KWANZA niwape habari njema zisizo njema. Siku hizi nimepata kibarua cha kuandika umbea kwenye gazeti letu la Mawazo.
Baada ya kudaka kazi hii ya kujidai ilikuwa furaha si kawaida. Mama Ndiza wangu aliangusha bonge la pilau kusherehekea mumewe kupata kazi ya heshima na jina.
Niwaonye. Mimi si kanjanja kama wale wanaojipendekeza kwa jamaa na mafisadi wenzake kwa kuhongwa vyeo uchwara visivyo na heshima kwa jamii. Mie ni Kidume jeuri kama kawa.
Baada ya kuanza kibarua ngwengwe cha kuandika umbea, nilijiona nimeula nisijue nimeliwa! Kwanza malipo yalikuwa ni kwa manati ukiachia mbali kuwa mchinjo ile mbaya. Hayo tuyaache.
Baada ya Nistori Nguru aliwaye na wakubwa kutangaza: wafanyakazi, sorry, wafanywa kazi za kipunda wangegoma, nilikuwa wa kwanza kutia nia kufanya kweli. Eti linasema lilikunwa na hotuba uchwara ya mkuu! Furaha yenu ni mauti yetu. Amekukuna wewe si sisi wafanywa kazi. Acha usanii kwenye maisha yetu na vizazi vyetu. Acha kunyonya na kunywa jasho na damu zetu.
Nakumbuka. Ilikuwa tarehe, ohoo! Nimeisahau! Hilo si ‘big deal’. Baada ya kujua tarehe ya mgomo wa wafanya kazi kaya nzima, nilijiandaa kuingia kivyangu vyangu ili kieleweke.
Nilikwenda chombingo nikakata mzinga wa pombe kubwa. Kwa vile mie ni bingwa wa ngonjera kama Cheka cheka, nilimkopa Mama Ngenge muuza ulabu na kupata tani yangu. Tangu ajue mimi ni paparazzi, ananigwaya kama ndata! Akileta gozi gozi namlipua kwenye pepa na biashara yake ndiyo bye.
Baada ya kutoka kwa mama Ngenge wa Ngwengwe nilikwenda kwa mama Ndiza wangu. Nilikwisha kuutwika. Sikumkopesha. Nilitangaza siku ya mgomo na maandamano kupinga wafanywa kazi kudhalilishwa na kunyonywa na makupe watu wenye siri kali ya kuwaumiza wenzao.
Nilipanga kugoma kwenda ofisini. Pia niliazimia kutofanya kazi yoyote isipokuwa kazi ya kugoma na kuandamana. Hata ningekuwa peke yangu. Siku hiyo nitasusa kazi zote kuanzia umbea hadi zile za usiku na mshirika wangu. We koma we!
Nikiwa na msigara wangu mkubwa, si bangi kumbuka. Nilizidi kujaza mafuta ili nitoe nishai tayari kufanya kweli.
Kwanza nilimtwangia simu bosi uchwara wangu mwenye jina kama kijumba kidogo. Nilimpa laivu kuwa nimetangaza mgomo baada ya kuona Nguru analeta gozi gozi na longolongo. Alidhani sijui kuwa amekatiwa na Chekacheka ili awatwishe mkenge wavuja jasho wa kaya. Mie siyo bwege kama yeye wala wao.
Lazima nifanye kweli. Ohooo! Patachimbika bila jembe na patakuwa hapatoshi. Na huu siyo utani wala usanii kama wao.
Nitachukua pyolilo yangu mdomoni huku sigara kubwa ikitoa moshi kama treni. Huyo nitaanza safari kuelekea Ikulu kumuona mheshimiwa.
Kabla ya kuondoka, nilikumbuka. Kuna wastaafu wa jumuiya mfu ya Afrika Mashaka waliotwishwa mkenge kwa miaka 31. Nitataka nao washirikiane nami kuwakomesha wanyonyaji wa jasho letu.
Pia nakumbuka. Kuna wajawazito wanaofanya kazi ya kuongeza idadi ya wana kaya lakini wanaonewa na manesi uchwara pale Anama, Mwanamanyala, Tekeme na kwingineko. Nao nilitaka waandamane na kugoma hata kuzaa ili tuone nani mjanja.
Pia nawakumbuka wale wazee wa mituringa wanaosafiri bure huku wenye magari wakilalamika. Nitataka waandamane kudai wanunuliwe mashangingi kama wabunge. Wanalinda taifa wakati wanaojiita wakubwa wakati ni wa hovyo ni wezi wanaotuuza kama wale wa Richmond na WEPA.
Katika kusukuti nilikuta wana kaya ni woga sana. Hivyo nimeamua kugoma na kuandamana peke yangu.
Kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu, nitaandaa hoja zangu.
Mosi, wezi wote wa WEPA na Richmond wapewe nishani za uzalendo na ushujaa na wake zao huku watoto wao wakiajiriwa kwenye taasisi zote nyeti. Kisa? Wanajenga kaya kwa kuwa na ukwasi wa kutisha ukiachia mbali kuchangia ufanisi na ushindi wa kiayama.
Pili, wafanyakazi wote kuanzia wa ndani hadi wa nje walipwe mshahara sawa bila kujali huyu ni daktari, polisi, mbunge wala rais. Kima cha chini kiwe shilingi milioni saba. Zitapatikana wapi? Kaya ina madini mengi kiasi cha kuuza kwa tani.
Hapa hatujaongelea mbuga za wadudu na wanyama zinazochezewa na wanaoitwa wawekezaji wakati ni wachukuaji. Pia kaya ni tajiri kuweza kusamehe wizi kama wa WEPA na Richmond. Una habari hata Marekani haiwezi kusamehe dola milioni 133 ukiachia mbali zile tusizozijua?
Tatu, mawaziri wote waendeshe magari yao wenyewe na yawe ‘Beattle’ si mashangingi. Na hili liwe onyo. Kama wataendelea kulega lega, tuwatimue kazi nchi ijiendeshe yenyewe.
Nne, kama tutashindwa kutekeleza mapendekezo haya, tutafute mwekezaji tumuuzie kaya tugawane kila mtu apate zake akapige ulabu na sigara kubwa.
Tano, kuanzia sasa mkuu alipe kodi pamoja na mkewe huku akilipwa mshahara kima cha chini maana hajaonyesha kufanikiwa kwa kiasi cha juu. Kwanza, anafanya nini iwapo mafisadi wanazidi kutanua huku yeye akitanua ughaibuni? Au naye tumfute kazi nchi iendeshwe na sungu sungu.
Sita, wavuta bangi wote wateuliwe kuwa washauri ili ijulikane kuwa kaya sasa inaendeshwa na walevi kuliko machizi. Wakishaliweka wanatumia uwazi na ukweli. Maana ukiona watu wanaoitwa waheshimwa wanavyofanya mambo kibangi bangi, afadhali hata ya wavuta bangi. Maana hawana muda wa kuficha ficha.
Saba, wafungwa wote waliofungwa kwa wizi wa kuku, mikufu, pochi na vitu vidogo vidogo wapewe nishani na fidia na kuachiwa mara moja huku mafisadi wakinyongwa na wawekezaji wote wafukuzwe kayani: wameshindwa kuleta maendeleo.
Nane, ofisi zote za kaya zigeuzwa mabaa na madangulo ili uchangudoa na ulevi uliojificha kwenye ufisadi ukose soko. Shule na vyuo vyote vifungwe na kugeuzwa super markets. Maana kila siku vinazalisha wasomi lakini wezi na woga.
Bangi, ukabaji, ubakaji, uongo, gongo na uzururaji vihalalishwe. Mbona akina nonihino wanalewa mamlaka na hawapigwi marufuku? Mbona mafisadi wanaikaba kaya na kuibaka na hawafungwi?
Kusema ukweli liwe kosa la jinai na mwenye kulitenda anyongwe. Hapa tutaweza kuwakomesha akina Nipe Mapepe wa Naweye. Hamkuona alivyonyolewa bila maji?
Hoja zillikuwa nyingi kiasi cha kuweza kujaa gunia. Tufupishe stori.
Baaada ya kuhakikisha hoja zangu nimeziandika kwenye bango kuuubwa nitanza kupiga mkuu kuelekea kwenyewe.
Kwanza nitapita kwenye ofisi ya Nguru niibonde mimawe huku nikimwaga mitusi yote niijuayo. Pili nitapitia kwenye ofisi yangu niwachambe wanaosalitiana wakitenda ufisadi huku wakijidai wanaupiga vita. Makanjanja wote kuanzia wa pale hadi Ikulu watanikoma siku hiyo. Nitachukua pili pili ili kama ndata watajitokeza kunikwaza niwamwagie niwaache wakilia.
Mwisho sitakuwa na msalie wala usuhuba na mafisadi. Nitakumbushia kesi zote za ufisadi kuanzia Richmond, WEPA, TICTS, IPTL, ANBEN, Fosnik, Kiwira mine, Meremeta, Deep Green Finance, MAWA, EOTF, rada na ndege mkangafu ya jamaa.
Nitamkaribisha Mapepe Nipe wa Mawe aje tuwakabili akina Richmond na vijisenti bila kukisahau.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 17, 2008.
No comments:
Post a Comment