KUTEULIWA Endelea Chenga na Chama cha Maulaji na Mafisadi (CCMM), kuchunguza uovu na uoza wakati yeye ndiye mkuu wa genge la maangamizi la uchafu na uovu kwenye kaya.
Yaani wanadhani sisi ni wapuuzi kama wao? Wanadhani tumesahau kuwa Chenga aliiba njuluku zetu na kuzificha kisiwani kwa mother kule Uingilishi?
Kweli vibaka ni wepesi wa kusahau wakidhani nasi tutasahau na kusamehe kama alivyofanya mkuu hivi karibuni. Eti bila aibu alisingizia haki za binadamu utadhani wanakaya wadanganyika siyo binadamu!
Watu walishangaa kuona hata mkuu akimwaga chozi la mamba eti kumruhusu kijana Mapepe kukata rufaa wakati aliishanyongwa! Huu ni ushahidi wa usanii ambao wengi tumekuwa tukinyooshea kidole. Sijui nani anamdanganya nani katika upuuzi huu?
Ajabu, la pili katika wiki iliyopita kwenye kaya yetu Tanzia ya Wadanganyika ni kuokoka kwa jambazi Tunituni wa Makapu aliyetangaza kuwa atakuwa akijihusisha na mambo ya Sir God wakati tunamdai njuluku na miradi yetu kibao aliyoiba na nkewe aitwaye Annae Binti Tamaa Makapu. Hawezi kuokoka akabaki na Kiwila.
Upuuzi huu unanikumbusha kisa cha Paka na tasbihi ya vichwa vya dagaa. Hakuna tofauti na kitubio cha nyani kuacha kula na kuiba mahindi. Rejesheni mali zetu kwanza ndipo mtangaze upuuzi wenu wa kuokoka.
Hivi ni kwa nini kila kibaka siku hizi anakimbilia kwenye dini kama yule fisadi Rost tamu wa Laziz? Je, huu si uvivu wa kufikiri na ufisi wa viongozi wa dini wanaokumbatia fisi hawa wanaoisumbua kaya yetu?
We kibaka mkubwa rejesha njuluku zetu na ule mgodi wa kuchimba makaa ya mawe kule Kiwila.
Jambazi mwingine wa zamani aitwaye Freddie Sumuye eti kumtetea kijana mapepe akashindwa kukemea majambazi wenzake kina Eddie Luwasha, Emmie Mpimbi, Yusufa Makambafu na Kimdunge Ngumbaru mwehu.
Kwanza huyu anadaiwa kukopa mashirika ya kaya njuluku ambazo hakuzirudisha. Pili ilidaiwa na mchungaji tapeli, Chiristofu Mtu kula kuwa amejilimbikizia mimali kibao ya wizi.
Hajawahi kujibu! Jibu tuhuma kwanza ndipo uchonge kumtetea Mapepe. Au ni yale ya machozi ya mamba na mchawi kumlilia mtoto aliyemuua na kumla nyama?
Wanuka jasho kuendelea kuingizwa mkenge na Nistori Nguru aliyewahadaa kuwa alikunwa na kuizimia hotuba uchwara ya jamaa kiasi cha kuachana na mpango wa kugoma ambao nilipanga kuutekeleza mwenyewe hivi majuzi.
Sasa nasema tena kwa kinywa kipana. Wafanywa kazi si mabwege kama nyinyi. Lazima waandamane na kugoma ije mvua au jua. Huwezi kujua. Huenda na wafanyakazi punda ni mabwege kiasi cha kuendelea kufa na tai shingoni. Mei simo nshasema zamani.
Ajabu, jingine ni kurejea kwa wanakaya toka Uchina wakiwa na medali zote za ulaji mahanjumati huko nao ni muujiza ingawa umekuwa ukijirudia kila mwaka.
Naambiwa walishindwa kwenye michezo yote lakini wakashinda kwenye kubukanya, kushangaa na kujinoma kule Beijing. Hawa watalii uchwara sitawaongelea sana. Maana walitia aibu sina mfano. Ingekuwa Uropa mbona wangezamia wasirejee kwenye likaya lililozamishwa na ufisadi.
Muujiza mwingine tulioshuhudia tukabaki bila kuamini ni waliwaji waliotoa kura wakawapa walaji kula kuzidi kuvumilia ujambazi wa Richmonduli na EPA.
Niulize kwanini mwizi Luwasha aliyetimliwa kutokana na wizi anaendelea kulipwa njuluku za kustaafu wakati alitimliwa na Son of Kyembe? Kwa nini asipelekwe lupango akanonihino kwenye debe au mtondoo? Au ni kwa vile ni beste wa Chekacheka?
Kaya hii kweli ya mataahira. Jitu linakwapua mabilioni bado linaongezewa maulaji mengine kwa kisingizio cha likatiba viraka na uchwara. Kama nyie mmeridhia mie simo na wala sitakuwamo hadi nazikwa.
Luwasha ameuwasha kujisafisha baada ya kusafishwa na chama cha majambazi. Amewahonga wahariri na wana habari kanjanja kama Deiwaka Balila Mbweha, ambaye anaendesha gazeti la fisadi Rostitamu la Rau. Changudoa huyu wa kimaadili amejitoa mwili na roho kuhakikisha anashiba mabaki ya uoza wa mafisadi.
Hata changu ana nafuu. Dume zima linatumiwa na kujikomba utadhani halina ubongo! Hata kama Balila kasomeshwa na mafisadi awatetee, ukweli ni kwamba hajasoma kitu wala kuelimika.
Afadhali angerejeshwa vidudu. Maana usomi siyo kutumia makamasi kufikiri kama afanyavyo. Bahati mbaya, kama changu huyu ana watoto ajue basi anawaharibu.
Nao watakuwa vyangu kama yeye. Hasara namna gani? Au ni yale yale ya Silver Rwamunyama changu wa machangu, msemaji wa mkuu wa machukizo?
Kwa haya nipayukayo wapo wanaoweza kudhani nawatukana wanakaya. Anayeona nawatukana wana kaya anieleze ni kwanini wameshindwa kulianzisha kikaeleweka?
Ni kwa nini wananunua magazeti ya umbea kama Rau? Yaani wanapoteza njuluku zao kusoma sifa za mafisadi! Gomea magazeti yote ya mafisadi muone kama hawatadondoka kama kupe kwenye mgongo wa ng’ombe. Nguruwe ni nguruwe hata ukimpaka lipstick anabakia kuwa nguruwe.
Kuonyesha kaya ilivyo na watu matutusa, hebu angalia mafisi na mafisadi wanavyozidi kufichuana huku umma ukinenua. Juzi ulifichuliwa ujambazi wa tapeli mmoja chiriku wa kuwaimba wenzake asijue yake yanajulikana bali watu wanalimbika.
Nani alidhani Joni Kombo wa Kombahaha angekuwa fisadi tena wa kuiba njuruku za wanuka jasho wanaokesha kama majogoo wakiumiza makoo yao majukwaani? Ajabu jingine, eti mgosi Yusufa Makambaye anasimama na kuapa kuwa atamtoa mtu udenda hasa yule aliyevujisha uchafu huu? Kwani kutapisha uchafu ni kosa jamani?
Huyu mgosi naye sijui kaingiliwa na nini? Kwa Mapepe na Luwasha anakinga kifua! Kumsafisha kibaka Luwasha, yumo. Kunani mgosi kutumiwa kama dodoki au nawe umekatiwa? Nani anajua? Zee wewe una nini au ni yale ya Kimdunge Ngumbaru Mwehu –mtu mzima hovyo?
Kwa vile Kombahaha ni jirani yetu huenda ataelewa busara ya methali hii, ‘Chikomekome cha mkuyu, mkati muli nyerere’ maana yake siyo kila ving’aravyo ni dhahabu.
Kama Kombahaha alikuwa hajui kuwa watu wanamdeku, basi aambiwe. Tunajua alivyoshirikiana na kibaka wa Malawi Bakuli Miluzi kuubia umma wa Wamalawi maskini kiasi cha kuibuka na shule mbili huku akiwa kihiyo.
Joni, acha utoto we mtu mkubwa sasa. Pia elewa watu wanakujua kuliko unavyojijua. Rudisha njuluku za wachovu uendelee kula za huyo mjinga wa Kiyao.
Ajabu jingine la wiki hii ni kuumbuana kwa mimama mizima tena wake wa vigogo wa kiama na kaya hii. Nani alijua kuwa waziri Lion na mama Jena ati Kahame wangevuana nguo hadharani!
Huu ulaji wa dezo una mambo. Yaani waume zao walikula kaya hadi wengine wakawa wanajipaka piko kuficha mvi ili waendelee kutula hadi tukawastukia.
Walipoacha wakawaacha wake zao nao waendelee kutula hadi sasa wameanza kulana! Jamaa yangu hupenda kuziita nafasi hizi za nguo za ndani sawa na zile wanazotoleana roho kina Mpimbi na Mapepe.
Sisi tunazidi kuwaombea mbomoane. Maana ugomvi wa kunguru neema ya nzige. Adui yako muombee njaa. Nasi tunawaombea nakama. Muendelee kuvuana nguo hadharani hata kutiana midole. Bado Annae Fisadi Abidullah na vitisho vyake uchwara.
Ajabu la mwisho, ajabu jingine ni waziri Bill Ngereza kukiingiza kijiwe cha Idodomya mkenge kwa kushindwa kuwataja wezi wanaomilki mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwila. Hivi tutaendelea kugeuzana mabwege hadi lini bila kuchenjiana?
Ajabu funga kazi, ni kufungishwa virago kwa rais Thabo Mvunyelwa Mbeki wa Bondeni baada ya chama chake kumuona analeta gozi gozi na kupakaziana. Nilitamani ingetokea Danganyika.
Wenzetu wa Bondeni usipotimiza matarajio yao wanaku-recall kama bidhaa mbovu. Je, na wana kaya watajifunza hili toka Bondeni? Nani anajua?
Kazi kwenu tia akilini.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 24, 2006.
No comments:
Post a Comment