti na chawa alalaye maungoni na kuvaa za wenzie. Huna tofauti na mjusi ajivuniaye mahekalu ya wenzake.

"Huna tofauti na panya agugunaye kila kitu. Hakika umekosa aibu. Huna tofauti na kenge aionaye mvua akakimbilia mtoni. Tazama. Unadhani una siri? Tazama unavyojidanganya kwa kuwahadaa wajoli wangu. Hata namba yako ya mauti nakupa. Ni 521977.

"Usiangalie juu. Huwezi kuniona. Unajiona mjanja. Wajoli wangu wanapokuabia badala ya kukulaani! Wazidiwa hata na sanamu! Unazuzuliwa na nyimbo tamu na vinanda unavyopigiwa na wale ulao nyama zao! Uliokwisha kula wewe na mbweha na mafisi wenzio wanatosha. Zamu ya kuliwa wewe imefika. Pepo uliyojitengenezea itageuka jehanamu yako. Ukuu uliojikatia utageuka udhalili wako. Sifa ulizolewa zitageuka aibu yako usipotubia."

Niliamka tena kutaka kuukimbia ukweli huu. Lakini miguu tena uliingiwa na ganzi ikawa kama vijiti. Sauti iliendelea: "Unaonekana umenawiri kwa nyama za wajoli wangu. Umenona kama paka wa dukani au yule nune mdudu wa zizini. Zako zaisha. Kaa ukijua na kukumbuka. Kama kipanga unawala hata vifaranga. Huna kesho wala jana. Huna mbele wa nyuma zaidi ya maangamizi.

"U mbaya kuliko Delila. Ni machukizo kuliko Nabkanezza mtenda machukizo. Umejizungushia mainzi mafu yakupumbazo huku yakifaidi uoza na harufu ya mizoga mlayo. Mnanuka. Kwa inzi mwanukia. Umekula mioyo ya wajoli wangu ukibakiza miili iliyooza! Maskini wakuita mchungaji wakati mchinjani.

"Wanakuita mkombozi wakati mkomozi. Wanakuita tegemeo wakati angamio! Wanakuita kimbilio wakati anguko. Wanakupenda unawachukia. Wanakuheshimu unawadharau. Wanakutegemea unawaguguna! Wewe ni hovyo kuliko pumba na uvumba. Ni hovyo kuliko kinyesi. Kwani jana kilikuwa chakula."

Nilijisogeza vizuri na kuendelea kusikiliza: "Nikimaliza utoke nje ukayatazame majani. Uyaone yalivyonawiri. Baadaye jikumbushe yanavyonyauka wakati wa kiangazi.

Ukitoka kayatazame makaburi. Jikumbushe waliomo walikuwa nani? Kuna mitume na manabi, vibaka, watu wema na vichanga. Hata tai asifikaye kwa kuruka ipo siku mbawa zake hugoma kupaa akaishia kuwa uoza. Je wewe ni nani?

"Litazame jua lichwapo na ulikumbuke liwapo ukaingia usiku. Yakumbuke masika na kiangazi. Jikumbushe kila kitu unikumbuke na kujikumbuka huku ukikumbuka ubaya uliokwisha kuutenda kwa wajoli wangu.

Hata yale mayai yatakuwa jogoo na jogoo alikuwa yai la jana. Je jogoo aweza kuyacheka mayai? Sungura na ujanja wake umemfikisha wapi? Angekuwa mjanja angeishia kuwa hayawani? Na je, kifukuzi hufukua mashimo mangapi asiishi humo? Busara ni tunu waliyoikosa wengi. Ujinga ni manukato ya wapumbavu. Sifa ni maangamizi ya majuha. Apendaye sifa huichagua aibu asijue.

"Mkunga baharini hujiona mfalme asijue aimilikiye bahari, je, mkunga si nyoka hata aitwe samaki? Mkubuzi husafisha mahali akabaki kuwa mchafu! Swala na mbio zake hambebi kobe. Hata kobe na nyonde nyonde zake hufika atakako hata kama kwa kusuasua. We juha."

Nilishtuka na kughafilika nisijue la kufanya. Sauti iliendelea: "We juha wa majuha marhuni wa marhuni ujipaye ushufaa usijue u dhaifu. Nani aweza kuyamaliza malimwengu? Nani aweza kuwa yeye wakati wote kama si kitambo kidogo. Acha kula nyama ya watu wangu. Acha kuwahadaa wajoli wangu. Unajidanganya ukidhani unawandanganya. Wayajua ya kesho?

"Hata uwaite watabiri, huwezi kujua lijali nukta moja ijayo. Sasa kwanini kushangilia matanga ukidhania harusi? Toka mbele zangu ukagange madonda yako. Toka ukajitakase na kuacha kula nyama ya wajoli wangu. Toka. Ila nyama ya mtu tamu hasa vichwa."

Ghafla nilistuka nikiwa nimelowa jasho. Ah kumbe naota!

Source: Tanzania Daima Mei 14, 2008.

No comments: