The Chant of Savant

Friday 27 March 2009

Mwakani tusichague serikali ya buibui



MDUDU buibui anasifika kwa kujenga utando wenye kuvutia. Ni mdudu bingwa wa sanaa. Ukimkuta kazini akijenga, unaweza kudhani atajenga ghorofa. Lakini mwisho wa yote hujenga wavu tu usioweza kusitiri hata maungo wala mayai yake.

Buibui hutumia utando kuwanasa wadudu wachovu kama mbu na inzi wadogo, lakini wakati mtego wake huu akiusifia na kuuona mali, wadudu kama dondora, kereng’ende na viwavi huukata wavu wake na kupeta.

Mfano huu unafanana na serikali ya sasa. Kabla ya kuingia madarakani, Rais Jakaya Kikwete aliahidi angetuondoa kwenye kadhia zilizokuwa zikitusumbua; rushwa, umaskini, ubabaishaji, kichwa maji na mengine mengi. Aliahidi ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya huku akisema serikali yake italisafisha taifa tusijue italichafua!

Aliahidi kupambana na ufisadi na wizi wa fedha za umma ukiachia mbali umaskini ambao kimsingi husababishwa na majanga tajwa. Ajabu sasa, kama buibui, badala ya kujenga nyuma tusitirike, amejenga utando (mitandao) wa jinai ulioishia kuyafanya maisha bora tuliyoahidiwa kuwa ndoto na tusi la nguo.

Wale wadudu waletao uharibifu, yaani mafisadi, wanazidi kupeta wakiubomoa utando wa buibui huku mwenyewe akikodoa macho na kutoa kila aina ya visingizio! Hii inaananisha tulikula hasara kwani mtego tuliodhania ungekamata, umegeuka dhihaka ya hali ya juu!

Ukiachia mbali kuwanasa inzi (wala rushwa wadogo), kereng’ende na manyigu yanaendelea kutuumiza huku buibui akifanya nao shirika!

Kutokana na hali hii, mwakani lazima tuje na hoja mpya. Tuchague watu safi na wenye dhamira safi ya kupambana na ufisadi na siyo kuupamba huku wakiwa wanufaika wakuu.

Juzi, ziliripotiwa taarifa kuwa pesa iliyokuwa ikitoka kuchapishwa Ujerumani, ilichotwa. Ajabu habari hii haikupewa hata uzito na vyombo vingine vya habari ukiachia mbali gazeti tafitishi la Thisday!

Kwanza, wapo wanaoohoji kwanini pesa ichapishwe karibu na uchaguzi? Na haya yamekuwa mazoea. Wasipochapisha pesa mpya, watakuja na EPA na Richmond mpya. Kila msimu wa uchaguzi ni wizi mtupu. Inatia kinyaa na hasira kuona wale tulioamini wangelinda na kuiweka nchi yetu kwenye usalama, wameibomoa na kuishia kuwa wezi wakubwa.

Niambie. Hivi CCM ina haja ya kurejeshwa madarakani bila kutukamatia na kufunga Kagoda? Je, itakuwa na kazi gani kwetu iwapo imeshindwa kumkamata Richmond na wenzake?

Nchi yetu imekuwa kama kambi ya wendawazimu au kundi la mainzi ambapo hakuna mpangilio wala matumaini. Imefikia mahali hadi walioko ndani wanasema nchi inatawaliwa kienyeji. Si kienyeji, waliogopa kusema yote. Nchi inatawaliwa kijambazi. Watu wanauawa kwa tamaa ya utajiri huku mamlaka zikija na maigizo uchwara. Jiulize, hivi vikongwe na albino wana usalama ndani ya nchi hii?

Nchi imekuwa ikiibiwa kila uchao utadhani haina wenyewe! Rejea kuendelea kutoroshwa madini yetu kwa kisingizio cha kwenda kupima mchanga. Mbona Afrika Kusini hata DRC hawafanyi hivyo? Kama si ujambazi wa kitaifa, mchanga wetu una nini cha mno zaidi ya wenzetu wenye madini?

Je, tatizo letu ni nini? Bila shaka ni kuwa na utawala mabaka uliojaa walafi na wezi watupu wakitumia madaraka kutufanyia ugaidi. Tanzania ni nchi pekee ambayo mtu anaweza kuiba na akaendelea kuitwa mheshimiwa. Ni nchi pekee ambapo watu wanaweza kuiba halafu wezi hao hao wakaunda tume za kusafishana. Rejea Takukuru ilivyojaribu kuwasafisha baadhi ya vigogo wa kashfa ya Richmond au CCM inavyopigana kufa na kupona kuwaficha na kuwasafisha akina Kagoda, Mereremeta Deep Green Finance, Mwananchi Gold na majambazi wengine.

Wako wapi akina Andrew Chenge na Idris Rashid walioripotiwa na mamlaka za Uingereza kujipatia mabilioni toka kwenye wizi ulioitwa ununuzi wa rada ya usalama?

Yako wapi maelezo yanayoingia kichwani toka kwa CCM kuwa iliasisi EPA kupata mtaji wa kuhongea wapiga kura? Ajabu mwizi anaaminiwa kuwa atamkamata mwizi!

Hivyo basi, hoja kubwa mwakani iwe ni kupambana na ufisadi kwa vitendo na si kauli za kisanii kama ilivyo sasa. Watu wanateuana kwa rushwa na kulipana fadhila huku umma ukizidi kutopea kwenye umaskini wa kunuka, halafu watu hawa hawa wanatuaminisha watatupeleka Kanani wakati wanachofanya ni kutupeleka motoni!

Ukiondoa wabunge wachache wa CCM na upinzani, Bunge limejaa wezi wanaotetea hata mambo ambayo kuku hawezi kutetea. Rejea Mbunge Samuel Chitalilo aliyethibitishwa na polisi kughushi, kumtetea Chenge kuwa hakuvunja nyumba ya mtu hivyo kuiba mabilioni na kuyaficha kisiwani Jersey si wizi wala kosa!

Tunao akina Kingunge Ngombale-Mwiru wanaotetea kila upuuzi wa CCM kwa kile ninachoamini kuwa kufurahia na kulipa fadhila za kuachiwa wachote mapato yetu.

Wapo wengi. Wameteuliwa kuwakilisha matumbo yao huku wengine wakichaguliwa na wananchi wakawasaliti na kwenda bungeni kutetea biashara za Richmond, Dowans na IPTL bila hata chembe ya aibu. Je, hawa wanapaswa kweli kurejeshwa bungeni ili wakaibe na kuhatarisha usalama wetu zaidi? Tukifanya kosa hili hatutastahili msamaha hata kidogo.

Tumejaza wachumia tumbo kwenye maofisi yetu. Hebu jiulize, kwa nini, kwa mfano Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) bado wamo kwenye ofisi za umma wakati wanatuhumiwa kuhusika na hujuma ya Richmond? Hawa wanaweza kuifanyia nini nchi zaidi ya kuiangamiza?

Ajabu serikali ile ile iliyotuaminisha ingetuvusha na kutupeleka Kanani tupate maisha bora imegoma kuwaachisha kazi licha ya kuandamwa na tuhuma hizo! Je, kuirudisha serikali hii, si sawa na kumkaribisha chatu nyumbani ili amalize watoto wako?

Tujiulize, serikali yetu ina tofauti na mbwa anayerudi vitoto vyake au fisi anayemla mwenzie?

Mwakani tusirudie kosa.
Chanzo; Tanzania Daima Machi 25, 2009.

No comments: