How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 9 September 2008

Ziara za Kikwete nje hazina faida





Ingawa wapambe wa rais, Jakaya Kikwete, wanajitahidi kutuaminisha kuwa ziara zake za mara kwa mara nje ya nchi zina faida kwa taifa, kuna walakini katika hili.

Ukimuondoa rais wa Kameruni, Paul Biya, anayesifika kwa kuishi Ulaya akirejea mara kwa mara kuja nchini mwake kuchukua pesa toka benki kwa ajili ya kugharimia uharamia wake, marais Kikwete na Thabo Mbeki (Afrika Kusini) wanashika rekodi ya kupenda kufanya ziara za nje. Wananchi wamepiga kelele hadi makoo yamewakauka huku Kikwete akizidi kuwapuuzia.

Wapo wanaoshangaa marais kama hawa hupata muda wapi wa kushughulikia masuala ya kitaifa nchini mwao. Rais Kikwete hivi majuzi alithibitisha hili alipopokea taarifa ya tume ya kuchunguza wizi wa Richmond kimya kimya na kuiacha mezani kwenda nchini Marekani. Hivi ni mwenye nyumba gani mwenye busara anayeweza kwenda harusini huku akiacha nyumba yake inabomolewa na majizi asiwe mwenzao? Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani rais anathamini ziara kuliko masuala muhimu kwa taifa.

Tangu aingie madarakani, kama mtangulizi wake,
Benjamin Mkapa, aliyependa sana kusafiri, Kikwete amefanikisha kitu kimoja-kutumbua pesa ya walipa kodi maskini kwa kufanya ziara nje hadi watani wake wakamwita Mtalii. Kwa mtu mwenye uchungu kwa taifa, angalau Kikwete angewekeza sana kwenye kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa uchanguzi uliompa ushindi wa kishindo cha Tsunami kinachoanza kugeuka Tsunami kweli kwa maisha yetu. Ajabu alipata fursa ya kuzunguka nchi nzima wakati wa kampeni tena ndani ya miezi michache. Muulize ameisha kwenda mara ngapi vijijini kuhimiza ‘maendeleo’.

Kama kuna jibu ni aibu, uongo au ukweli unaouma. Alitegemewa apambane na kuongezeka kwa rushwa na ufisadi karibu katika kila idara na wizara ikiwemo Ikulu. Inaonekana. Rais, kutokana na maisha ya kifalme anayoishi, hajui kuwa nchi yetu ni maskini inayoishi kutegemea kuomba omba na kukopa. Ni kweli hawezi kujua hili kutokana na mamlaka ya kupita kipimo aliyo nayo. Yuko juu ya sheria. Laiti angekuwa anawajibika angetoa maelezo kwanini asishitakiwe kuhusiana na tuhuma za ufisadi kwenye list of shame.

Tunaambiwa. Hii ni mara ya sita tangu Kikwete kuingia madarakani. Hii maana yake ni kwamba amekuwa akienda Marekani kila baada ya miezi sita tangu aingie madarakani. Hata ukiangalia nchi zinazoongoza kuifadhili Tanzania, Marekani haimo. Je hapa kunani anachokwenda kukifanya kila mara?
Kinachoongeza shuku ya hasara ni ile hali ya watawala wetu kusafiri kama wafalme wa kiarabu ambapo huandamana na misafara mikubwa bila sababu. Kwa mfano umma umekuwa ukilalamikia kuwamo kwa mke wa rais karibu katika kila msafara. Hii inaufanya urais wa Kikwete kugeuka aina fulani ya utalii wenye hasara kwa taifa. Maana misafara hii humgharimu sana mlipa kodi maskini.

Tunapata wasi wasi na faida na kazi anazofanya rais huko nje. Kama ni kuashughulikia maendeleo mbona wenzake wa Kenya na Uganda hawasikiki wakisafiri nje mara kwa mara kama yeye?
Hapa tusipewe kisingizio cha kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (UA). Na kama hiki kitatumika kama kisingizio basi ni bora tukamwambia rais aachane na wadhifa wenye hasara kwa uchumi na maisha yetu.

Kwanini wadhifa huu uwe big deal iwapo matatizo yanazidi kuongezeka nchini mwetu huku tukijisifu kutatua ya wenzetu? Rejea jinsi tulivyoshiriki kusuluhisha migogoro ya Comoro na Kenya huku tukishindwa wa Zanzibar unaotishia usalama wa taifa na muungano wetu kwa sasa. Je huku kama siyo kuishiwa na unafiki ni nini?
Anachofanya Kikwete hakina tofauti na kile wanachofanya wasaidizi wake.

Ukiangalia aina ya magari wanayotembelea na idadi ya misururu ya magari wawapo mikoani, utaona ukweli unaotisha kuwa mojawapo ya sababu za nchi yetu kuwa maskini licha ya kuwa na utawala usio na visheni wala mipango, ni matumizi mabaya ya pesa ya umma yanayofanywa na watawala wetu.
Lazima tuseme. Maana sisi ndiyo tunaolipa kodi inayogharamia maisha ya kifalme ya watawala wetu. Lazima tulalamike ili waone ukweli. Kama wataendelea kwa jeuri kama walivyozoea basi tuwatolee uvivu kwa kuwagomea na kufanya kutawala kuwa kugumu hadi watakapowajika kwetu badala ya matumbo yao.

Kinachosikitisha na kukera ni ile hali ya watapanyaji wa fedha zetu kama hawa kutuaminisha kuwa wanaweza kutuletea maisha bora kwa kila mtanzania. Yatapatikanaje iwapo ufisadi na matumizi mabaya ndicho wanachojua? Yatapatikanaje iwapo hawawajibiki? Rais asiye na muda wa kutulia ofisini na nchini kwake yupo madarakani kwa bahati mbaya. Kutokana na upogo huu, imefikia mahali watawala wetu wanategemea kusifiwa na mataifa fadhili au benki ya dunia badala ya wananchi waliowachagua na kuwagharimia maisha yao! Rejea sifa za uongo zilizotolewa na shirika la fedha la umoja wa mataifa (IMF) kwa Kikwete kushughulikia kashfa ya EPA wakati hajaishughulikia lolote.

Naye bila kujua anapigwa vijembe alizipokea ‘sifa’ hizi kwa moyo mmoja asijue wananchi hawaoni cha kusifiwa nacho!
Hali hii ya kulegalega katika kuendesha nchi imefikia pabaya kiasi cha baadhi ya wachambuzi kufikia hitimisho kuwa Kikwete ameshindwa nchi. Bahati mbaya naye hajibu mapigo zaidi ya kufikiria kufanya ziara nje ya nchi.

Kuna haja ya rais wetu kujiepusha na maisha ya hovyo kama ya akina Mswati III ambao wapo madarakani kwa ajali na kinyume cha tararibu zote za kidemokrasia.
Kuna haja ya walipa kodi kugomea aina hii mpya ya ufisadi kwa kisingizio cha madaraka na maendeleo. Ni maendeleo gani haya yanayotegemea ziara za nje badala ya mipango, uwajibikaji, matumizi mazuri na juhudi za wananchi wenyewe? Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kwa kuomba na kuzurura nje. Unajirudia ushauri wa bure wa marehemu Nyerere wa mali mnayo lakini mmeikalia.

Urais uwe ni utumishi badala ya kuwa chambo cha kufanyia utalii na isirafu.
Tunaomba kutoa hoja. Rais Kikwete acha ziara zisizo na faida kwa taifa nje ya nchi. Iga mifano ya marais jirani ambao kwa kiasi fulani nchi zao zinasonga mbele kuliko Tanzania. Rejea Rwanda kuanza kuwa tishio kiuchumi wakati haina raslmali hata moja ya mia ya Tanzania. Wenzetu wanatucheka. Global trotting si jambo jema kwa taifa maskini kama letu. Hata marais wa nchi tajiri wanaogopa upuuzi huu. Sisi tusio na lolote tunauwezaje?

Chanzo: Dira ya Tanzania Septemba 9, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

Shukrani sana kumtandika huyu mtalii na mwizi anayelizamisha taifa letu huku akijichekesha. Nakubaliana nawe kuwa watanzania tuamke na kuzuia wizi huu unaofanywa na watawala wetu wezi.
Nimefaidika sana na blogu hii kusema ukweli.
Ingekuwa vizuri kama akina Kikwete na wenzake wangesoma na kujua kuwa mambo yanazidi kubadilika. Kuna kila dalili za alama za nyakati katika falsafa za Mhango. Kudos.