Hakuna uzembe uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi kama baadhi ya maamuzi yake tata na ya kuchukiza.
Uamuzi utakaoigharimu wa hivi karibuni ni ule wa baraza la umoja wa vijana wa CCM kumvua uanachama Nape Nnauye. Ingawa bado ni mapema kutabiri, kuna kila uwezekano kuwa maamuzi mengi ya CCM likiwemo na hili unazidi kuianika kwa wananchi kiasi cha kuichoka na kuichukia.
Angalia Nape anavyozidi kuichanganya na kuigawanya CCM. Vigogo wake akiwamo rais Jakaya Kikwete wameishaanza kumuunga mkono dhidi ya vigogo wenzao kama katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Edward Lowassa na Emanuel Nchimbi ambao wanalalia upande wa ufisadi kulingana na tuhuma alizotoa Nape.
Hakuna ubishi kuwa mradi wa ujenzi wa jengo la umoja wa vijana una kila harufu ya rushwa. Kwa watu wanaochukia ufisadi, kilichopaswa kufanyika siyo ‘kumshughulikia’ na kumpatiliza mtoa shutuma bali shutuma zenyewe.
Ila kwa vile shutuma alizotoa Nnauye zinawahusu wateule wasioguswa wa chama kama Lowassa,Nchimbi na wengine , hili halikufanyika na saa nyingine halitafanyika. Litafanyikaje iwapo chumo litokanalo na jinai hili linaishia kwenye mitandao tawala ndani ya chama? Rejea kuchunguzwa kwa mawaziri Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha huku mhusika mkuu Lowassa akiachwa baada ya ‘kusafishwa’ na kamati kuu ya Chama chini ya uenyekiti wa rais Jakaya Kikwete. Rejea kutoshitakiwa kwa wezi wa EPA na Richmond. Rejea serikali kupokea pesa kinyume cha sheria.
Kama serikali na CCM visingekuwa taasisi fisadi, hakika Lowassa na wenzake wangekuwa gerezani huku wakiwa hawana hata chembe ya nyadhifa. Kuonyesha CCM na serikali yake vilivyo hatari, Lowassa bado eti analipwa mafao ya kustaafu. Je Lowassa anastahiki kulipwa mafao haya? Je Lowassa alistaafu au alifukuzwa?
Kwa watu waliojua jinsi katibu mkuu wa CCM, Makamba alivyomkaripia na kumdhalilisha Nnauye, walijua hatima yake bila shaka. Je kwa namna hii CCM inajijenga au inajibomoa? Je wananchi wanaonaje na kuchukuliaje jinai hizi? Je hili ni onyo kwa yeyote anayejua ufisadi unaowahusisha wateule kuwa atapatilizwa kama ilivyotokea kwa Nnauye? Je huu siyo unafiki wa wazi unaopingana na dhamira ya maneno ya rais Kikwete hata katibu mkuu wa CCM Makamba kuwa wenye ushahidi dhidi ya mafisadi wawapelekee?
Nani atapeleka ushahidi iwapo anajua fika utatumika kummaliza badala ya tatizo? Christopher Mtikila analijua hili fika. Alipomtuhumu waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye kujilimbikizia utajiri utokanao na kuubia umma, alianza kuandamwa na Takukuru!
Kuonyesha kuwa mchezo huu wa kupatilizana na kulinda mafisadi na uchafu kwa CCM haukuanza jana, rejea jinsi katibu mkuu wa zamani wa CCM Horace Kolimba alivyokolimbwa baada ya kudai chama kimepoteza mwelekeo.
Unaweza kurejea pia kwenye sakata la EPA na Richmond ambapo Dr. Willbroad Slaa ameundiwa kila kashfa na mizengwe. Kisa? Kufichua ufisadi kwenye list of shame ambamo hata rais Kikwete mwenye anahusishwa na hajawahi kukanusha.
Je mpaka hapa CCM bado ni chama cha kumkomboa mtanzania au kumzamisha? Je mpaka hapa mafisadi hawajawa na ubia kwenye serikali na chama? Wana propaganda uchwara wa chama na serikali wanaweza kupinga vikali shutuma hizi. Lakini matendo yao yanasema kwa kinywa kipana kuliko ghilba zao. Je huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM?
Tukimuangalia Nape na ujana wake, kufukuzwa kwenye umoja wa vijana ni onyo kuwa ama anyamaze apotee kisiasa au aendeleze mapambano wamkolimbe. Je Nape atangoja hili iwapo ana mifano safi kama ule wa Kolimba? Ingawa Nape kalelewa ndani ya chama na kwa pesa ya chama, anapaswa kung’amua kuwa chama cha sasa na kile cha nyakati za baba yake ni tofauti. Wakati ule chini ya Mwalimu Nyerere chama kilikuwa chama kweli na siyo kiama kama sasa. Kilikuwa na mwelekeo lengo na ithibati ya kuwakomboa watanzania.
Lakini baada ya Nyerere kuondoka na kila kitu cha maana ndani ya chama kiliondoka. Rejea kufa kwa Nyerere akilalamika kuwa chama chake kimetwaliwa na wafanyabiashara wachafu kama akina Jeetu Patel na wengine wengi ambao wamefikia hata kuwapenyeza watoto wao kuwa wabunge ili kulinda uchafu wao. Rejea chama kilivyomsafisha Lowassa huku kikimsifia rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe wakati walitenda makosa tena makubwa kwa uchumi wa taifa.
Rejea kutajwa moja kwa moja kwa CCM kwenye wizi wa EPA na ujambazi wa Richmond. Rejea CCM kushindwa kutoa maelezo ilipopata pesa ya kuhonga kwenye uchaguzi ulioiingiza serikali ya sasa madarakani.
Nape kama kweli ana uchungu na nchi hii, anapaswa kutafuta chama kingine cha upinzani na kujiunga nacho. Vinginevyo anazidi kuhatarisha maisha yake. Wezi anaopambana nao hawana huruma. Ni wanyama kuliko wanyama.
Inapaswa Nape ajue. Kama anafukuzwa na kukaliwa vikao yeye badala ya watuhumiwa wenyewe anangoja haki itendeke wapi na vipi ndani ya chama ambacho kilikwisha kujitofautisha na uwajibikaji na uongozi bora?
Leo mguse mtu kama Mkapa na Mkewe kuhusiana na uchafu wao wakiwa madarakani. Utaundiwa kila mizengwe na kupatilizwa. Ukimgusa na kubakia wewe sharti uwe nje ya chama. Rejea anavyoandamwa mbunge wa Vunjo aliyevalia njuga uchafu wa Mkapa na mkewe na marafiki. Rejea waziri wa nishati na madini na waziri mkuu Mizengwe Pinda kushindwa kutangaza wamilki wa Kiwira inayodaiwa kutwaliwa na Mkapa kama walivyokuwa wameliahidi bunge. Wako tayari hata kuhatarisha nyadhifa zao ilmradi wasimguse Mkapa!
CCM kwa sasa ina wenyewe na wenyewe wanajulikana hasa unapoangalia serikali yake inavyoshughulikia ufisadi kwa kutoa hata misamaha kwa mafisadi.
Juzi juzi kulikuwa na tuhuma kuwa mtuhumiwa mkuu ambaye si mwanasiasa kwenye wizi wa EPA marehemu Daudi Ballali aliuawa. Nani amejihangaisha na kuchunguza iwapo wajanja wenye madaraka waliishamtumia kuuibia umma wakimuacha mchafu na marehemu?
Kuepuka kupoteza muda mwingi, ni kwamba Nape kapewa onyo. Kama ataendelea kung’ang’ania chama kilichokwisha kumchosha, yatakayomkuta huko tuendako asilaumu.
Kwenye mmomonyoko huu wa maadili na utu, Nape na wenye mawazo kama yeye wasitegemee kukibadili chama. Sana sana chama kitawabadili na watajikuta kwenye hali wasiyoweza hata kutikisa kope za macho. Nape waachie chama akina Nchimbi na Lowassa waliothibitisha kuwa wateule na maswahiba wa wakubwa wenye kunuka kama wao.
Tafuta chama chenye maana uendelee na mapambano badala ya kuyatafuta ya kuyatafuta. Jiunge na chama kingine na utumie kesi yako kama fimbo kwa waliokukataa. Wewe si wa kwanza. Dr. Slaa ni mfano wa kuigwa katika mazingira ya siasa chafu na nyemelezi kama zilizokukumba.
Wakati ukitafakari la kufanya, jirejeshe kwa yaliyomkuta Amina Chifupa alipotaka kugombea cheo ulichokuwa ukitaka kugombea asijue kina wenyewe.
Hakika CCM imeanza kujichimbia kaburi bila kujua.
Chanzo: Dira ya Tanzania Septemba 16, 2008.
No comments:
Post a Comment