How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 30 September 2008

Uhuni, ufisadi na somo tokana na Mbeki

Wasomaji wangu wengi huwa wananiona kama mshambuliaji. Kwao huwa sioni jema la mtu. Kama huna jema kwanini mimi nikutengenezee jema ili iwe nini? Mimi siyo mwandishi changudoa kujikomba kwa wakubwa.

Safu hii leo inakuja na sifa za kweli za shujaa ambaye anaondoka madarakani akiwa anang’aa ingawa amefanyiwa uhuni na mafisadi nchini mwake.


Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mvuyelwa Govan Mbeki, mpambanaji wa muda mrefu dhidi ya ubaguzi wa rangi hakuwa mtu mbaya kabisa. Ukiachia mbali kuwa kutojua kilichokuwa kinaendelea nchini na chamani mwake, anaondoka akiwa msafi na shujaa wa kuigwa.

Mbeki hakuwa kupe wala mpenda madaraka kama watawala wengine vidhabi barani mwetu. Hakuwa king’ang’anizi. Ingawa alionekana kulewa madaraka sawa na walevi wa madaraka wengine, hakuwa fisadi. Rejea kuondoka bila kuhusishwa na uchafu wowote kwa muda wote mrefu aliokuwa madarakani.


Ingawa ameondolewa kihuni, Mbeki atabaki kwenye vitabu vya historia kuwa angalau hakupend ufisadi. Alimtimua kazi makamu wake wa rais Jacob Zuma kutokana na tuhuma za kushiriki ufisadi. Lilipotokea hili, Mbeki hakuwa na cha mwenzetu au atataja siri zetu. Aliweka nchi mbele kuliko chama huku akiongoza kwa kuwa mbele badala ya kufanya hivyo kwa sanaa na ujanja ujanja.

Ingawa anashutumiwa kuwa aliingilia kwenye kesi ya ufisadi inayomkabili hasimu wake Zuma, bado ukweli uko pale pale kuwa Zuma ni fisadi na hata asherati aliyewahi kukiri hata kutembea na binti wa rafiki yake tena muathirika.

Cha kushangaza ni jinsi taifa hili tajiri barani linavyoweza kumtosa msomi na mtu msafi aliyetoa mchango mkubwa kwake likamkumbatia mtu wa darasa la nne tena mwenye kunuka kila kona!

Changamoto ni je huyu msanii ataweza kuunganisha chama na nchi akiweka mbele maslahi ya nchi badala ya tamaa yake ya ukwasi na madaraka? Je huu ni mwanzo wa kugawanyika kwa chama kikongwe kwenye mapambano dhidi ya dhuluma cha African National Congress (ANC)?

Hata hivyo, kama kweli Mbeki aliingilia kwa namna yoyote kwenye kesi, kufanya hivi kumemgharimu sana. Ameondoshwa kimya kimya kana kwamba hana mchango kwa taifa lake! Na hakika hii ni aibu kwa taifa la Afrika Kusini siyo kwa Mbeki.

Mbeki hataisha kwenye vitabu vya historia. Ni rais wa kwanza kuondoshwa madarakani na chama alichokiongoza. Hii si kawaida kwenye siasa chafu na za kifisadi za kujuana za Kiswahili. Hata hivyo Mbeki hakutetemeka wala kulia zaidi ya kuachia madaraka ambayo yameanza kugeuka utata mtupu.

Mbeki mpigania amani na msuluhishi wa kupigiwa mfano, atakakumbukwa kwa juhudi zake zilizoleta serikali ya umoja wa kitaifa (Government of National Unity (GNU)).


Ingawa Mbeki alilaumiwa kumkingia kifua imla wa Zimbabwe, baadaye alijua kosa lake na kuamua kuwasuluhisha Mugabe na hasimu wake waziri mkuu Morgan Tsvangirai.



Hata hivyo Mbeki anaondoka aking’ara kama nyota huku ukweli ukingoja kuchukua nafasi yake. Maana aliyemfanyia uhuni naye atafanyiwa. Kwani imenenwa: aishiye kwa upanga atakufa kwa upanga. Mbeki kama binadamu anaweza kusikitika hata kujenga chuki. Lakini ukweli ni kwamba wealiompindua ingawa wameidanganya dunia kuwa walitanguliza maslahi ya nchi, ukweli ni kwamba walitanguliza maslahi ya Zuma ambaye kimkakati na kila namna hana jipya wala ajenda kwa taifa. Atapata wapi ajenda wakati yu fisadi anayenuka ukiachia mbali kuwa kihiyo?

Ukichunguza ni nani ametanguliza nchi na maslahi ya binafsi, utagundua kuwa Mbeki ametoa funzo kubwa kwa bara zima la Afrika kuwa madaraka ni wingu la kupita sawa na nguo ya kuazima. Wenye madaraka wakiyataka wape.

Mbeki amejitofautisha kuwa si mtu tegemezi ima wa kujikomba kwenye chama au kutegemea mitandao kama wengine wafanyavyo. Ameacha uchumi imara ukiachia mbali amani. Amejitahidi kuukuza na kuulea uchumi ambao waliompindua wamekuwa mstari wa mbele kuuhujumu.

Ingawa uhuni aliofanyiwa Mbeki unasikitisha, Afrika inapaswa kujifunza somo moja kuu. Kuwa kuna haja ya kuanza kufikiria kuwa-recall watawala waovu na wabovu waliotamalaki barani kwetu.

Huu ni wakati muafaka kwa vyama tawala vya Tanzania Uganda na Rwanda kujifunza kitu. Kwani vimeziteka nchi zao na kuwang’ang’ania viongozi wabovu na mafisadi chini ya dhana mbovu za uwenzetu.

Mbeki angekuwa king’ang’anizi angeweza kutunisha misuli hata kukataa kuachia madaraka. Alikuwa na watu wengi kwenye serikali yake waliomuunga mkono na kumpenda. Rejea kujiuzulu kwa mawaziri 11 na makamu wa rais hata walipoombwa waendelee kuwamo serikalini.

Mbeki anaondoka akiwa mweupe na msafi. Hakujilimbikizia mali wala kushirikiana na wafanyabiashara wezi kama kwenye nchi zetu. Wala mkewe hakuwa na NGO kama ilivyo sasa kwenye nchi nyingi ambapo wake wa wakubwa ni wezi wakubwa kupitia NGO zao za uongo.

Mbeki ameondoka bila kuacha utata kama ilivyowahi kutokea hapa kwetu ambapo rais mstaafu anashutumiwa licha ya kufanya biashara akiwa ikulu na kujilimbikizia utajiri lukuki, anadaiwa kujitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao serikali ya sasa imeshikwa hata kigugumizi kutoa maelezo. Rejea kushindwa kuwataja wamiliki wa Kiwira ahadi iliyotolewa mbele ya kikao kilichoisha cha bunge na waziri mkuu na waziri wa nishati na madini. Kulikoni hapa? Je huu nao siyo uhuni? Je hawa siyo wanaopaswa kuwa re-called?


Uhuni na unyang’au aliofanyiwa Mbeki ingawa unaumiza, unapaswa kutoa somo moja kuu kuwa kung’ang’ania madarakani iwe ni kwa nguvu ubabaishaji au usanii ni masuala yanayopaswa kupigwa buti.

Mbeki umeondoka ukiwa shujaa kuliko ulivyoingia madarakani. Kazi yako pevu imekoma. Tunangoja kuwaona wahuni waliokupindua watachangia nini zaidi ya kubomoa mema uliyofanya. Tanzania tuna uzoefu na hili. Yako wapi mema aliyoacha Nyerere?

Leo wahuni wanaweza kujiona washindi. Kesho itawafichua. Tuulize. Yako wapi matunda ya ushindi wa Tsunami na safari ya kwenda Kanani vilivyogeuka kuwa vitendawili. Ulilza tena. Yako wapi maisha bora kwa kila mwananchi?

malizia. Je tumepambana na ufisadi zaidi ya kuupamba kiasi gani? Kuna mambo ya ajabu. Nani angeamini kuwa paka angepewa maziwa ayalinde? Imetokea ambapo katika chama fulani watuhumiwa wakuu wa ufisadi wameteuliwa eti kuchunguza ufisadi.

Imetokea ambapo vigogo fulani wa taasisi nyeti waliotuhumiwa kwa rushwa na ufisadi unaonuka waliteuliwa kuchunguza kashfa ya EPA. Imetokea ambapo wezi wakuu wameteuliwa hata kuwa wawakilishi wetu nje.
Nenda salama na kapumzike Thabo Mvuyelwa Govan Mbeki.
Amandla.

Chanzo: Dira ya Tanzania Septemba 30, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

Awesome!!!! Aiseee sio mchezo!! Kabla ya kusoma hii kitu nilikuwa namuona Mbeki muhuni lkn maamuzi yake ya mwisho nimeanza kuona yamesimama!!!
Nimekubali aticle hii kuwa iko makini.
Anony.